Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bi. Mindi Kasiga, akiongea na waandishi wa habari kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ambapo alizungumzia Mkutano wa Tume ya pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda uliofanyika nchini Rwanda pamoja tarehe 28 hadi 1 Mei, 2016 na Kikao cha Serikali ya Tanzania na Zambia kilichojadili utatuzi wa changamoto za mipaka kilichofanyika tarehe 27 Aprili, 2016.
Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia, Dkt. Watengele Kitojo (kushoto) akiwa na Maafisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Taasisi zake wakati wa Mkutano kati ya Wizara na Waandishi wa Habari.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikitolewa na Msemaji wa Wizara.
Wakati Mkutano ukiendelea.
================================================
================================================
Kikao cha Kumi na Nne
cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Jamhuri ya Rwanda, 29 Aprili – 1 Mei, 2016
Kikao
cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilifanyika
kuanzia tarehe 29 Aprili hadi Aprili, 2016, Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam
wa sekta mbalimbali waliazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi
hizi mbili.
Kikao
hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania
na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda
mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Wakati
wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano
ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi
baina ya nchi hizo mbili.
Wakati
wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi
Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania
aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa
kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia fursa za
ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili baada ya
mindombinu ya kikanda kuimarika.
Kwa
upande wake, Balozi Jeanine Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Rwanda na mwenyeji wa kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo
yanayotekelezeka na tarehe za ukomo kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili
kusukuma utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.
Pamoja
na mambo mengine, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika
sekta muhimu kama vile miundombinu ya ushoroba wa kati (central corridor),
kuharakisha ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa (standard
gauge), kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya
ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na
teknolojia, afya, kilimo na ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.
Mkutano
huo pia umekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint
Implementation Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya
ushirikiano yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo
itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili,
itakutana kila robo mwaka.
Aidha,
Serikali ya Rwanda imeonesha utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na Watumishi
wa Serikali kwa lengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu
nchini kama vile Chuo cha Diplomasia
(CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii na Wanyamapori (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kwa
upande wa Tanzania, Serikali imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya
elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa
mitaala ya elimu ya tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.
Mkutano
ujao wa kumi na tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya
Tanzania na Rwanda utafanyika mwaka 2018, nchini Tanzania.
WAKATI HUO HUO, Kikao cha pamoja cha
Makatibu Wakuu kati ya Tanzania na Zambia kwa ajili ya kujadili utatuzi wa
changamoto za mpaka wa Nakonde Tunduma kilifanyika Lusaka Zambia 25 hadi 27
Aprili, 2016.
Ujumbe
wa Tanzania katika Mkutano huo
uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius
Likwelile na kwa upande wa Zambia uliongozwa na Bw. Bright Nundwe, Katibu Mkuu
wa Jimbo la Muchinga.
Miongoni
mwa changamoto zilizojadiliwa na ufumbuzi wake wakati wa mkutano huo ni pamoja
na:- Msongamano wa magari ambapo kwa
upande wa Zambia huduma kwa
magari ya mizigo zinafanyika hadi saa nne usiku na kwa magari ya abiria
huduma inatolewa kwa masaa 24. Ili kupunguza msongamano, Tanzania imeiomba
Zambia kutoa huduma kwa magari ya aina zote kama Tanzania inavyotoa huduma ya
masaa 24; na Kuimarisha usalama mpakani ili kukabiliana na biashara haramu za
kubadilisha fedha, biashara za magendo na biashara haramu za binadamu.
Mwisho,
pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lishughulikiwe kwa kufanya ukaguzi na
ulinzi wa pamoja na kubadilishana taarifa za kiusalama.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa,
05
Mei, 2016
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.