Tuesday, December 11, 2018

Siku ya Tanzania ilivyosherehekewa sambamba na maonesho ya Jua Kali/Nguvu kazi

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson K. Mandgo alipokuwa akizungumza na wajasirimali katika sherehe ya siku ya Tanzania viwanja vya michezo Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea mjini hapo. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana.

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akiweka saini kitabu cha wageni mara baada ya kufika  kwenye banda la  Tanzania lililopo kwenye viwanja vya michezo vya Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi. Mhe.Mandgo alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya siku ya Tanzania katika maonesho hayo zilizofanyika tarehe 9 Desemba 2018. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana na kushoto ni Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Profesa Margrate Kamar.

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Mandgo akipanda mti ikiwa ni kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizoadhimishwa leo tarehe 09 Desemba 2018. Wanaoshuhudia tukio hilo ni pamoja na  Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana
Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akinunua nguo alipotembelea Banda la Wajasiriamali wa Tanzania baada ya kufurahia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo. Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana aliambatana na Gavana huyo kutembelea mabanda ya wajasiriamali kutoka Tanzania.



Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akivishwa vazi la kabila la Wamaasai kutoka Tanzania na kukabidhiwa mkuki na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe.Dkt. Pindi Chana wakati wa sherehe ya siku ya Tanzania zilizofanyika sambamba na maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi
===============================================

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya, Mhe. Jackson K. Mandgo amezishauri Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka bidhaa za wajasiriamali katika maduka makubwa (super market) ili wananchi kuzinunua na kuacha tabia ya kuthamini bidhaa za kutoka nje.

Gavana Mandgo aliyasema hayo wakati wa kusherehekea siku ya Tanzania iliyofanyika sambamba na maonesho ya 19 ya Afrika Mashariki ya Jua kali/Nguvu Kazi yanayoendelea katika Viwanja vya michezo vya Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret Kenya ambapo alikuwa mgeni rasmi kwenye siku ya Tanzania. Mhe. Mandgo alisema kwamba bidhaa za wajasirimali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinakidhi vigezo vya kuuzwa katika maduka hayo kutokana na kuwa na  ubora wake.

Katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi kila nchi husherehekea siku yake kwa kutangaza bidhaa na utamaduni wake. Tanzania ilitumia fursa hiyo kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara iliyoadhimishwa nchini kote tarehe 9 Desemba 2018.

Gavana Mandgo alisema kwamba wajasiriamali wanauwezo mkubwa wa kutengeneza  bidhaa bora ambazo kwa bahati mbaya hazipatikani katika maduka makubwa (super makert) hivyo alitoa wito kuwa wakati umefika sasa kwa bidhaa hizo kuuzwa katika maduka hayo.

Aidha alizishauri nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvitumia Vituo vya Elimu za Ufundi kama VETA hapa nchini, kutoa taaluma zaidi kwa wajasiriamali kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.

Alisema kwamba  Serikali ya Kenya hususan Kaunti ya Uasin Gishu ya  Eldoret itapeleka Mswada katika Baraza lake kwa kufanyia marekebisho ya sheria ya kutoa vyeti kwa wajasiriamali ambao watatahiniwa kwa  ubora wa bidhaa ambazo wanazalisha badala ya kufanya mitihani ya kuandika.

Pia alizitaka ofisi zote za Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, kutumia samani zinazotengenezwa na wajasiriamali kutokana  na kuwa  ni madhubuti na zenye ubora kuliko zilivyotengenezwa kutoka  nje ya Afrika Mashariki.

Gavana Mandgo ameipongeza Tanzania  kwa kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara.


