Thursday, August 30, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.







TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU MKUTANO WA JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA (FOCAC)

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) utafanyika Beijing kuanzia tarehe 01 hadi 04 Septemba, 2018.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. Viongozi wengine watakaoshiriki Mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga; Mhe. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mhe. Rashid Ali Juma, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Viongozi wengine Waandamizi.

Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa China, Mhe. Xi Jinping ambaye pia ni Mwenyekiti wa jukwaa hilo, kwa kushirikiana na Mwenyekiti Mwenza, Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa, utahudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ambaye pia ni Rais wa Chad, Mhe. Idriss Deby Itino. Mkutano huo pia utashuhudia uchaguzi wa Mwenyekiti Mwenza mpya kutoka Afrika.

Kaulimbiu ya Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika kwa mwaka 2018 ni “China na Afrika: Kuelekea Jumuiya Imara kwa mustakabali wa wote kupitia ushirikiano kwa manufaa ya wote” (China and Africa: Toward an Even Stronger Community with a Shared Future through Win-Win Co-operation).

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 01 Septemba, 2018. Kikao hicho pamoja na mambo mengine kitapitia agenda za mkutano huo na kuziwasilisha kwenye kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 02 Septemba, 2018.

Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati Afrika na China pamoja na mambo mengine utajadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na China na kufanya mapitio ya mikakati ya pamoja ya maendeleo iliyopo kati ya Afrika na China. Jukwaa hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2000 huwaleta pamoja viongozi wa Afrika na China kujadili masuala ya ushirikiano na maendeleo na kutathmini utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa kati yao.

Aidha, masuala ya ushirikiano katika uendelezaji Miundombinu kama Barabara, Reli, Bandari na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Bara la Afrika yatajadiliwa kwa kina. Agenda nyingine itahusu kilimo cha kisasa ambapo China itatoa uzoefu wake katika kutumia sayansi na ubunifu wa kiteknolojia katika kufikia uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani kwa mazao ili kuwa na soko la uhakika.

FOCAC 2018 pia itajadili masuala ya biashara na uwekezaji ambapo kwa kuona umuhimu huo, Mhe. Xi Jinping, Rais wa China atafungua rasmi Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya China na Afrika utakaofanyika tarehe 03 Septemba, 2018.

Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa hili ulifanyika Beijing mwaka 2006 na Mkutano wa Pili ulifanyika nchini nchini Afrika Kusini mwaka 2015.

Wakati wa Mkutano wa pili, China ilitangaza mpango kabambe wa kuhamasisha mapinduzi ya viwanda na kilimo cha kisasa kwa Afrika wenye gharama ya Dola za Marekani bilioni 60 katika utekelezaji wake. Kufuatia ushirikiano kupitia Jukwaa hilo biashara kati ya China na Afrika imeongezeka pamoja na ongezeko la ushirikiano wa kiutamaduni na biashara baina ya watu wa China na Afrika.

Pembezoni mwa Mkutano huo, Tanzania na China zimeandaa Kongamano la Biashara ambalo litafunguliwa rasmi na Mhe. Waziri Mkuu tarehe 02 Septemba, 2018. Kongamano hilo ambalo litajadili kwa kina masuala ya uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na China litashirikisha takribani makampuni 80 kutoka nchi hizi mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
30 Agosti 2018

Wednesday, August 29, 2018

TAMASHA LA KWANZA LA MICHEZO LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI LAFIKIA TAMATI


Bw. Addo Komba Afisa kutoka Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, akikabidhiwa kombe kufuatia ushindi timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania kwenye Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki lililofanyika Bujumbura, Burundi.

Tamasha la Kwanza la Michezo la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililokuwa likifanyika jijini Bujumbura limefikia tamati leo tarehe 29 Septemba, 2018. Hafla ya kufunga tamasha hilo ilihudhuriwa na Viongozi waandamizi wa Serikali kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchini Burundi.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Liberatus Mfumukeko alisema maadhimisho  ya tamasha hilo yameleta tija kubwa katika kuleta na kuimarisha umoja na shirikiano, kuibua na kuendeleza vipaji mbalimbali vya wananchi wa Afrika Mashariki.

Mhe. Sindimwo Gaston Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, kwa upande wake amesema ni fahari kubwa kwa Burundi kuandaa tamasha hilo lililofanyika kwa kipindi cha wiki mbili. Aliongeza kusema washiriki wa wamichezo hiyo watakuwa mabalozi wa kuelezea sifa nzuri za amani na utulivu ulipo nchini Burundi tofauti na inavyosemwa na baadhi ya watu.

