Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada Mhe. John Baird baada ya mazungumzo yao tarehe 29-10-2011 |
“Serikali ya Tanzania imedhamiria kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika nyanja ya elimu ya mafunzo ya ufundi”.
Hayo yamebainishwa leo na Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. John Baird mjini Perth, Australia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Katika mazungumzo hayo, Waziri Membe alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Canada kushirikiana katika kuendeleza Sekta ya Elimu ya Ufundi nchini Tanzania ili kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana.
Waziri Membe alisema Wizara yake ina dhamana ya kushughulikia masuala ya ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani kwenye sekta tofauti ili kuleta maendeleo kwa Watanzania. Sekta ya Elimu ya Ufundi imepewa kipaumbele katika mahusiano hayo, ili kuwajengea vijana wengi zaidi nchini Tanzania uwezo wa kujiajiri baada ya kupata elimu ya ufundi.
Kwa kutambua hatua kubwa iliyopigwa na Canada katika sekta ya elimu ya ufundi, Waziri Membe aliiomba Serikali ya Canada kuisaidia Serikali ya Tanzania kujenga uwezo wa taasisi za elimu ya ufundi nchini Tanzania ili kukuza ujuzi na hatimaye uwezo wa vijana kujiajiri na kuajiriwa.
Kwa upande wake, Waziri Baird alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupiga vita umasiki na aliahidi kuwa Serikali ya Canada itakuwa tayari kuisaidia Tanzania katika Sekta ya Elimu ya Ufundi.
Pia alielezea uzoefu wa Canada kwenye sekta hiyo ambapo wahitimu wa vyuo vya Elimu ya Ufundi wamefanikiwa kupata ajira kwa urahisi zaidi kuliko wahitimu wa Elimu ya Juu.
Katika Mkutano huo mawaziri hao pia walizungumzia umuhimu wa kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Canada na Tanzania katika nyanja mbalimbali za ushirikiano na masuala ya kimataifa.
Mhe. Baird aliishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika Tume ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya afya ya wakina mama wajawazito na watoto iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiongozwa na wenyeviti wenza Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Steven Harper, Waziri Mkuu wa Canada.
Mawaziri hao pia walijadili masuala ya ushirikiano katika ulinzi wa amani na suala la ugaidi katika bahari ya hindi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.