TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Taarifa kuhusu
Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki na kujeruhiwa huko Saudi Arabia
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa za kufariki kwa Mahujaji zaidi ya 700 na wengine zaidi ya 800
kujeruhiwa wakati wakishiriki ibada ya Hijja iliyofanyika Makkah, Saudi Arabia
tarehe 24 Septemba, 2015.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania, Saudi Arabia
Mahujaji hao
walifariki na kujeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea kwenye
eneo la Mina.
Aidha, taarifa hizo
zinaeleza kuwa hadi sasa Mahujaji wapatao watano (5) kutoka Tanzania wamefariki
dunia na wengine kujeruhiwa. Majina ya Watanzania waliofariki na kutambuliwa ni
Bi. Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla. Mtu mwingine
aliyefariki ni Raia wa Kenya anayeishi nchini ambaye ametambulika kwa jina la Bi. Fatuma Mohammed Jama.
Ubalozi unaendelea
na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyefariki kwenye tukio hilo.
Aidha, Serikali ya Saudia imetangaza kuwa itatoa taarifa kamili ikiwemo idadi
ya watu waliofariki na majeruhi na nchi wanazotoka mara itakapokamilika.
Pia Ubalozi wetu
kwa kushirikiana na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Hijja za Tanzania
ikiwemo BAKWATA pamoja na Mamlaka za Serikali ya Saudi Arabia unaendelea
kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo na majeruhi wengine kutoka
Tanzania.
Hivyo basi,
Wananchi wanaombwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali
ikiendelea kufuatilia.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
25 Septemba, 2015
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.