Tanzania yazidi kung'ara Maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi nchini Kenya


Waziri wa Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Siaya Kenya Mhe. Jaokon O. Odinga (katikati) akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Balozi Dkt. Pindi Chana (kulia)  alipotembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret nchini Kenya, pembeni ni Mkurugenzi  Kitengo cha Diaspora Balozi Anisa Mbega wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Balozi wa Uganda nchini Kenya, Mhe. Phibby Otaala (kushoto) akibadilishana mawazo na Afisa Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Hassan Mnondwa (aliyesimama) juu ya ubora wa bidhaa za Tanzania zinazozasilishwa  na wajasiriamali  na kuuzwa katika maonesho ya Jua kali/Nguvu Kazi alipotembelea banda la Tanzania. Anayeweka saini kitabu cha wageni ni  Mhe. Namugwanya Benny Bugembe (MP) Waziri wa Nchi anayesimamia Mamlaka ya Jiji la Kampala Uganda.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana wa pili kutoka kushoto, Balozi wa Uganda nchini Kenya Mhe. Phibby Otaala wa pili kutoka kulia wakishikana mikono pamoja na viongozi wengine wa Uganda. Kutoka kushoto ni Waziri wa Biashara  na Viwanda wa Kaunti ya Uasin Gishu Dkt. Emily Kongos na kulia ni Mhe. Namugwanya Benny Bugembe (MP) Waziri wa Nchi anayesimamia Mamlaka ya Jiji la Kampala Uganda wakishikana mikono kuonesha ishara ya mshikamano wa viongizi wanawake wa Afrika Mashariki.

Juu na Chini ni Wananchi wa Kaunti ya Uasin Gishu wakitembelea kwa wingi katika mabanda ya Tanzania   wakifurahia na kununua bidhaa zinazozalishwa na Wajasiriamali na kuoneshwa katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea  mjini Eldoret.
Maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea  kufanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret Kenya ni ya kwanza kufanyika nje ya miji mikuu ya Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Friday, December 7, 2018

Watanzania wanogesha maonyesho ya 19 ya Jua Kali/ Nguvu Kazi


Juu na Chini ni Wajasiriamali wa Tanzania wakionesha bidhaa zao katika maonesho ya 19 ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayofanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu jijini Eldoret nchini Kenya. Kiasi cha Wajasirimali  wa Tanzania 250 waliwasili  mjini humo kwa ajili ya kushiriki maonesho  hayo.



Wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye maonyesho hayo wakionekana wakifurahia bidhaa za wajasiriamali zilizozalishwa na Watanzania wakati walipoyatembelea mabanda ya Tanzania katika maonesho ya 19 ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea jijini la Eldoret nchini Kenya.

Thursday, December 6, 2018

Japan yaadhimisha Siku ya Taifa

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda (Mb.) akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Taifa la Japani ambapo katika hotuba yake ameipongeza Japan kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali zinazo changia maendeleo ya nchi kama vile ujenzi wa miundombinu, Elimu na Afya.  Aidha, Mhe. Kakunda ameihakikishia Japan kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano pamoja na kuendeleza urafiki wa kidiplomasia kati ya Mataifa hayo mawili. Hafla hiyo imeudhuriwa na Mabalozi mbalimbali na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini Tanzania. Maadhimisho hayo yamefanyika katika makazi ya Balozi Masaki, jijini Dar es Salaam 
Balozi wa Japan nchni naye akitoa hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya Japan.
Balozi wa Japani akiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa walio hudhuria maadhimisho hayo.




Tuesday, December 4, 2018

Waziri Mahiga atembelea kiwanja kitakachojengwa Ofisi za Wizara kilichopo Ihumwa Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi alipofika eneo la kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Eneo la Mji wa Serikali la Ihumwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza  ujenzi wa Ofisi za Wizara unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Katikati ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Bibi Maimuna Tarishi. 
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Dorothy Mwanyika (mwenye miwani myeusi) wakimwonesha Mhe. Waziri Mahiga ramani inayoonesha kilipo kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Mhe. Waziri akimsikiliza Bibi Tarishi alipokuwa akimweleza jambo kuhusu ramani hiyo 
Mhe. Waziri Mahiga akiwaeleza jambo Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu, Bibi Tarishi,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Mwanyika na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi  alipofika eneo la kiwanja kilichotengwa kwa ajili ya kujenga Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichopo Ihumwa. 
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi akimwonesha  Mhe. Waziri Mahiga ukubwa wa eneo la kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

 

Mhe. Mahiga akimsikiliza Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Manyama Mapesi akimweleza kuhusu eneo hilo la kiwanja cha Wizara kilichopo Ihumwa. Wengine ni Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waliofika kwenye kiwanja hicho.

