Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula
(Mb) amesema moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Rwanda ni kuimarisha uhusiano wa
Kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya
uchukuzi baina ya Tanzania na Rwanda.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amesema kuwa mbali
na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, pia ziara ya Mhe. Rais nchini Rwanda nchini
Rwanda ziara hiyo imekuwa kielelezo kizuri cha ujirani mwema, na imeweka msingi
mzuri wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili katika siku za usoni na walionesha
kuridhishwa kwao na hali ya uhusiano uliopo.
Pamoja
na mambo mengine, Waheshimiwa Marais walikubaliana kuharakisha majadiliano
kuhusu Rwanda kuongeza matumizi yake ya Mkongo wa Taifa wa Tanzania.
“Nchi
zetu zilikubaliana kuhakikisha kwamba upembuzi yakinifu unaofanywa kuhusu
kuanzisha kiwanda cha maziwa Mkoani Mwanza unakamilika ifikapo mwezi Septemba,
2021. Kukamilika kwa mchakato huo na kuanza kwa uwekezaji kutatoa fursa za
ajira kwa vijana wetu, lakini pia kutaongeza soko kwa wafugaji wa ng’ombe wa
maziwa katika Kanda ya Ziwa,” amesema Balozi Mulamula.
Balozi
Mulamula ameongeza kuwa Waheshimiwa Marais wamebaini fursa mbalimbali za
ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ambazo zitakuwa na manufaa kwa Serikali
na wananchi ikiwemo sekta za biashara na uwekezaji na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano.
“Ziara
ya Mhe. Rais Samia nchini Rwanda ililenga pia kuimarisha ushirikiano katika
uendelezaji wa miundombinu ya ushoroba wa kati ambapo Serikali ya Tanzania
inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uchukuzi kupitia ushoroba wa
Dar es Salaam chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ikiwemo uboreshaji wa
Bandari za Dar es Salaam na Tanga na ujenzi wa miundombinu ya reli. Jitihada
hizo zinalenga kurahisisha na kupunguza muda na gharama za usafirishaji. Hivyo,
Mhe. Rais aliwakaribisha wafanyabiashara na wasafirishaji kutoka Rwanda
kuendelea kutumia Bandari za Tanzania, ameongeza Balozi Mulamula.
Balozi
Mulamula pamoja na Mambo mengine amesema kuwa katika ziara hiyo, Mhe. Samia akiwa
na mwenyeji wake Mhe. Paul Kagame walishuhudia utiaji saini wa Hati za
Makubaliano ya Ushirikiano nne (4) ambazo ni ati ya Makubaliano ya Ushirikiano
katika sekta ya Elimu, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya
TEHAMA, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Uhamiaji pamoja na Hati
ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Usimamizi wa Bidhaa za Dawa.
“Waheshimiwa
Marais walishuhudia pia uwekaji saini wa Tamko la Pamoja la Ziara (Joint
Communique) linaloainisha maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na kutoa mwongozo
wa utekelezaji,” amesema Balozi Mulamula.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mulamula ameongeza
kuwa, Rais Samia alitembelea kiwanda cha kutengeneza maji, maziwa na juisi cha
Inyange, kutembelea eneo la Makumbusho la Mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini
Rwanda Mwaka 1994 ambapo aliweka Shada la Maua kama ishara ya kumbukumbu
kwawote waliopoteza maisha.
Katika
ziara hiyo, Mhe. Rais Paul Kagame alielezea utayari wa Rwanda kuanza kufundisha
lugha ya Kiswahili katika shule zake na hivyo watahitaji walimu wa lugha ya
kiswahili.
Katika
Tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam
nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien.
Pamoja
na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa
Kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Vietnam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari
(Hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya
Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Naimi Aziz. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya
Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Naimi Aziz. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Kikao cha Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi
wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien kikiendelea
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.