Thursday, February 22, 2024

WAZIRI MAKAMBA; DUNIA INAHITAJI MFUMO MPYA WA MAAMUZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akichangia mada kwenye Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb), ameieleza Jumuiya ya Kimataifa kuhusu umuhimu wa kuwa na mifumo mipya ya kimataifa itakayo zingatia haki na usawa katika kufanya maamuzi hasa kwa Mataifa ya Afrika.

Waziri Makamba ameeleza hayo kwenye mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India. Mkutano huo unawakutanisha wabobezi wa diplomasia, watunga sera, wafanyabiashara, wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili na kutafuta majawabu ya changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazoikabili dunia.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Makamba ameeleza kuwa, Afrika imepoteza imani na baadhi ya mifumo ya sasa ya Kimataifa ambayo mara nyingi imekuwa ikifanya maamuzi yanaoegemea au kunufaisha wachache na kusahau maslahi ya pande zingine ikiwemo Afrika.

Ameitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni Umoja wa Mataifa pamoja Baraza la Amani na Usalama la umoja huo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa kufanya maamuzi yanayopendelea upande mmoja, hivyo kujenga hali ya kuto aminiana miongoni mwa Mataifa.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo wa Raisina 2024, Waziri Makamba ameutaja kuwa ni jukwaa muhimu ambalo linapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ni chachu katika kuleta mabadiliko ya namna ya kutafuta majawabu na suluhu ya changamoto mbalimbali za kiuchumi na kisiasa kwa haki na usawa.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amefanya mazungumzo na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India pembezoni mwa mkutano wa Raisina 2024. Mazungumzo hayo yalijikita katika kufuatilia utekelezaji wa suala mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini humo mwezi Oktoba 2023.

Mawaziri hao wameeleza kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa sehemu kubwa ya masuala yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili.

“Tumeridhishwa na hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa makubaliano na Wakuu wa Nchi zetu, mimi na mwenzangu Mhe. Jaishankar tumekubaliana kuendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kuhakisha masuala yote yaliyokubaliwa tunayatekeleza ndani ya muda uliopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili” Alisema Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba anatarijiwa kufanya mazungumzo na Mhe. Shri Piyush Goyal Waziri wa Masuala ya Walaji, Chakula na Usambazaji kwa Umma wa India (Minister for Consumer Affairs Food and Public Distribution) ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kufuatilia utekelezaji.
Mkutano wa Raisina 2024 ukiendelea jijini New Delhi, nchini India
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na washiriki wenzake wa majadiliano kwenye Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Anisa Mbega akifuatilia Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba kwenye picha ya pamoja na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa Raisina 2024
Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa kwenye mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India
Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe. Subrahmanyam Jaishankar akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba

RAIS SAMIA AWAPONGEZA KUWAIT KUADHIMISHA MIAKA 63 YA TAIFA HILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salaam za pongezi na kumtakia afya njema Amir wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Mishal Al Ahmad Al Jaber Al Sabah katika kuadhimisha miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo imeadhimishwa tarehe 21 Februari 2024.

Katika salaam zake za pongezi, Mhe. Rais Samia amepongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa na nchi ya Kuwait katika maeneo mbalimbali ikijumuisha sayansi na teknolojia, huduma za afya na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla na kuiwezesha Kuwait kuwa moja wapo ya nchi zenye uchumi imara duniani na kituo maarufu  cha kifedha, mitaji na uwekezaji. 

Aidha, Mhe. Rais Samia ameeleza kuridhishwa na uhusiano imara uliopo baina ya Tanzania na Kuwait na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na Kuwait katika kuimarisha biashara, uwekezaji na maendeleo ya jamii kwa maslahi ya wananchi wa pande zote.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) ameipongeza na kuishukuru  Serikali ya Kuwait kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya afya nchini ikiwemo msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mhe. Ummy ametoa kauli hiyo aliposhiriki kama mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru na miaka 33 ya Siku ya ukombozi wa Kuwait yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 21 Februari 2024 na kuongozwa na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Kuwait imekuwa mshirika mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya hapa nchini ambapo tayari imetoa msaada wa mashine za ganzi kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Vifaa tiba katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Mashine za Watoto Wachanga zisizo na hewa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Handeni, Tanga unaofadhiliwa na Taasisi ya Abdullah Al Nouri ya Kuwait. 