Friday, November 30, 2018

Dkt. kigwangalla na Dkt. Ndumbaro wafanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) akitoa neno la ufunguzi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Maiasili na Utalii, Mhe. Dkt. Khamis Kigwangalla kuongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo. Viongozi hao walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kuelezea mikakati inayochukuliw na Serikali ya awamu ya tano ya kuvutia utalii nchini. Mikakati hiyo imeanza kuzaa matunda ambapo wnanchi wa Urusi wameichagua Tanzania kuwa eneo bora zaidi kwa utalii duniani na kutoa Tuzo maalum kwa serikali. Aidha, Mikakati iliyofanywa nchini China hivi karibuni imewezesha kuingiwa kwa Mkataba wa kuleta watalii elf 10 kutoka Shangai mwaka 2019. Kushoto ni Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Yuri popov.
Dkt. Kigwangalla akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani ambapo alitumia fursa hiyo kuwaeleza namna Watalii wanavyoongezeka kuja nchini kwa wingi.  Alisema sekta ya utalii ndiyo inayoongoza kuingizia Taifa hili fedha za kigeni ambapo kitakwimu sekta hiyo inachangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni. Aidha. alitoa pongezi zake za dhati kwa balozi zetu zilizopo nje ya nchi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa zimekuwa zikifanya jitihada kubwa katika kutangaza Vivutio vilivyopo nchini Tanzania  ambapo kutokana na juhudi hizo Tanzania inapokea watalii wapatao Milioni 1.3 na malengo waongezeke zaidi kila mwaka. 
Balozi wa Urusi naye akizungumza na Waandishi wa Habari
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya naAmerika Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas Nyamanga (kushoto) pamoja na Naibu Balozi wa Urusi wakiwasikiliza kwa makini Mawaziri pamoja na Balozi wa Urusi wakizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Sehemu ya waandishi wa Habari wakisikiliza kwa makini Mawaziri walipokuwa wakiongea.

Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Hassan Mwamweta (wa kwanza kulia), akinukuu yaliyokuwa yakizungumzwa na Mawaziri (hawapo pichani).
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea




Wadau wa maendeleo wana imani na Tanzania, Dkt. Mahiga

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wadau wa maendeleo wana imani na Tanzania, Dkt. Mahiga

Ziara zinazofanywa nchini na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi ni ishara ya wazi kuwa nchi rafiki na wadau wengine wa maendeleo wana imani kubwa na Tanzania.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi nne kutoka Ulaya na Amerika Kusini kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere tarehe 29 Novemba 2018.

Viongozi hao ni Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura; Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen; Mjumbe kutoka China, Balozi Zhui Yuxiao, anayesimamia masuala ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na Mkurugenzi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugou-Moulin ambaye alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.

Wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Dkt. Mahiga alieleza kuwa, licha ya Tanzania na Norway kuwa na uhusiano mzuri na imara wa kidiplomasia, kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya nchi zote mbili. Dkt. Mahiga alitoa wito kwa Serikali ya Norway kushawishi sekta binafsi ya nchi hiyo kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Alisema kuna kampuni 33 za kutoka Norway nchini Tanzania ikiwemo kampuni ya Equinor ambayo ipo katika mchakato wa kuwekeza katika gesi asilia mkoani Lindi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kusafirisha nje. “Uwekezaji huu ni mkubwa na unahitaji ardhi kubwa ambayo ishapatikana na utakapokamilika utatoa ajira za maelfu kwa vijana wa Kitanzania”. Balozi Mahiga alisema.