Katika tamasha hilo Tanzania imeshinda kombe moja la mpira wa miguu wa wanawake ,medali ya fedha katika riadha, mpira wa pete na karatee.

Tamasha hili lilifanyika kuanzia tarehe 16 hadi 29 Agosti 2018, katika Jiji la Bujumbura na Gitega nchini Burundi.

Kikundi cha ngoma ya asili ya nchini Burundi kikisherehesha kwenye hafla ya kufunga Tamasha la  Michezo la Afrika Mashariki.

Bw. Liberatus Mfumukeko Katibu Mkuu wa  Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (kulia) akikabidhi kombe kwa mkuu wa msafara wa Uganda.

Bw. Liberatus Mfumukeko Katibu Mkuu wa  Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki akizungumza katika sherehe za kufunga Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki
Wachezaji wa timu ya wanawake ya mpira wa miguu Tanzania wakionyesha furaha yao ya kupata kombe baada ya kuibuka washindi katika mchezo huo kwenye Tamasha la Michezo la Afika Mashariki



Monday, August 27, 2018

Makamu wa Rais ashiriki sherehe za kuapishwa Majaji wapya wa Mahakama ya Afrika

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wapya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambao wameapishwa jijini Arusha. Kutoka kushoto ni Mhe. Jaji Amani Aboud (Tanzania), Mhe.Jaji Blaise Tchikaye (Congo) na kulia ni Mhe. Jaji Stella Isibhakhonem Anukam (Nigeria) 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya kuapishwa kwa majaji wapya watatu wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Arusha.


Viongozi Mablimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa pili kulia) wakimsiliza  Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia kwenye hafla ya kuapishwa majaji watatu wapya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Arusha. 
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya Mhe. Samiha Suluhu Hassan 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi kutoka kwa  Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mhe. Jaji Sylvain Ore mara baada ya kuapishwa kwa Majaji wapya watatu wa mahakama hiyo jijini Arusha.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimpongeza Mhe. Jaji Stella Isibhakhonem Anukam (Nigeria) mara baada ya kuapishwa
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Caroline Chipeta akisalimiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk Adelardus Kilangi katikati ni Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Wilbroad Kayombo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samiha Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), wakiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Arusha. 























Saturday, August 25, 2018

Tanzania yajitwalia medali za dhahabu katika Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki



Timu za mpira wa miguu za Wanawake  ya Tanzania (waliovalia jezi nyeupe) na Burundi wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mechi ya marudiano iliyofanyika katika uwanja wa Gitega, Burundi. Katika mpambano huo  wa Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki linaloendelea nchini humo Tanzania imeibuka na ushindi wa goli 5-0 dhidi  ya Burundi.

Aidha, Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki katika kipengele cha mpira wa miguu limekamilisha ratiba kwa mpambano kati ya Tanzania na Burundi, ambapo Tanzania imejishindia medali ya dhahabu kufuatia ushidi ilioupata. Burundi imejitwalia medali ya fedha kwa kushika nafasi ya pili katika mchezo huo.

Katika mchezo wa awali Tanzania iliibuka na ushindi wa goli 8-1 dhidi ya wenyeji wa tamasha Burundi.
 
Timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania ikishangilia ushindi wa medali za dhahabu kufuatia ushindi  wa goli 5-0 ilioupata dhidi ya Burundi katika Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki

Sehemu ya mashabiki wakishangilia mchezo uliokuwa ukiendelea kati ya Tanzania na Burundi
Mmoja wa wachezaji wa timu ya Tanzania akipongezwa na Bw. Addo Komba Afisa kutoka Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo mara baada ya kuvishwa medali ya dhahabu

Picha na Matukio ya Mpira pete

Timu ya mpira wa pete ya Tanzania ikiwa tayari kwa mchuano dhidi ya Uganda kwenye Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki. Katika mchuano huo Uganda iliibuka na ushindi wa goli 53-33 dhidi ya Tanzania.

Katika mchezo wa awali Tanzania iliibuka na ushindi mnono wa goli 79-14 dhidi ya wenyeji wa mashindano Burundi.
Wachezaji wa timu ya Tanzania (waliovalia jezi rangi ya waridi) wakijaribu kuzuia moja ya shambulio lililofanywa na timu pinzani ya Uganda
Mchezo wa mpira wa pete kati ya Tanzania na Uganda ukiendelea

Mshambuliaji wa timu ya Tanzania akilekeza mashambulizi kwa timu pinzani ya Uganda kwenye moja ya pambano la Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki.