Aidha ameongeza kusema mwaka 2023 Kuwait kupitia Kuwait Children Heart Association ilileta madaktari bingwa walioshirikiana na watalaam wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto 100 wa kipato cha chini.

“Tunaishukuru Kuwait kwa msaada wake katika Sekta ya Afya, pamoja na kutoa msaada wa mashine za ganzi, wameweza kusaidia vifaa vya upasuaji kwa watoto wanaosumbuliwa na vichwa vikubwa (Hydrocephalus) kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).” alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan alisema kuwa ushirikiano wa Kuwait na Tanzania umekuwa ukikuwa na kuimarika tangu mwaka 2015. Kuwait itaeendelea kushirikiana na Tanzania kijamii, kisiasa na kiuchumi wakati wote.

“Tunapoadhimisha siku hii muhimu, mataifa yetu yanategemea kuanzia ushirikiano katika sekta ya michezo kati ya Mamlaka ya Michezo ya Kuwait na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ya Tanzania. Aidha, Balozi Alsehaijan aliongeza kuwa Kuwait itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Balozi Alsehaijan.

Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru na miaka 33 ya Siku ya ukombozi wa Kuwait yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa Shaib pamoja na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Tanzania na Kuwait zinashirikiana katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, maendeleo ya miundombinu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji ambapo kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.


Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan akizungumza wakati wa kuadhimisha miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo iliyoadhimishwa tarehe 21 Februari 2024 jijini Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akiwasilisha hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo iliyoadhimishwa tarehe 21 Februari 2024 jijini Dar es Salaam



Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya miaka 63 ya siku ya Taifa la Kuwait na Miaka 33 ya ukombozi ambayo iliyoadhimishwa tarehe 21 Februari 2024 jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa Shaib.  




TANZANIA – PANAMA MBIONI KUANZISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney wakifurahia jambo walipokuta kwa mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia jijini New Delhi, India.


Tanzania na Panama zimefungua mlango wa majadiliano wa kuanzisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za uchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. Miongoni mwa sekta zinazoangaziwa kwenye ushirikiano huo ni pamoja na utalii, biashara na uwekezaji, madini, Mabadiliko ya Tabia Nchi, na Kilimo. 

Hayo yamejili katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia unaoendelea jijini New Delhi, India. 

Waziri Makamba katika mazungumzo hayo alieleza kuwa licha ya uongozi imara, uwingi wa rasilimali, vivutio lukuki vya kipekee vya utalii, amani na utulivu wa kisiasa uliopo nchini, Tanzania ipo katika nafasi nzuri zaidi kijiografia inayoifanya kuwa lango la kuzifikia kwa urahisi nchi nyingi za jirani. Hali hiyo inawavutia wawekezaji na wafanyabishara wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuwekeza nchini.

“Serikali chini uongozi imara wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeboresha sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji ambazo zimefanya mazingira ya biashara kuwa rafiki zaidi. Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Panama kuwekeza mitaji yao kwakuwa kijografia, Tanzania ni lango la kuzifikia Nchi nane ambazo ni soko kubwa kwa wawekezaji na pia ni nchi ya amani inayoamini katika usawa na utawala wa sheria” Alisema Mhe. Makamba. 

Kwa upande wake Waziri Tewaney ameeleza kuwa Panama inashauku kubwa ya kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kwa kuwa inatambua fursa zinazopatika katika pande zote mbili zikitumiwa ipasavyo zitaleta tija katika mandeleo ya uchumi ya pande zote. 

