Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Indonesia na kuwaambia wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia sababu tano zinazowafanya waje Tanzania kuwekeza mitaji yao.
Akifungua Kongamano hilo, lililofanyika jijini Jakarta tarehe 25 Januari, 2025 Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji kutoka Indonesia sababu tano zinazoifanya Tanzania kuwa kituo bora cha kuwekeza mitaji yao.
Ametaja sababu ya kwanza kuwa ni amani na utulivu uliopo nchini na Serikali inayofuata utawala bora, sababu nyingine ni sehemu ilipo Tanzania kijiografia kwa kuzungukwa na nchi ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni kuwepo kwa fursa za kutengeneza bidhaa na kupata masoko kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya za Kikanda kama EAC, SADC na Soko Huru la Pamoja la AfCFTA ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.2 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Indonesia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.
Sababu nyingine ni Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni na nia thabiti ya kisiasa ya Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi na kuweka msimamo wa kusaidia biashara na wafanyabiashara kukua.
“Uchumi mdogo na imara wa Tanzania ni himilivu, uchumi huo umeweza kuibuka baada ya janga la UVIKO 19. Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi baada ya kuisha kwa janga hilo, Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi baada ya kuisha kwa janga la UVIKO 19, hii inaifanya Tanzania kuwa mahali pazuri kwa uwekezaji, niwaambie majadiliano na nchi kama Indonesia yanadhihirisha azma ya Tanzania ya kujenga mazingira mazuri na bora kwa uwekezaji”, alisema Mhe. Rais Samia.
Katika kongamano Hati tatu za makaubaliano zilizosainiwa kati ya taasisi za Tanzania na taasisi za Indonesia zilitajwa. Hati hizo ni Makubaliano kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na PT Perusahaan Perdagangan Indonesia yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Mamlaka zinazosimamia Biashara Tanzania na Indonesia hivyo, kutengeneza umahili katika masoko na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kati ya Tanzania na Indonesia.
Hati nyingine ni Makubaliano kati ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania, Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar na Chemba ya Biashara na Viwanda ya Indonesia ikilenga kukuza na kuwezesha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ili kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania na Indonesia.
Hati ya tatu ni Makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Teknolojia cha Bangung yenye lengo la kuwezesha kufanyika kwa tafiti za pamoja za kitaaluma katika masuala mbalimbali, kutoa fursa za kujengeana uwezo na fursa za masomo ya elimu ya juu kutoka Serikali ya Indonesia.
Rais Samia amesema kuwa kusainiwa kwa hati hizo kunalenga kuchochea kasi mpya katika sekta ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Indonesia kwani biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi bado ni muhimu.