Thursday, August 5, 2021

WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA NJE YA NCHI

Na Mwandishi wetu, Dar

Watanzania wamepewa changamoto ya kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana Nje ya Nchi ili waweze kuinua uchumi wao pamoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Changamoto hiyo imetokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amewasihi watanzania kuchangamkia fursa za masomo, masoko pamoja na biashara na uwekezaji na endapo kuna mtanzania anakwama basi asisite kuwasiliana na Wizara ili asaidiwe kupata ufumbuzi wa changamoto inayomkabili na kumwezesha kupata fursa husika.

“Fursa mbalimbali zimekuwa zikitangazwa katika Mashirika na Asasi za Kimataifa lakini watanzania wamekuwa wazito kiasi flani kuchangamkia fursa hizo, mfano fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nje ya nchi, fursa ya kuuza bidhaa za kilimo nje ya nchi na nyingine nyingi………rai yangu kwa watanzania tuchangamkie fursa hizi ili tuweze kuinua kipato na uchumi wetu na taifa kwa ujumla,” amesema Balozi Mulamula

Pia Balozi Mulamula amewahakikishia ‘Diaspora’ kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wao na kwa sasa inaendelea kuandaa Sera ya Mambo ya Nje ili kuwawekea mazingira bora na salama ya uwekezaji nchini.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula ameipongeza Kampuni ya Mwananchi kwa kuhabarisha na kuelimisha jamii kwa weledi wa taaluma ambao umekuwa ukiwawezesha wananchi kufahamu mambo mbalimbali yanayoendela nchini.

“Vyombo vya habari vya Mwananchi ni mdau muhimu sana kwani vimekuwa vikihabarisha na kuelimisha wadau mbalimbali mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali ya Tanzania,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari katika kuhakikisha kuwa vinaitambulisha vyema Serikali ya Tanzania vyema katika mataifa mbalimbali.

Balozi Mulamula ametembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na kujionea shughuli zinavyofanyika pamoja na kuongea na wahariri wa Magazeti hayo. 

Tarehe 04 Juni, 2021 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula alifanya ziara yake ya kwanza katika vyombo vya habari vya habari vya IPP ambavyo ni ‘The Guardian Ltd’ inayozalisha magazeti ya The Guardian na Nipashe, Radio One, Capital radio, East Africa radio, ITV, Capital TV pamoja na East Africa TV.

1.  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi za Mwananchi Communications Ltd Jijini Dar es Salaam. Mwingine ni Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo 


1.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwaelezea jambo Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu pamoja na Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo 


1.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiangalia gazeti la Mwananchi wakati wa kikao


1.  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nakala za Magazeti ya Mwananchi, The Citizen pamoja na Mwanaspoti


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mmoja kati ya wafanyakazi wa mwananchi   

1.  Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo akimuonesha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula namna magazeti yanavyohifadhiwa katika jalada maalum


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na wahariri wa Mwananchi Communications Limited kikiendelea 

1.  Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na wahariri wa Mwananchi Communications Limited kikiendelea  



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.