Tuesday, April 26, 2022

TANZANIA KUENDELEA KUULINDA MUUNGANO ILI KUWAENZI WAASISI WAKE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka watanzania kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuulinda, kuuheshimu na kuusherehekea kwa kuwa una manufaa makubwa kwao ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.


Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wananchi kwa ujumla.


Mhe. Dkt. Mpango ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe hizo amesema kuwa, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao waasisi wake ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ni tunu ya taifa inayotakiwa kulindwa, kuheshimiwa na kusherehekewa kwani amani, umoja, usalama na mshikamano uliopo miongoni mwa watanzania unatokana na Muungano huo.


Pia, ameongeza kusema kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 58 ni mengi na ya kujivunia katika sekta zote za uchumi, utamaduni, siasa, elimu na ajira.


“Tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwani una manufaa makubwa kwetu sisi kama taifa moja. Tunaposherehekea miaka 58 ya Muungano tunayo mengi ya kujivunia, biashara kati ya Watanzania imeimarika, raia wetu wanaweza kuishi popote bila tatizo lolote tuna amani na utulivu unaowawezesha wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii bila kikwazo chochote, alisema Mhe. Dkt. Mpango.


Halikadhalika Mhe. Mpango amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni wa kipekee duniani, umeendelea kuijengea heshima Tanzania tangu enzi za kupigania ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika hadi sasa.


“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuheshimika duniani kutokana na mchango wake kwenye medani za kimataifa. Tangu harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika Tanzania ilikuwa mstari wa mbele hadi sasa Tanzania imeendelea kuchangia vikosi vya kulinda amani kwenye nchi mbalimbali duniani na kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro. Tanzania itaendelea kunufaika kama nchi moja na fursa zote zinazotokana na mashirika ya kikanda na kimataifa ikiwemo SADC, EAC na Soko Huru la Biashara Huru barani Afrika “aliongeza kusema Mhe. Dkt. Mpango.


Wakati wa Maadhimisho hayo, Makamu wa Rais alizindua Kitabu Maalum cha Historia ya Muungano ambacho aliagiza kisambazwe kwenye Shule, Vyuo na Taasisi mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuuelewa Muungano.


Awali akizungumza kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya mwaka 2022 ambayo ni ya kipekee yataambatana na midahalo na makongamano ya uelimishaji kuhusu Muungano ili kuhakikisha kila Mtanzania hususan vijana wanauelewa Muungano ambao ni tunu na urithi wa Wanzania.


Aidha, akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdula amesema Mhe. Rais Mwinyi ameahidi kuendelea kuusimamia na kuulinda Muungano kwa nguvu zake zote na kwamba Muungano upo salama kwenye mikono yake na ya Mhe. Rais Samia.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Muungano upo salama na kwamba tayari kero za Muungano 18 kati ya 25 zimetatuliwa.


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni moja ya Wizara za Muungano imeshiriki maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Miaka 58 ya Muungano: Uwajibikaji na Uongozi Bora; Tushiriki Sensa ya Watu na Anuani ya Makazi kwa Maendeleo Yetu”.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiwa miongoni mwa viongozi wa Serikali walioshiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika waliopo nchini wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab akishiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwenye bendera ni Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Wizara, Bw. Salifius Mligo akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Alex Mfungo 
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi wa Wizara kama wanavyoonekana kwenye picha. Wa kwanza kulia ni Bi. Lilian Kimaro, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akifuatiwa na Balozi Caroline Chipeta, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria na Bi. Rosemary Jairo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama. 
Wakurugenzi kutoka Wizarani wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wa kwanza kulia mwenye bendera mkononi ni Bw. Magabilo Murobi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi akifuatiwa na Bw. Justine Kisoka, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango
Sehemu nyingine ya washiriki kutoka Wizarani wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Mpango akizindua kitabu maalum cha historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi nakala ya kitabu mwakilishi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi Mzee Hasanieli Mrema nakala ya kitabu. Mzee Mrema ni mmoja wa  wazee waliochanganya mchanga kuashiria kuasisiwa kwa Muungano
Mhe. Balozi Mbarouk akifurahia  jambo na Balozi Fatma mara baada ya maadhimisho kumalizika
Mhe. Balozi Mbarouk kwa pamoja na Balozi Fatma wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara walioshiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania
Balozi Fatma akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wa Wizara nje ya Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma ambazo zilipambwa kipekee kwa ajili ya kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Picha ya pamoja
Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma (katikati) akiwa na sehemu ya timu ya Wakurugenzi Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje wakifurahia miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Balozi Caroline Chipeta, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Bi. Tagie Daisy Mwakawago, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora, Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika. Wa kwanza kulia ni Bi. Lilian Kimaro, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akifuatiwa na Balozi Agnes Kayola, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Bi. Rosemary Jairo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama. 

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.