Aidha, Waziri Tewaney ameongeza kuwa hatarajii kuishikia kwenye ushirikiano wa sekta za uchumi pekee, bali anaona ipo fursa kwa Nchi hizo mbili kufungua milango ya kuanza kuangazia namna kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kwa kuwa zina mtazamo unaoshahabiana katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje. 

Pande zote mbili zimeazimia kuanza kwa utekelezaji wa haraka wa masuala yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Katika hatua nyingine Mhe.Waziri Makamba amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Uingereza anayesimamia Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika, Kusini mwa Asia, Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa Mhe. Tariq Mahmood Ahmad (Mb) yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia jijini New Delhi, India. 

Mazungumzo yao yalijikita kujadili na kutafuta majawabu ya masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa hususani katika maeneo ya ulinzi na usalama na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Waziri Makamba yupo nchini India kushiriki katika Mkutano wa 9 wa Raisina (9th Raisina Dialogue)unaofanyika nchini humo terehe 21 – 23 Februari 2024. Mkutano huo umefunguliwa Februari 21, 2024 na Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi na Waziri Mkuu wa Ugiriki Mhe. Kyriakos 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney walipokuta kwa mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia unaoendelea jijini New Delhi, India. 
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney (kushoto) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisalimiana na Waziri wa Nchi wa Uingereza anayesimamia Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika, Kusini mwa Asia, Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa Mhe. Tariq Mahmood Ahmad (Mb) yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia jijini New Delhi, India. 
Mazungumzo yakiendelea

Wednesday, February 21, 2024

AFRIKA YASHAURIWA KUWA NA SERA YA LUGHA ZA ASILI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezishauri nchi za Afrika kuwa na sera ya lugha za asili ambayo itazingatia mchango wa lugha za asili katika kukuza uchumi.

Ushauri huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kufunga Kongamano la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni.

Katika Hotuba hiyo Dkt. Mwinyi, amesema Bara la Afrika ndilo bara lenye idadi kubwa ya vijana duniani na linategemewa kuwa na nguvu kazi ya dunia hivyo ni lazima kujiandaa kuona Afrika inaandaa nguvu kazi yenye ustadi na maarifa inayosimamia utamaduni na lugha zake za asili.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa kuna umuhimu wa kujadili maarifa kupitia lugha za asili yanavyoweza kupatikana na jamii zikaweza kutumia ili kunufaika katika kulinda maliasili na kuendeleza shughuli za uzalishaji kama vile kilimo, uvuvi na utamaduni wa ufinyanzi, ususi na nyenginezo.

“Katika jamii za kiafrika, mfungamano uliopo baina ya lugha za asili na maisha ya kazi, ya ubunifu  na ya ugunduzi wa biashara siyo wa kinadharia, bali ni ukweli tunaoishi nao. Kuwapo kwa lugha hizi za asili na hasa matumizi yake ni lazima kuchangie katika maendeleo ya kiuchumi ambayo yatakuwa endelevu,” alisema Dkt. Mwinyi katika hotuba yake.

Kadhalika, Dkt. Mwinyi amewataka wataalamu wa lugha kuongeza ushawishi na mchango katika kuhakikisha Kiswahili kinakuwa daraja muhimu la kukuza diplomasia ya uchumi na kiutamaduni katika ukanda wa Afrika kwa kuzingatia nafasi yake miongoni mwa lugha za asili za kiafrika.

Kongamano hilo limeshirikisha wataalamu wa lugha na watafiti, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, watu mashuhuri na Viongozi Wastaafu na mahiri katika kutumia lugha adhimu ya Kiswahili ikiwa ni miongoni mwa lugha za asili ambayo inazidi kupata mafanikio.

Rais Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia nafasi ya lugha, matumizi ya kidijiti na uchumi wa buluu ambapo alisema kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana  wanaotarajiwa kuwa mstari wa mbele katika ubunifu, ugunduzi na matumizi ya vifaa vya kidijiti.

“Tunapaswa kujiuliza ni kwa namna gani wingi wa lugha za asili za kiafrika unavyoweza kutumika kujenga uchumi wa mataifa yetu na kuona kwa vipi tutatumia tofauti za rasilimali tulizonazo na lugha katika kujifunza mifumo ya ikolojia ya bahari ya hindi ili kukuza uchumi wa buluu,” alisema Dkt. Mwinyi. 

Katika hatua nyingine Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano ametembelea makumbusho ya Taifa na Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es salaam. 

Akizungumza baada ya kutembelea makumbusho ya Taifa, Mhe. Chissano amesema kuna haja ya kuendelea kuhifadhi historia zinazohusu waafrika ili kuonesha ulimwengu juu ya maendeleo yaliyofikiwa na waafrika kabla ya ukoloni.

Mhe. Chissano alikuwa nchini kuhudhuria Kongamano  la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni. lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 20 na 21 Februari 2024.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akiwasilisha hotuba ya kufunga Kongamano la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Jijini Dar es Salaam

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Utamaduni wa Makumbusho ya Taifa, Bi. Anthonia Mukama wakati alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi Makumbusho ya Taifa alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano akimsikiliza mmoja kati ya maafisa wa Kijiji cha makumbusho wakati alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam





WAZIRI MAKAMBA KUENDELEA KUIPAISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI KATIKA MKUTANO WA RAISINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mheshimiwa January Makamba (Mb), anatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa 9 wa RAISINA (9TH RAISINA Dialogue) unaotarajiwa kufanyika nchini India kuanzia Februari 21 hadi 23, 2024. Ushiriki wake katika mkutano huo unaonesha azma ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, diplomasia na kutafuta ushirikiano wenye tija kwa maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii ya Taifa. 

Mkutano huo wa RAISINA unaofanyika kila mwaka unaandaliwa na Observer Research Foundation (ORF) ya India kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo tangu mwaka 2016. Mkutano huo unawakutanisha nguli wa wanadiplomasia, watunga sera, wafanyabiashara, wataalamu na wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili na kutafuta majawabu ya changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazo ikabili dunia.

Ushiriki wa Tanzania kwa mara ya kwanza katika mkutano huo tokea kuanzishwa kwake, kunashsiria azma ya serikali ya kutumia ushawishi wake wa kidiplomasia katika kutafuta fursa, kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wake. Kuongezeka kwa ushawishi wa Tanzania na kukubalika kwake katika majukwaa ya kimataifa pamoja na masuala mengine kunatokana na uongozi imara, amani na utulivu wa kiasiasa uliopo nchini, nafasi ya kimkakati ya kijiografia, uwingi wa rasilimali na ukuaji endelevu wa uchumi wa Nchi. 

Bila shaka, ushiriki wa Makamba katika jukwaa hili la kimataifa unaakisi dhamira yake ya kuendeleza maslahi na diplomasia ya kimkakati ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa kwa kuendelea kuimarisha urafiki wa kudumu na mataifa mengine na taasisi za kimataifa.

Mbali na hayo Waziri Makamba katika mkutano huo anatarajiwa kuonyesha dhamira ya Tanzania ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kukuza biashara, vilevile kuonesha jitihada na hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto zinazofifisha ukuaji wa sekta muhimu kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, afya, mawasiliano, kilimo, nishati, uchumi wa buluu, kilimo na madini. 

Jambo la muhimu zaidi mkutano huo unatoa fursa hadhimu kwa serikali ya Tanzania kushiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo yenye tija katika uhusiano wa kidiplomasia na India na Nchi mbalimbali duniani. Hatua hiyo itachagiza ukuaji maradufu wa biashara, uwekezaji, teknolojia na na utalii na kuchangi katika ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na kidiplomasia hususan katika biashara na uwekezaji ambao umeifanya India kuwa mshirika wa tatu mkubwa wa biashara wa Tanzania, ikikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1 kwa mwaka 2022/2023. Kiasi hiki kimeendelea kukua ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 2.6 katika kipindi cha 2017-2018. Mwaka 2021/2022 India imerekodiwa kusajili miradi 630 ya uwekezaji nchini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.7 ambayo imezalisha ajira zaidi 60,000.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na mmoja wa watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Indira Gandhi. Waziri Makamba yupo nchini India kushiriki kwenye Mkutano wa Raisina unaoanza tarehe 21  Februari 2024.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika maandalizi kushiriki katika Mkutano wa Raisina unaofanyika nchini India kuanzia tarehe 21 -23 Februari, 2024. Wengine Balozi wa Tanzania  nchini India Mhe. Hanisa Mbega na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bw. Salvatory Mbilinyi 

Tuesday, February 20, 2024

BALOZI MBAROUK AKUTANA NA WABUNGE NA MASENETA WA CANADA JIJINI DODOMA

Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas (kushoto) akizungumza na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) wakati balozi huyo alipoambatana na Wabunge na Maseneta wa Canada walipokutana na Balozi Mbarouk ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa kwanza kulia) akizungumza na  Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas (wapili kulia) na Seneta Mhe. Amina Gerba  wa Canada (wa pili kushoto) na Mbunge wa Canada Mhe. Brenda na Shahan (wa kwanza Kushoto) walipokutana ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma

mazungumzo yakiendelea


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas (wa kwanza kushoto) na Mbunge wa Canada Mhe. Brenda na Shahan (wa kwanza Kulia) na Seneta Amina Gerba (wa pili kushoto)  walipokutana na Balozi Mbarouk ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na ujumbe wa wabunge na maseneta kutoka Canada walipokutana naye ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma
 



Baadhi ya Wabunge na Maseneta wa Canada wakimsikiliza Naibu Waziri Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana naye ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk  (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na Wabunge na Maseneta kutoka Canada walipomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma

 



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amekutana na Ujumbe wa Jumuiya ya Maseneta na Wabunge wa Canada (Africa Parliamentary Association (CAAF) ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma Februari 20, 2024.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Mbarouk ameelezea kuridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Canada, hususan katika sekta za sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.

Amesema Serikali ya Canada imekuwa mdau mkubwa katika harakati za kusaidia uboreshwaji na uimarishwaji wa mifumo ya afya nchini kwa kusaidia kuimarisha huduma za afya ya uzazi na vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini.

“Canada imekuwa mdau wetu mkubwa katika sekta ya afya nchini, imetupatia Dola za Canada zipatazo Milioni 15 kupitia mfuko wa bajeti ya afya, msaada huu una maana kubwa kwa Tanzania, unasaidia sana kuboresha sekta ya afya nchini,” alisema

Amesema Canada pia imekuwa ikisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ambapo imetoa msaada wa Dola za Canada milioni 53 ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuboresha kiwango cha elimu hasa kwa watoto wa kike nchini.

Kuhusu Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mbarouk amesema kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi kinaendelea kuimarika na kuongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 26 kiwango cha mauzo ya Canada kwa Tanzania kimeongezeka kwa asilimia 9.27 kutoka Dola milioni 16.1 za Canada hadi kufikia Dola Milioni 194 za Canada kwa mwaka 2023, na mwaka huo huo, Tanzania iliiuzia Canada bidhaa zenye thamani ya Dola za Canada Milioni 19.9.

Amewahakikishia  Wabunge na masenator hao kutoka Canada kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutoka Canada kuja nchini kuwekeza mitaji yao hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina soko kubwa kutokana na uanachama wake katika jumuiya za kikanda za EAC na SADC.


Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa wabunge na masenata, Bi Brenda Shanahan (MP) amesema kuwa ziara hiyo inalenga kuwajengea uwezo wabunge hao katika nchi wanazozitembelea na kuona jinsi ambavyo Serikali yao inavyoshirikiana na Tanzania na nchi nyingine za Afrika.


Ujembe huo upo nchini kwa ziara ya kikazi tangu tarehe 18 Februari 2024 na umeshatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukutana na Spika wa Bunge hilo ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt Tulia Ackson pamoja na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama. Ujumbe huo pia unatarajiwa kwenda Zanzibar tarehe 21 Februari 2024 ambapo pamoja na mambo mengine utakutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi.


Madhumuni ya ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Canada hususan baina ya Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Canada.



DKT. MPANGO: PANGENI MIKAKATI YA KUKUZA LUGHA YA KISWAHILI, LUGHA NYINGINE ZA ASILI KATIKA UCHUMI WA KIDIJITI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewasihi washiriki wa Kongamano la lugha za asili kujielekeza kupanga mikakati itakayohakikisha lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za asili zinapata fursa katika uchumi wa kidijiti ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni linalofanyika kwa siku mbili (2) tarehe 20 - 21 Februari, 2024 Jijini Dar es salaam. 

Makamu wa Rais amesema Kongamano hilo linapaswa kuangazia namna ambayo Kiswahili na lugha nyingine za asili za Afrika zitakavyotumika kuendeleza teknolojia za asili, kuchochea uvumbuzi, uwekezaji na kukuza diplomasia.

Aidha, Makamu wa Rais ameongeza kuwa Kongamano hilo linapaswa kusaidia kuonesha fursa zilizopo katika matumizi ya lugha za asili ili kuwafanya vijana kujipatia stadi na maarifa mbalimbali katika kujiandaa kwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia ndani na nje ya bara la Afrika.

Makamu wa Rais amesema kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kumepanua wigo wa matumizi ya Kiswahili na kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kiutamaduni.

“Kongamano hili muhimu linabeba jukumu kubwa la kuibua fursa zaidi na kuendeleza historia ndefu ya Kiswahili katika kujenga uhusiano kati ya watu wa tamaduni, lugha na misingi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii,” alisema Dkt. Mpango.

Amesema Katika muktadha wa ukuaji na maendeleo ya Kiswahili, ni pamoja na kuhifadhi lugha nyingine za asili, sambamba na  tamaduni na mifumo yake. Afrika Mashariki na Kati, wafanyabiashara wadogo na wanaoinukia  “Wamachinga” wametoa mchango ambao hauna budi kutambuliwa na kuthaminiwa

Dkt. Mpango ameongeza kuwa lipo hitaji la kufanya utafiti wa kina ili kuona jinsi nchi za Kiafrika zinavyoweza kuendeleza mifumo inayozingatia ushiriki wa vijana na makundi kama ya wafanyabiashara waliojiajiri katika diplomasia ya uchumi na kukuza biashara.  

Kadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika kukuza lugha ya Kiswahili, ambapo inalenga kuifanya lugha hiyo kuendelea kuleta umoja, amani na kuvumiliana katika bara zima la Afrika. 

Aidha, Dkt. Mpango amekipongeza  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendelea kushirikiana na Vyuo na Taasisi za nje katika kukuza Kiswahili na kuendeleza diplomasia ya kiutamaduni.

Kongamano hilo limehudhuriwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, Mabalozi wa nchi za nje nchini, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James G. Bwana, Watunga sera, Wafanyabiashara, Wajasiriamali na wenye Viwanda, Viongozi wa Dini, Wanataaluma na Wakuu wa Taasisi za Utafiti, Vijana, Wanawake na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kiraia. 

Kongamano limeandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kwazulu-Natal cha Afrika Kusini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Sehemu ya mabalozi wakifuatilia Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe James G. Bwana akifuatilia Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta akiteta jambo na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano wakati wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024

Mmoja kati ya Washiriki akichangia jambo katika Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni 

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe.Uhuru Kenyatta akifuatilia mada katika Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni 




Monday, February 19, 2024

UJUMBE WA NDC WATEMBELEA WIZARA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) amekutana na Ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) jijini Dodoma, Februari 19, 2024.