Balozi Mahiga aliishukuru Norway kwa misaada ya kimaendeleo inayoipatia Tanzania ikiwemo ya kusaidia kufanya mabadiliko ya kimfumo katika masuala ya ukusanyaji kodi, miundombinu, nishati ya umeme na mbolea.
Aidha, Norway inafadhili mafunzo ya vitendo kwa wahandisi wa kike ili waweze kuwa na sifa ya kusajiliwa na Bodi ya Usajili ya Wahandisi. Kutokana na ufadhili huo ambao kwa miaka minane iliyopita umegharimu Shilingi bilioni 4.2 na kuwezesha wahandisi wa kike 504 kusajiliwa na kupunguza pengo kubwa la uwiano la wahandisi wa kike na kiume ambapo uwiano wao kabla ya ufadhili huo ulikuwa ni 1:27 na sasa ni 1:10.

Waziri huyo kutoka Norway alimdokeza Dkt. Mahiga kuwa Mfalme wa Norway ana panga kufanya ziara nchini Tanzania mwaka 2019.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, wawili hao walisisitiza umuhimu wa Tanzania na Venezuela kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi ambapo Venezuela imepiga hatua na sekta ya madini ambapo Venezuela ingependa kujifunza zaidi kutoka Tanzania. Ili kurahisisha utekelezaji wa mazaungumzo yao, Mhe. Naibu Waziri amewasilisha barua rasmi ya maombi ya nchi yake ya kufungua ofisi ya ubalozi nchini jambo ambalo Balozi Mahiga aliahidi litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Dernmark, Waziri Mahiga alijulisha kuwa Kiongozi huyo alitaka kupata ufafanuzi wa hali ya mambo yanavyoendelea nchini badala ya kutegemea taarifa za vyombo vya habari ambazo wakati mwingine zinakuwa sio sahihi. 

Baada ya ufafanuzi ambao ulimridhisha na hivyo kuihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa Denmark haijasitisha misaada kwa Tanzania. Ilielezwa kuwa misaada ambayo inakwenda moja kwa moja katika sekta ambayo ina thamani ya Dola za Marekani milioni 550 inaendelea kutolewa. Msaada unaokwenda kwenye bajeti ya Serikali moja kwa moja wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10 ambao mchakato wake umekamilika,  lakini kwa kawaida huwa unatolewa kwa pamoja na wadau wengine (Umoja wa Ulaya na Sweden) wanasubiriwa wakamilishe michakato yao ya ndani ili uweze kutolewa. Msaada huo kwa upande wa Sweden ni Dola milioni 9 na Umoja wa Ulaya ni Dola milioni 37.

Kuhusu mazungumzo na Balozi Zhui Yuxiao ambayo yalihusu mikakati ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC uliofanyika Beijing mwei Agosti 2018. Balozi Zhui alishauri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iteue mtumishi mmoja mwandamizi ili awe mratibu wa masuala ya FOCAC pamoja na kuteua kamati ya utekelezaji yenye wajumbe wa sekta mbali mbali lakini iratibiwe na Wizara ya Mambo ya Nje.

Kwa upande wa mazungumzo kati ya Dkt. Ndumbaro na Katibu Mkuu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugou-Moulin, wawili hao waliridhika na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zao ambao umedumu kwa miaka 98 tokea mwaka 1920.
Dkt. Ndumbaro alihimiza wawekezaji wengi zaidi kutoka Uswisi waje nchini kuwekeza kwa kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa kwa kiasi kikubwa. Alisema hakuna mabadiliko ya sheria za uwekezaji isipokuwa mabadiliko ambayo yamelenga kuboresha zaidi yamefanyika katika sheria ya madini. Hivyo, aliwataka wawekezaji wasiwe na hofu yeyote kuhusu Tanzania.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
Tarehe 30 Novemba 2018