Wito huo umetolewa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 77 ya
Umoja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Oktoba 2022.
Amesema Mkataba huo unaitaka Jumuiya ya
Kimataifa kuzisaidia nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwemo
kujenga uwezo, kubadilishana teknolojia na kuhakikisha nchi hizo
kiuchumi ili kuziwezesha kujitegemea katika kukabiliana na athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wiki mbili zijazo kuanzia leo, Mkutano wa 27 wa
Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utafanyika Sharm El Sheikh,
Misri. Ni kwa muktadha huo tunahitaji kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba
pamoja na mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, bado Afrika
ni Bara linaloathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na uwezo mdogo wa
kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo, tunaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa
kutimiza ahadi kulingana na maelekezo katika Mkataba wa Paris,’’ amesema
Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania
itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza program
mbalimbali za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu
kwa manufaa ya wananchi.
Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema, Tanzania inapoungana
na ulimwengu mzima kuadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo
kinachowakumbusha wadau wote nchini kujiimarisha katika ushirikiano ili
kuiwezesha Tanzania kutekeleza pamoja na mambo mengine Mpango wake wa Maendeleo
wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Tatu wa Umoja wa
Mataifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu
inayosema “Maendeleo Yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi yote” imebeba
ujumbe mzito unaomkumbusha kila mmoja kuungana na kutafuta suluhu kwa
changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia pasipo kumwacha mtu yoyote nyuma.
Pia amesema Tanzania ipo kwenye hatua za mapitio
ya utekelezwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuwataka wadau
mbalimbali kushirikiana nayo ili kufanikisha mapitio hayo.
Vilevile, wakati wa maadhimisho hayo,
Mhe. Dkt. Ndumbaro ameuomba Umoja wa Mataifa kuitambua Lugha ya Kiswahili
kama Lugha rasmi ya Umoja huo.
“Tunapoadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa,
Tanzania inaikumbusha dunia kuwa wakati umefika sasa wa kuridhia Kiswahili kuwa
miongoni mwa Lugha rasmi za Umoja huo” alisema Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya
Kimataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea
kuhifadhi wakimbizi na kwamba Umoja wa Mataifa na Taasisi zake utaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema Umoja huo unachangia katika miradi
mbalimbali ya kuwainua kiuchumi wanawake na vijana walio katika mazingira
magumu ikiwemo kuchangia katika uunzishwaji wa madawati ya jinsia yaliyo chini
ya Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu madawati 400 yameanzishwa nchini kote.
Wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro
alipata fursa ya kuzindua Tovuti ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili.
Maadhimisho hayo ya aina yake yamehudhuriwa na
Viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Mhe. Tabia Mwita, Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa yaliyopo nchini.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Zlatan Milisic akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akifuatilia Wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa |
Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa , Bi. Ellen Maduhu akitoa mwongozo wa maadhimisho hayo kwa washiriki |
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es Salaam wakitoa burudani na elimu kuhusu historia ya Umoja wa Mataifa kupitia sanaa ya uimbaji |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizindua rasmi Tovuti ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili |
Picha ya pamoja |