Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka watanzania kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuulinda, kuuheshimu na kuusherehekea kwa kuwa una manufaa makubwa kwao ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wananchi kwa ujumla.
Mhe. Dkt.
Mpango ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan kwenye sherehe hizo amesema kuwa, Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ambao waasisi wake ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ni tunu ya taifa inayotakiwa kulindwa, kuheshimiwa na kusherehekewa
kwani amani, umoja, usalama na mshikamano uliopo miongoni mwa watanzania
unatokana na Muungano huo.
Pia, ameongeza
kusema kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 58 ni mengi na ya
kujivunia katika sekta zote za uchumi, utamaduni, siasa, elimu na ajira.
“Tutaendelea
kuulinda Muungano wetu kwani una manufaa makubwa kwetu sisi kama taifa moja. Tunaposherehekea
miaka 58 ya Muungano tunayo mengi ya kujivunia, biashara kati ya Watanzania
imeimarika, raia wetu wanaweza kuishi popote bila tatizo lolote tuna amani na
utulivu unaowawezesha wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii
bila kikwazo chochote, alisema Mhe. Dkt. Mpango.
Halikadhalika
Mhe. Mpango amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni wa kipekee
duniani, umeendelea kuijengea heshima Tanzania tangu enzi za kupigania ukombozi
wa Nchi za Kusini mwa Afrika hadi sasa.
“Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeendelea kuheshimika duniani kutokana na mchango wake
kwenye medani za kimataifa. Tangu harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa
Afrika Tanzania ilikuwa mstari wa mbele hadi sasa Tanzania imeendelea kuchangia
vikosi vya kulinda amani kwenye nchi mbalimbali duniani na kushiriki kwenye
usuluhishi wa migogoro. Tanzania itaendelea kunufaika kama nchi moja na fursa
zote zinazotokana na mashirika ya kikanda na kimataifa ikiwemo SADC, EAC na Soko
Huru la Biashara Huru barani Afrika “aliongeza kusema Mhe. Dkt. Mpango.
Wakati wa
Maadhimisho hayo, Makamu wa Rais alizindua Kitabu Maalum cha Historia ya Muungano ambacho aliagiza kisambazwe kwenye Shule, Vyuo na Taasisi mbalimbali
ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuuelewa Muungano.
Awali
akizungumza kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya mwaka 2022 ambayo ni ya
kipekee yataambatana na midahalo na makongamano ya uelimishaji kuhusu Muungano
ili kuhakikisha kila Mtanzania hususan vijana wanauelewa Muungano ambao ni tunu
na urithi wa Wanzania.
Aidha,
akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdula amesema Mhe. Rais Mwinyi ameahidi
kuendelea kuusimamia na kuulinda Muungano kwa nguvu zake zote na kwamba
Muungano upo salama kwenye mikono yake na ya Mhe. Rais Samia.
Kwa upande
wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Muungano na
Mazingira, Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Muungano upo salama na kwamba tayari
kero za Muungano 18 kati ya 25 zimetatuliwa.
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni moja ya Wizara za
Muungano imeshiriki maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo ““Miaka 58 ya Muungano: Uwajibikaji na Uongozi
Bora; Tushiriki Sensa ya Watu na Anuani ya Makazi kwa Maendeleo Yetu”.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022 |
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika waliopo nchini wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. |
Sehemu nyingine ya washiriki kutoka Wizarani wakiwa kwenye maadhimisho hayo. |
Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Mpango akizindua kitabu maalum cha historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. |
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi nakala ya kitabu mwakilishi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania |
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi Mzee Hasanieli Mrema nakala ya kitabu. Mzee Mrema ni mmoja wa wazee waliochanganya mchanga kuashiria kuasisiwa kwa Muungano |
Mhe. Balozi Mbarouk akifurahia jambo na Balozi Fatma mara baada ya maadhimisho kumalizika |
Mhe. Balozi Mbarouk kwa pamoja na Balozi Fatma wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara walioshiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.