Tuesday, July 25, 2023
VIONGOZI AFRIKA WAENDELEA KUWASILI NCHINI KUSHIRIKI MKUTANO WA WAKUU WA NCHI KUHUSU RASILIMALI WATU
Monday, July 24, 2023
VIONGOZI MBALIMBALI WAENDELEA KUWASILI NCHINI KUSHIRIKI MKUTANO WA WAKUU WA NCHI KUHUSU RASILIMALI WATU
Balozi wa Ivory Coast nchini Afrika Kusini, Mhe. Sakaria Kone akizungumza na mmoja kati ya wajumbe alioambatana na kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu tarehe 25 - 27 Julai 2023 |
Waziri wa Fedha wa Kenya, Mhe. Prof. Njuguna Ndug’u (kushoto) akizungumza na mmoja kati ya wajumbe wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam |
Friday, July 21, 2023
NCHI WANACHAMA WA SADC ZARIDHIA KUMUUNGA MKONO DKT. TULIA NAFASI YA URAIS UMOJA WA MABUNGE DUNIANI
Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) imeridhia kwa kauli moja kumuunga mkono mgombea wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mgombea wa Kanda katika nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Luanda, Angola mwezi Oktoba 2023.
Hatua hiyo imefikiwa wakati wa Mkutano wa 25 wa Kamati hiyo uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 20 na 21 Julai 2023, baada ya Kamati hiyo kupokea na kuridhia ombi la Serikali ya Tanzania la kumuunga mkono Mhe. Dkt. Tulia lililowasilishwa kwao na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.
Aidha, wakati wa Mkutano huo, Jamhuri ya Zimbabwe ilitangaza kuwa imemuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho mgombea wake ambaye ni Spika wa Bunge la nchi hiyo, Mhe. Jacob Mudenda ili kumuunga mkono mgombea wa Tanzania kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza mara baada ya hatua hiyo, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Zimbabwe na Kanda kwa ujumla kwa kumuunga mkono mgombea wa Tanzania na kueleza kuwa Kanda itawezesha mgombea huyo huyo kushinda nafasi hiyo.
Vile vile, Mhe. Dkt. Tax ameieleza Kamati hiyo kwamba Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) tayari ameungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU), Bunge la Afrika (PAP), Jukwaa la Maspika wa Mabunge ya Afrika Mashariki na Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC PF) katika kugombea nafasi hiyo.
Meza Kuu |
Hafla ya kufunga mkutano ikiendelea |
Picha ya pamoja |
Picha ya pamoja |
Thursday, July 20, 2023
DKT. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 25 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SADC YA SIASA, ULINZI NA USALAMA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 20 na 21 Julai, 2023.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 19 Julai 2023, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 24 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amezipongeza nchi wanachama kwa ushirikiano katika kuendelea kuimarisha amani, usalama na utulivu katika Kanda ambavyo amevitaja kama msingi wa maendeleo endelevu.
Amesema kuwa kwa ujumla hali ya usalama katika kanda inaridhisha na kwamba Jumuiya ya SADC itaendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika maeneo yenye changamoto za usalama ikiwemo eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na lile la Kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.
Ameongeza kusema nchi wanachama zinaendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa ya hali ya usalama mashariki mwa Congo ili hatimaye eneo hilo lifikie hali ya utulivu na amani ya kudumu.
Akizungumzia hali ya usalama Kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado la nchini Msumbiji, Mhe. Nandi-Ndaitwah amesema hali kwa kiasi kikubwa ni shwari na vitendo vya ugaidi vimedhibitiwa huku maisha ya wananchi hususan wale waliokimbia makazi yao yakirejea katika hali ya kawaida.
Kadhalika ametoa wito kwa nchi wanachama kuendelea na jitihada za pamoja katika kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu kwa kuimarisha masuala ya sheria, kuwajengea uwezo wataalam na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu suala hili.
Kadhalika ametoa rai nchi wanachama ambazo hazijasaini au kuridhia Itifaki ya Uhuru wa raia wa Kanda ya SADC kutembea kwenye nchi za Jumuiya hiyo ya mwaka 2005 kufanya hivyo ili kuwawezesha wananchi kunufaika kikamilifu na agenda ya Mtangamano wa SADC.
“Nazihamasisha nchi ambazo hazijasaini au kuridhia Itifaki ya Uhuru wa Raia katika Kanda Kutembea ya mwaka 2005 kufanya hivyo. Itifaki hii ikianza kutekelezwa itaimarisha utalii miongoni mwetu na kuwawezesha raia kufanya biashara na uwekezaji katika kanda kwa uhuru zaidi, alisisitiza Mhe. Nandi-Ndaitwah.
Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Pia alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Nandi-Ndaitwa kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia.
Pia alitumia fursa hiyo kumtambulisha kwa Mawaziri Mkurugenzi mpya wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane kutoka Afrika Kusini.
Mbali na Mhe. Dkt. Tax, Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kaspar Mmuya, Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab na Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba.
Ufunguzi ukiendelea |
Mhe. Bashungwa akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Mnyepe. Kulia ni Balozi Fatma |
Mkutano ukiendelea |
Mkutano ukiendelea |
Sehemu ya Sekretarieti ya SADC wakati wa mkutano |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakati wa Mkutano |
Picha ya pamoaja |