Wednesday, May 19, 2021

WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOPATIKANA SADC


Watanzania wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatina kwenye mtangamano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo biashara, uwekezaji na soko la bidhaa mbalimbali za Tanzania ili kunufaika na Jumuiya hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 19 Mei 2021 na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini  mwa Afrika (SADC)  lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Mhe. Prof. Mwamfupe amesema kwamba, katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SADC mwezi Aprili  1980, wigo wa fursa umeongezeka ambapo sasa Jumuiya imejikita katika kuwanufaisha  wananchi wake kiuchumi baada ya kukamilisha jukumu la kuzikomboa kisiasa  Nchi za Kusini mwa Afrika ambalo lilikuwa moja ya lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya ya SADC.

Kadhalika alisema kuwa maadhimisho ya miaka 40 ambayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Miaka 40 SADC ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahimilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia” yanalenga pamoja na mambo mengine kuenzi mchango wa waaanzilishi wa SADC, lakini pia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu Mtangamano wa SADC na faida za uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaeleza wananchi fursa zinazopatikana za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Pia aliongeza kuwa, maadhimisho haya yanalenga kuangazia mafanikio yaliyofikiwa pamoja na kuongeza hamasa kwa makundi mbalimbali kama vile wafanyabiashara, vijana, wanawake, makundi maalum na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zinazopatikana SADC.

“Leo tunaposherehekea miaka 40 ya SADC tunafungua wigo kwa wadau mbalimbali hususan wafanyabiasha na vijana kuwaonesha namna gani wanaweza kunufaika na Jumuiya hiyo kutoka ile ya kufundishwa darasani hadi SADC inayotuwezesha kupanga mipango yetu ya maendeleo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, vijana na makundi mengine. Hivyo tuna kazi kubwa moja ya kuhakikisha elimu kuhusu fursa zinazopatikana SADC inawafikia wananchi wote” alisema Prof. Mwamfupe.

Awali akizungumza kuwakaribisha Washiriki wa Kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Faustine Bee alisema anashukuru Chuo hicho kuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya SADC kwani ni heshima kubwa kwao ambayo imewezesha wadau mbalimbali kukutana na kubadilisha mawazo ya namna ya kuiimarisha Jumuiya hiyo.

Aliongeza kusema kwamba, wakati Nchi Wanachama wa SADC zikiadhimisha miaka 40 ya Jumuiya hiyo, Chuo hicho kinatambua faida za SADC kwani tayari kinashirikiana na Nchi za Jumuiya hiyo ambapo Tanzania kwa sasa inapokea wanafunzi kupitia ushirikiano huo. Alisema mfano mzuri ni ule uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji ambazo tayari zinashirikiana katika kubadilishana wanafunzi kupitia utaratibu wa TAMOSE (Tanzania –Mozambique Students Exchange Program) ambapo tayari wanafunzi kutoka Msumbiji wanasoma UDOM na Vyuo vingine hapa nchini na vivyo hivyo wapo wanafunzi kutoka Tanzania wanaosoma nchini Msumbiji.

Kadhalika alisema, Chuo hicho ambacho kinapokea wanafunzi kutoka Nchi zingine za SADC kama Comoro, Afrika Kusini, Zambia, Malawi, DRC na zingine kimejiwekea malengo ya kuingia kwenye vyuo bora 20 katika Afrika kufikia mwaka 2030. Alisisitiza kuwa, lengo hilo litafanikiwa endapo Chuo kitapokea wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi ikiwa ni moja ya kigezo  cha kupima ubora wa chuo na alitoa ombi kwa Serikali kukisaidia Chuo hicho kuongeza wanafunzi kupitia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zingine na ule wa kikanda na kimataifa.

Wakati wa Kongamano hilo, ambalo limeandaliwa kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo “Kuimarisha Amani na Usalama katika Kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu” iliyowasilishwa na Mkuu wa Chuo cha Diplomasia Mstaafu, Dkt. Mohammed  Maundi na mada isemayo          “Kuhamasisha Maendeleo na Uhimilivu katika kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu” ambayo iliwasilishwa na  Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Ajali Mustafa.

Viongozi wengine walioshiriki Kongamano hilo ni Mkuu wa Chuo cha Mipango, Prof. Hozen Mayaya, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, Dkt. Michael Msendekwa, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma anayeshughulikia Taaluma, Prof. Alexander Makulilo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Agnes Kayola. Pia, kongamano lilihudhuriwa na Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mipango na Chuo cha Serikali za Mitaa kilichopo Hombolo jijini Dodoma.


Mgeni Rasmi ambaye ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tarehe 19 Mei 2021. Kongamano hilo ambalo liliandaliwa chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi kutoka UDOM na Vyuo vingine vya Dodoma. 

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM), Prof. Faustine Bee akiwakaribisha Washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC Chuoni hapo

Mkuu wa Chuo cha Diplomasia Mstaafu, Dkt. Mohammed Maundi akiwasilisha mada kwa Washiriki kuhusu Kuimarisha Amani na Usalama katika Kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC lilifanyika UDOM

Mhadhiri Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Ajali Mustafa nae akiwasilisha mada kuhusu Kuhamasisha Maendeleo na Uhimilivu katika Kukabiliana na Changamoto za Ulimwengu wakati wa Kongamano la kuadhimisha miaka 40 ya SADC.

Sehemu ya Washiriki waliohuria Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Agnes Kayola, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, Dkt. Michael Msendekwa  na Mkuu wa Chuo cha Mipango, Prof. Hozen Mayaya 

Sehemu nyingine ya Washiriki wa Kongamano

Washiriki wa Kongamno wakiwemo wahadhiri wakifuatialia uwasilishwaji wa mada mbalimbali

Sehemu ya Wanafunzi wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Sehemu nyingine ya Washiriki

Washiriki wa Kongamano la maadhimisho ya miaka 40 ya SADC kama wanavyoonekana pichani

Sehemu nyingine ya washiriki

Waandishi wa Habari wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Washiriki kama wanavyoonekana pichani

Mmoja wa Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma akichangia jambao wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

Mmoja wa Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma akiuliza swali wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

Mwanafunzi kutoka Chuo cha Mipango nae akichangia jambo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC

Picha ya pamoja

Meza Kuu katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali



 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.