Friday, August 24, 2018

Waziri Mahiga amuaga Balozi wa Ubelgiji nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza kwenye hafla ya kumuaga Balozi wa Ubelgiji aliyemaliza muda wa kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania Mhe. Paul Cartier (wa tatu kutoka kulia). Dkt. Mahiga alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuiwakilisha nchi yake vyema hapa Tanzania. Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani), Kaimu Mkurugenzi Idara ya  Ulaya na Amerika, Bw.Jestas  Nyamanga na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Hyatt Regency  jijini Dar es Salaam.
Balozi Paul Cartier naye alipata fursa ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ushirikiano aliokuwa akipata kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Mhe. Mwakyembe akisikiliza hotuba zilizokuwa zikitolewa na Dkt, Mahiga pamoja na Mhe.Cartier
Dkt. Mahiga akimkabidhi Balozi Cartier zawadi yenye mchoro wa Hifadhi ya  Mlima Kilimanjaro kama ukumbusho wa moja ya vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania
Waziri Mahiga (katikati), Balozi Cartier (wa nne kutoka kulia), Waziri Mwakyembe (wa tatu kutoka kulia), Bw. Nyamanga (wa tatu kutoka kushoto), Mke wa Balozi Cartier (wa nne kutoka kushoto) pamoja na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja.

 





Mikutano ya JPC ni Injini ya Maendeleo ya kiuchumi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Uganda zimepata mafanikio makubwa kupitia Mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyofanyika Arusha Aprili 2017 na sasa wa Kampala unaohitimishwa leo.

Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe .Dkt. Augustine Mahiga (Mb) na mwenzake wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa walipokuwa wanasoma hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.

Mafanikio yaliyoelezwa ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda na ushirikiano katika masuala ya elimu na mafunzo iliyosainiwa leo katika mkutano wa Kampala.

Mkutano huo ulijulishwa kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo unaridhisha na inalenga kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo ili kutimiza azma ya viongozi wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Museveni wa Uganda ya kukuza biashara kati ya nchi hizo.

Mikataba iliyosainiwa  inahusu uendelezaji wa miradi ya miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati ya Umeme, barabara hususan za mipakani, bandari, reli na usafiri wa anga.

Kufuatia mikataba hiyo miradi mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kikagati/ Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020. Aidha, Shirika la Ndege la Tanzania litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam hadi Entebbe mwishoni mwa mwezi huu kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga katika mkutano wa Arusha mwezi Aprili 2018

Miradi mingine ni ya ukarabati wa bandari za Bell na Bukasa na ukarabati wa meli za Kagawa na Pamba kwa upande wa Uganda ambayo italeta muunganiko mzuri katika usafirishaji hasa baada ya Reli ya Kisasa ya kiwango cha kimataifa inayojengwa na Tanzania itakapokamilika.

Waheshimiwa Mawaziri walisisitiza umuhimu wa Serikali za Tanzania na Uganda kuwekeza ipasavyo katika ushoroba wa kati ili kuleta muunganiko kwa ajili ya kukuza biashara. Aidha. Walisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kushughulikia changamoto za mipakani kwa haraka kadri zinavyojitokeza

Kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa miradi inayoafikiwa katika mikutano hiyo, pande zote mbili ziliwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu. 

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu walishiriki mkutano huo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kampala
23 Agosti 2018

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akisoma hotuba katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2918.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji akichangia jambo katika mkutano wa pili wa JPC kati ya Tanzania na Uganda.


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC0 kati ya Tanzania na Uganda.

Sehemu ya Waheshimiwa Mawaziri kutoka Uganda wakiwa katika mkutano huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi akichangia jambo katika mkutano huo.

Wajumbe wa Tanzania na Uganda wakiendelea na mkutano.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) na Waziri wa Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Peter T. Lokeris wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kuendeleza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda. Aliyesimam kushoto kwa Mhe. Mahiga ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akibadilishana Mikataba na  Waziri wa Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Peter T. Lokeris baada ya kusainiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu ya Juu wa Uganda, Mhe. J.C Muyingo wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kushirikiana katika masuala ya Elimu na Mafunzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu ya Juu wa Uganda, Mhe. J.C Muyingo wakibadilishna Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kushirikiana katika masuala ya Elimu na Mafunzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akimkabidhi Hati za Viwanja va Ubalozi wa Tanania nchini Uganda Mhe. Dkt. Augustine Mahiga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi wakibadilishana taarifa ya masuala yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo.


