Na Mwandishi wetu, Addis Ababa
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia
Jenerali Wilbert Ibuge ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo
la kujionea utendaji kazi wa Ubalozi pamoja na kukagua mali za Serikali nchini
humo.
Balozi
Ibuge kabla ya kuanza kukagua mali za Serikali, alikutana na watumishi katika
mkutano ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa kuweka
mbele maslahi ya Taifa.
"Nawasihi
sana kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tufanye kazi kwa bidii na
kuwa wabunifu wa kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"
Amesema Balozi Ibuge
Pamoja
na Mambo mengine, Balozi Ibuge amewasihi Ubalozi huo kuhakikisha kuwa
wanatekeleza vyema vipaombele vya Serikali ya awamu ya tano kama ilivyoelekezwa
kwenye ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020 - 2025) katika Sura ya
Saba, ambapo sura hiyo imeelekezwa kuwa Balozi zote kutekeleza Diplomasia ya Uchumi
pamoja na Diplomasia ya Siasa.
Pia
Balozi Ibuge amekagua mali mbalimbali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania
nchini Ethiopia kwa lengo la kuijionea na kujiridhisha juu ya uwepo wa mali
hizo.
Kwa
upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi Elizabeth Rwitunga amemhakikishia
Balozi Ibuge kuwa watafanya kazi kwa umoja, bidii, weledi na ubunifu kwa
maslahi ya Taifa.
Bibi.
Rwitunga ameongeza kuwa mashirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri na
yanaendelea kuimarika ikiwemo ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga
ambapo Shirika la Ndege la Ethiopia linashirikiana na Shirika la Ndege la
Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya
ndege ambapo tayari watanzania watatu (3) wameshapatiwa mafunzo ya ndege.
Kuhusu
Sera ya Diplomasia, Kaimu Balozi, Bibi. Rwitunga ameahidi kusimamia sera ya
Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi
utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania
katika sekta za Nishati, Usafirishaji, Utalii pamoja na Biashara.
Ubalozi
wa Tanzania nchini Ethiopia unaiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Djibouti,
Yemen pamoja na Umoja wa Afrika na kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia
masuala ya Uchumi Barani Afrika (UNECA).
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa
Tanzania nchini Ethiopia
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo
pichani) wakati wa mkutano
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiendesha kikao na wafanyakazi wa Ubalozi
wa Tanzania nchini Afrika Kusini
Kaimu
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi. Elizabeth Rwitunga (mwenye gauni la
rangi ya bluu) akimpatia maelezo Balozi Ibuge wakati alipokuwa akikagua mali
zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia
Balozi Ibuge akipatiwa maelekezo kutoka kwa Afisa wa Ubalozi wakati wa ukaguzi wa mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia