Thursday, July 9, 2015

MEMBE ASISITIZA UMUHIMU WA VIWANDA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Kamilius Membe (Mb.), akiongea kwenye muhadhara kabla ya Mtoa mada mkuu Prof. Justin Yifu Lin hajaongea katika muadhara uliokuwa unazungumzia umuhimu wa viwanda nchini ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje 
Makamu wa Rais wa zamani wa Benki ya Dunia, Prof. Justin Yifu Lin akitoa mada yake juu ya uwanzishaji wa viwanda nchini Tanzania katika muadhara ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Hassan Simba Yahya (Kulia), na kushoto ni Balozi Mstaafu Mhe. Elly Mtango wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Dkt. Lin (hayupo pichani). 
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje wakimsikiliza kwa makini Prof. Lin (hayupo pichani), Katikati ni Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Nigel Msangi, Kushoto ni Afisa Mawasiliano mwandamizi wa Mambo ya Nje Bw. Ally Mkumbwa nao wakifuatilia kwa makini Muhadhara uliokuwa ukiendelea 
Balozi Simba akichangia mada katika muadhara uliokuwa ukiendelea  
Muhadhiri Chuo cha Diplomasia Bw. Innocent Shoo akiuliza swali 
Afisa Mambo ya Nje Bi. Felisita Rugambwa naye akiuliza swali katika muhadhara 
Dkt Lin akijibu maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea kulizwa.
Picha ya juu na chini ni watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje nao wakisikiliza mada kwa makini
KKatibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akitoa neno la shukrani kwa Prof. Lin, kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje mara baada ya kumalizika kwa muhadhara huo
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula akizungumza jambo huku akisikilizwa na Prof. Lin (Kulia) na Mhe. Membe (Katikati). 
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Diaspora Bi. Rosemary Jairo akizungumza jambo kwa Prof. Lin (kushoto) na Katibu Mkuu Balozi Mulamula.

Picha na Reginald Philip



  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe, amesema upatikanaji wa gesi ni nyenzo muhimu ya uendelezaji wa viwanda vya kati ili kutengeneza ajira na kuharakisha maendeleo ya nchi.

Mhe. Membe alipongeza uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika itakapohamishia baadhi ya viwanda vyake, akazitaka taasisi za uwekezaji na uendelezaji wa viwanda kuweka mikakati madhubuti ya kutumia fursa hiyo kikamilifu.

Mhe. Waziri alisema hayo leo wakati wa mhadhara wa aliyekuwa Mchumi Mkuu na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Prof. Justin Yifu Lin, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam, uliohudhuriwa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na wadau wengine.

Alisema uendelezaji wa viwanda lazima utiliwe mkazo katika mpango wa Tanzania kuingia uchumi wa kati 2025. "Tuache kukimbilia viwanda vikubwa vinavyohitaji mitaji mikubwa, ambayo hatuna.Tuchague viwanda vya kati vitakavyoajiri watu wengi kwa uwekezaji wa wastani."

Mhe. Membe alisema uendelezaji wa viwanda usambae nchi nzima ili kuvutia vijana kuishi vijijini badala ya kukimbilia mijini. "Sasa hivi nchi yetu ina viwanda takriban 3,000 lakini zaidi ya theluthi mbili viko Dar Es Salaam. Lazima umeme upelekwe vijijini kuleta uwiano wa maendeleo ya viwanda," alisisitiza.

Katika mhadhara wake, Prof. Lin alisema nchi nyingi zinazoendelea zilifanya maamuzi yasiyo sahihi kuhusu viwanda. "Nchi nyingi zilifuata kile kinachoitwa Muafaka wa Washington na kuanzisha viwanda vikubwa kwa maelekezo ya nchi tajiri, ambavyo viliwashinda kuendesha kwa kuwa vilihitaji uwekezaji mkubwa sana."

Alisema nchi za Asia zilizoendelea kwa haraka ni zile zilizoamua kuzingatia mazingira halisi na kwenda hatua kwa hatua katika kuanzisha viwanda. "Hii iliimarisha uchumi wao na kuukuza."

Prof. Lin alisema serikali zina wajibu wa kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kuweka sera sahihi, kuhimiza uwekezaji kwenye uzalishaji wa bidhaa zenye masoko ya uhakika na kusaidia sekta binafsi ishiriki kikamilifu.

Akiongelea Tanzania, Mchumi huyo wa Kichina alisema ingawa gharama za ajira ziko chini, gharama za uendeshaji ziko juu, hivyo hazivutii uwekezaji. Alisema moja ya sababu kubwa za Shilingi ya Tanzania kushuka thamani ni uuzaji mdogo wa bidhaa nchi za nje.

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.