Wednesday, July 25, 2012

Taarifa kwa vyombo vya Habari

Serikali ya Uswizi yatuma salamu za rambirambi
 
Serikali ya Uswizi imemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia ajali ya kuzama kwa Meli ya Skagit tarehe 18 Julai, 2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe katika Bahari ya Hindi ambapo watu 73 wamepoteza maisha.
 
Katika salamu zake za rambirambi kwa Rais Kikwete, Rais wa Shirikisho la Uswizi, Mama Eveline Widmer-Schlumpf amesema Serikali ya Uswizi na watu wa nchi hiyo wameshtushwa na kusikitishwa sana kutokana na taarifa za ajali hiyo.
 
“Serikali na Wananchi wa Uswizi wameshtushwa na kusikitishwa sana na habari za ajali mbaya ya meli iliyotokea kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ambapo watu wengi wamepoteza maisha”, amesema Widmer-Schlumpf katika salamu zake.
 
Amesema yeye kwa niaba ya Baraza la Shirikisho la Uswizi anatuma salamu za rambirambi kwa Serikali ya Tanzania na pole nyingi kwa familia na marafiki wa watu waliofikwa na msiba huo mkubwa.
 
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
25 Julai, 2012

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.