Ujumbe huo unaongozwa na Mkuu wa Chuo cha NDC, Balozi Meja Jenerali Wilbert A. Ibuge, upo katika ziara ya mafunzo ya kutembelea taasisi mbalimbali kujifunza kuhusu mchango wa taasisi hizo katika maendeleo ya nchi hususan kwenye sekta ya ulinzi. Ujumbe huo wenye jumla ya washiriki 88, unahusisha Wakufunzi 33, na Wanachuo 55 kutoka Tanzania na mataifa ya Afrika ikiwemo Nigeria, Namibia, Misri, Zambia na Zimbabwe.

 

Mej. Gen. Ibuge alieleza kuwa malengo ya chuo hicho ni kuwandaa Maafisa Waandamizi ndani na nje ya nchi kutoka vyombo vya Usalama na Watumishi wa Umma katika nyanja ya Usalama na Stratejia. Wakati wa ziara hiyo, ujumbe huo umeshiriki kwenye mjadala kuhusu Umuhimu wa Kuimarisha usalama wa jamii zinazoishi mipakani kwa ajili ya usalama endelevu wa Taifa (Enhancing Border Community Security for Sustainable National Security).


Ujumbe huo umepokea wasilisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambapo Balozi Dkt. Shelukindo alielezea majukumu ya Wizara hususan katika kuhamasisha usalama mipakani. Majukumu hayo yanahusisha uratibu wa mikutano ya ujirani mwema na Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPCs), Vituo Vya Utoaji Huduma Kwa Pamoja Mipakani (OSBPs), na kuratibu itifaki za kikanda na kimataifa.


Aidha, Wizara na Chuo cha NDC zimeahidi kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo mafunzo kwa Watumishi na maeneo mengine muhimu kwa maslahi ya pande zite mbili

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge wakati ujumbe wa chuo hicho ulipofanya ziara ya mafunzo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Chiku Kiguhe akitoa neno la ukaribisho wakati wa kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akitoa neno kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hususan yanayohusu ulinzi na usalama kwa wanachuo wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge akitoa maelezo mafupi kuhusu malengo na majukumu ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakati wa kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe wa chuo hicho.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akitoa neno kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hususan yanayohusu ulinzi na usalama kwa wanachuo wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Haji Janab akitoa wasilisho kuhusu majukumu ya Wizara wkati wa kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe wa chuo cha Taifa cha Ulinzi

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge akitoa maelezo mafupi kuhusu malengo na majukumu ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakati wa kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe wa chuo hicho.

Mmoja wa wanachuo wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi akijitambullisha  wakati ujumbe wa chuo hicho ulipofanya ziara ya mafunzo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.

Mwanachuo akijitambulisha 

Mwanachuo akijitambulisha 
Mwanachuo akijitambulisha 

Mwanachuo akiuliza swali baada ya kusikiliza wasilisho kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Mwanachuo akiuliza swali baada ya kusikiliza wasilisho kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akijibu maswali mbalimbali yayoulizwa na wanachuo wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Mwanachuo akiuliza swali baada ya kusikiliza wasilisho kuhusu majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Mhandisi Abdillah Mataka akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Vituo vya Pamoja vya Mipakani 

Mwakilishi kutoka Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Amani Mwatonoka akifafanua masuala ya usalama katika mipaka wakati wa kikao baina ya kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Mwanachuo akitoa neno la hukrani baada ya kikao baina ya kikao baina ya uongozi wa Wizara na ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akitoa zawadi kwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge baada ya ujumbe wa chuo hicho kufanya ziara ya mafunzo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Mej. Gen. Wilbert Ibuge akitoa zawadi kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo baada ya ujumbe wa chuo hicho kufanya ziara ya mafunzo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.