Tuesday, January 24, 2017

Rais Erdogan aondoka nchini baada kumaliza ziara yake

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimsindikiza Rais wa Jumhuri ya Uturuki Mhe. Recep Tyyip Erdogan wakati akielekea kupanda ndege, kuondoka nchini mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Rais wa Uturuki Mhe. Recep Tyyip Erdogan wakipena mikono wakati wa hafla fupi ya kumuaga Rais huyo iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Rais Mhe. Erdogan na Mke wake wakipungia mikono wananchi waliojitokeza kumuaga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiwa na Waziri Mhe. Augustine Mahiga wakati wa kumuaga Rais Erdoga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Rais Magufuli ampokea Rais wa Uturuki Ikulu



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli  na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Recep Tyyip Erdogan wakiwasalimia wananchi walijiotokeza kwenye hafla ya kumkaribisha katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Recep Tyyip Erdogan akikabidhiwa ua na mtoto, Amara Asenath Tarimo wakati wa hafla ya kumkaribisha Rais huyo iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais Mhe. Dkt Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Erdogan wakiwa wamesimama wakati wimbo wataifa ukipigwa
Rais Mhe.Erdogan akikagua gwaride mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam


Rais Mhe. Erdogan akipiga moja ya ngoma zilikuwepo wakati wa hafla ya mapokezi ya kumkaribisha Ikulu Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Eng. John Kijazi wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakindelea 

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na hadhira waliojitokeza kwenye ukumbi wa Mikutano Ikulu Jijini Dar es Salaam

Monday, January 23, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Rais wa Uturuki nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayip Erdogan kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea katika mpango wake wa kuzitembelea nchi za Afrika. Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa anaongea na waandishi wa habari pamoja na mgeni wake huyo.

Rais Magufuli alimuhakikishia, Rais Erdogan kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uturuki na ana matumaini kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo kutakuza mahusiano zaidi ya kibiashara ambapo kwa takwimu zilizopo zinaonesha kuwa biashara kati ya nchi hizi mbili imekua kutoka Dola za Marekani milioni 66 mwaka 2011 na kufikia Dola milioni 190 mwaka 2016.

Aidha, Rais alielezea matumaini yake kuwa ziara ya Rais Erdogan nchini, itaongeza uwekezaji kutoka Uturuki ambapo kwa sasa takribani makampuni 30 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 305 ambayo yameajiri watu 2,959 yapo nchini.

Rais Magufuli na Mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 9 ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali kama vile, viwanda, utalii, usafiri wa anga, utangazaji, elimu, utafiti, ulinzi na afya. Uwekaji saini wa mikataba hiyo utaimarisha ushirikiano na utasaidia pia kufikia azma ya Serikali ya kuifanya kuwa nchi ya viwanda kutokana na teknolojia kubwa iliyofikiwa na Uturuki.

Rais Magufuli alieleza kuwa mojawapo ya kampuni zilizoomba zabuni ya kujenga reli ya kati ni kampuni kutoka Uturuki hivyo, amemuomba Rais Erdogan kuwa endapo kampuni hiyo itashinda zabuni, Benki ya Exim ya Uturuki  itoe mkopo kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya reli hiyo ambayo ina urefu wa zaidi ya kilomita 400.

Kwa upande wake, Rais wa Uturuki aliahidi kushirikiana na Tanzania kukuza uwekezaji na biashara ambapo alisisitiza umuhimu wa kukuza kiwango cha biashara angalau kifikie Dola milioni 500 kwa mwaka.

Aidha, Rais Erdogan alielezea tukio la jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali yake lililofanywa na kikundi cha Fethulla tarehe 15 Julai 2016 ambalo lilisababisha vifo vya watu 240 na maelfu ya majeruhi nchini humo. Alisema wafuasi wa kikundi hicho kilichopanga jaribio hilo wamesambaa hadi katika nchi za Afrika, hivyo, aliomba viongozi wa nchi za Afrika kushirikiana naye katika kukabiliana nao  ili kujihakikishia amani kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Rais wa Uturuki alihitimisha mazungumzo yake kwa kumuomba Rais Magufuli azuru nchini Uturuki wakati wa ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo ambapo Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Januari 2017.

Sunday, January 22, 2017

Rais wa Jamhuri ya Uturuki awasili nchini

Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdogan akiwa ameambana na mkewe Mama Emine Erdogan, wakiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Mhe. Rais Erdogan atakuwa nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia leo tarehe 22 Januari, 2017. 
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akimkaribisha Mhe. Rais Erdogan mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na Mhe. Rais Erdogan mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akisalimiana na Mhe. Rais Erdogan mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, pembeni ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Ali Salum Hapi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akisalimiana na Mhe. Rais Erdogan mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere.
Mhe. Rais Erdogan akisalimia sehemu ya vikundi vya ngoma vilivyokuwa vikitumbuiza uwanjani hapo wakati alipowasili.
Wakiendelea kutumbuiza.

Friday, January 20, 2017

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Denmark


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa maendeleo wa Denmark Mhe. Martin Bille Hermann  walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo yao walijikita katika maeneo mbalimbali ya kuendeleza  ushirikiano katika maeneo ya afya, elimu na uwekezaji. 

Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza Waziri wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Hermann, Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Joseph Sokoine na Afisa kutoka Wizarani Bi. Tunsume Mwangolombe

Mazungumzo yakiendelea

Waziri Mhe. Mahiga na Waziri wa Maendeleo wa Denmark Mhe.Hermann wakijadili jambo



Mhe. Rais Magufuli awaapisha mabalozi sita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimwapisha Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazili, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Dkt. James Msekela kuwa Balozi wa Tanzania Geneva - Umoja wa Mataifa, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Mhe. Mbelwa Kairuki kuwa Balozi wa Tanzania nchini China, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Mhe. George Madafa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Profesa Elizaberth Kiondo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Bi. Fatma Rajab kuwa Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Ikulu jijini Dar esa salaam leo January 20, 2017.
Sehemu ya Viongozi waliohudhuria hafla hiyo, ikulu jijini Dar es Salaam
Waheshimiwa Mabalozi wakila Kiapo cha maadili Mbele ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (hayupo pichani), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassani Suluhu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Jasmine Kairuki pamoja na viongozi mbalimbali walihudhuria hafla hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa tano kutoka Kushoto), Makamu wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassani Suluhu (wa nne kutoka kushoto), Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Dkt. Augustine Mahiga (wa tano kutoka kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (wanne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wateule mara baada ya kuapishwa, Ikulu jijini Dar es Salaam.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA UTURUKI NCHINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uturuki nchini

Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Mhe. Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22 Januari, 2017 jioni  na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali. 

Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.

Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania

Mahusiano ya Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof. Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
Pia kumekuwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul  nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
Tume ya Pamoja ya Biashara
Tanzania na Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya Biashara mwaka 2010. Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu, Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.

Kikao cha Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Januari, 2017.

Pande zote mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul. Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki. 

Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini. Hali kadhalika, Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la Uturuki lilianzisha safari tatu  za moja kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni Zanzibar. Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na Tanzania  ambapo mwaka 2009  ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352. 

Aidha, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na  Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
20 Januari, 2017