Wednesday, August 22, 2018

Mafanikio makubwa yamepatikana kupitia JPC, Balozi Mwinyi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda kwa ngazi ya Makatibu Wakuu. Katika hotuba hiyo, Balozi Mwinyi alieleza kuwa tokea JPC kati ya Tanzania na Uganda ilipoanzishwa mafanikio makubwa yamepatikana. Mafanikio hayo ni pamoja na kusainiwa kwa mikataba ya makubaliano mbalimbali ikiwemo mkataba wa kushirikiana katika ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kikagati/Murongo na makataba wa kushirikiana katika usafiri wa anga ambapo Tanzania inakusudia kuanza safari za moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam kwenda Kampala hivi karibuni. 

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini hotuba ya Balozi Mwinyi

Ujumbe wa Uganda ukifuatilia hotuba za ufunguzi zilizokuwa zinasomwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za Tanzania na Uganda.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akiongea na mwenyeji wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya kabla ya viongozi hao hawajafungua rasmi mkutano wa JPC kwa ngazi ya Makatibu Wakuu.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi akibadilishana mawazo na Balozi wa Uganda nchini Uingereza, Mhe. Leonard Mugerwa nje ya ukumbi wa mikutano.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Balozi Julius Onen akisoma hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala siku ya Jumatano tarehe 22 Agosti 2018.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko akichangia mada katika mkutano huo ambapo alisema kuwa Mamlaka ya Bandari imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zake

Mkurugenzi wa Shirika la kukuza Biashara katika nchi za Afrika Mashariki kwa upande wa Uganda (Trademark East Africa), Bibi Dawali Ssali akieleza mikakati ya inayofanywa na shirika hilo katika kuboresha mazingira ya biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. mikakati hiyo ni pamoja na kushirikiana na nchi za EAC kujenga vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani.


Wajumbe wa Uganda na Tanzania wakijadili mikakati ya kukuza na kuimarisha biashara kati ya nchi zao.


Tanzania na Uganda za azimia kukuza biashara kati yao

Tanzania na Uganda zimeazimia kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kukuza kiwango cha biashara kati yao ambacho kwa takwimu zilizopo sasa zinaonesha kipo chini mno.

Hayo yalibainishwa katika mkutano wa Jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo kando ya Mkutano wa pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) unaofanyika kwa silku tatu jijini Kampala tokea tarehe 21 Agosti 2018.

Mgeni Rasmi katika mkutano huo ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirikia ya Uganda, Balozi Julius Onen alieleza kuwa Tanzania na Uganda zina nafasi kubwa ya kukuza biashara endapo njia za usafiri zitaboreshwa, vikwazo visivyo vya kibiashara vitaondolewa pamoja na kuwa na mikakati ya pamoja ya kuweka viwango vya ubora vinavyotambulika katika nchi zote na kanda nzima kwa ujumla.

Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema kuwa Mamlaka ya Bandari imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zake ikiwemo kuanza upya kwa njia ya Dar Es Salaam- Mwanza hadi bandari ya Bell nchini Uganda. Alisema kufunguliwa kwa njia hiyo kumepunguza idadi ya siku za kusafirisha mizigo kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda ambapo kwa sasa mizigo inasafirshwa kwa siku nne  na kwa kiwango kikubwa na gharama nafuu.

Jambo hilo liliungwa mkono na wafanyabiashara wa Uganda walioshiriki mkutano huo ambapo waliipongeza TPA kutokana na hatua inazozichukua kuboresha huduma katika Bandari ya Dar Es Salaam na walikiri kuwa kufunguliwa kwa njia ya Dar Es Salaam-Mwanza hadi Bandari ya Bell kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kufanya biashara pamoja na muda wa kusafirisha bidhaa zao.

Balozi Onen aliendelea kueleza kuwa licha ya changamoto zilizopo za kufanya biashara kati ya Uganda na Tanzania lakini vihatarishi vya kufanya biashara na Tanzania ni vichache ukilinganisha na nchi nyingine.  Hivyo, aliwsihi wafanyabiashara wa Uganda na Serikali kwa ujumla kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na nchi hiyo.

Alibainisha kuwa Tanzania na Uganda zinaweza kufaidika zaidi kibiashara kutokana na nchi zote kuwa kwenye eneo la Maziwa Makuu ambalo lina soko kubwa kutokana na idadi kubwa ya watu katika eneo hilo. Hivyo alizihimiza Serikali zaTanzania na Uganda kufanya uwekezaji mkubwa katika ushoroba wa kati (central corridor) ili kukuza biashara.

Mkutano wa JPC unatarajiwa kufungwa rasmi Alhamisi kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi. Isack Kamwele (Mb) na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu (Mb) watashiriki mkutano huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kampala
22 Agosti 2018