Taarifa
kuhusu Ziara ya Rais wa Benki ya Dunia nchini Tanzania
Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim, atafanya
ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 21 Machi 2017. Akiwa nchini, Dkt.
Kim atafanya mazungumzo na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ikulu Jijini Dar Es Salaam siku ya Jumatatu, tarehe 20
Machi 2017 pamoja na kushiriki uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara
za Juu katika eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).
Katika mazungumzo yao, Viongozi hao watajadili
namna bora ya kuimarisha zaidi uhusiano uliopo kati ya Tanzania na benki hiyo. Vilevile,
watazungumzia miradi mikubwa inayotarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya
Dunia katika kipindi kijacho.
Aidha, baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli na
mgeni wake watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba mitatu: (i) Uboreshaji Miundombinu ya Usafiri Jijini
Dar es Salaam ikiwemo awamu ya tatu na ya nne ya mradi wa DART pamoja na ujenzi
wa barabara ya juu katika eneo la Ubungo (Dar es Salaam Urban Transport Project
(DUTP); (ii) Awamu ya pili ya mradi wa Uboreshaji
wa Upatikanaji wa Maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya maji taka (Water
and Sanitation Project) na (iii) Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za msingi katika baadhi ya miji (Tanzania Strategic
Cities Project).
Wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kim atapata pia fursa ya
kutembelea Shule ya Msingi Zanaki ambayo ni moja ya Shule zinazonufaika na
mpango wa kuboresha elimu ya msingi unaogharamiwa na Benki ya Dunia.
Ziara ya Dkt. Kim inafuatia ziara iliyofanywa
nchini na Makamu wa Rais wa Benki hiyo wa Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop mwezi
Januari 2017 ambapo alishiriki uzinduzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi (BRT)
uliofanyika kwenye kituo kikuu cha mabasi hayo kilichopo Kariakoo jijini Dar Es
Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Machi, 2017
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.