Thursday, March 23, 2023

DKT. TAX AKUTANA NA BALOZI WA SWEDEN NA MWAKILISHI MKAZI WA ICRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amekutana na Balozi wa Ufalme wa Sweden nchini, Mhe. Charlotta Ozaki Macias na Mwakilishi Mkazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu Duniani (ICRC) Bw. Bart Vermeiren  ofisini kwake jijini Dodoma.

Akizungumza na Balozi wa Sweden nchini, Dkt. Tax amemuhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili na kusimamia miradi ya ushirikiano kwa maendeleo na ustawi wa watu wake.

Pia ameishukuru Serikali ya Sweden kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za elimu; afya; Uwekezaji na biashara; Teknolojia ya Habari, Usafirishaji na  Miundombinu; Nishati; Madini; Utafiti; maboresho kwenye mifumo ya ukusanyaji wa kodi; uchangiaji wa bajeti kuu ya Serikali; Misuti; Demokrasia, Haki za binadamu, Usawa wa jinsia; Utunzaji wa mazingira; na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Naye Balozi Charlotta Macias ameeleza kuwa wakati huu ambapo Tanzania na Sweden inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa rasmi kwa ushirikiano wa kidiplomasia ingependa kushirikiana na Tanzania katika shughuli mbalimbali zilizoandaliwa katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo.

Aidha, amefafanua kuwa miongoni mwa shughuli za maadhimisho hayo ni; Kukutana na Wahitimu wa kitanzania waliosoma nchini Sweden katika ngazi mbalimbali ambapo watajadili shughuli wanazozifanya na malengo yao ya baadae.

Vilevile akafafanua kuwa shughuli kama hizo za maadhimisho zitakuwa zikifanyika na ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden ambapo hivi karibuni kuliitishwa mkutano mkubwa wa Watanzania wanaoishi nchini Sweden ambao kwa upande wa Serikali ya Tanzania uliwakilishwa na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kwamba hiyo ni moja ya jitihada zinazofanywa na serikali zetu katika kuimarisha ushirikiano.

Pia, akaeleza kuwa Sweden itaungana na nchi nyingine za Nordic kuadhimisha wiki ya Nordic itakayofanyika tarehe 29 Mei 2023 hadi tarehe 1 Juni 2023 katika maadhimisho yanayotarajiwa kuwakutanisha Mabalozi wanaowakilisha nchi za Nordic nchini, nchi marafiki wa Nordic na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania.

Pamoja na ushirikiano uliopo kati ya Sweden na Tanzania katika miradi ya maendeleo, kampuni za kutoka nchini Sweden zimewekeza nchini katika sekta mbalimbali ambazo ni pamoja na kampuni ya Ericsson, Tigo, Scania na kampuni za uchimbaji wa madini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Tax amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) Bw. Bart Vermeiren aliyefika ofisini kwake kujitambulisha. 

Katika mazungumzo yao Dkt. Tax amemuhakikishia Bw. Vermeiren kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na ICRC katika kuhakikisha kuwa Tanzania wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu kuanzishwa kwa kamati ya kitaifa ya ICRC.

“Karibu sana Tanzania, nikuhakikishie kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi na ICRC Tanzania, ili wadau wapate uelewa wa pamoja na hivyo kurahisisha kuanzishwa kwa kamati ya Kitaifa,” alisema Dkt. Tax.

Naye Bw. Bart Vermeiren amemhakikishia Mhe. Wazirii kuwa ICRC Tanzania itaendelea kufanya kazi na Tanzania na kumuahidi kuwa Kamati hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania ili kufanikisha azma ya Tanzania kuanzisha kamati ya kitaifa katika eneo la kujenga uwezo katika Sheria za Kimatifa za msaada wa kibinadamu.

Ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa nchi ya amani katika ukanda wake. Pia amewapongeza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushinda mashindano ya Sheria za Kimataifa za Msaada wa Kibinadamu kwa bara la Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu Duniani (ICRC) Bw. Bart Vermeiren walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisalimiana na Balozi wa Ufalme wa Sweden nchini Mhe. Charlotta Ozaki Macias walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu Duniani (ICRC) Bw. Bart Vermeiren yaliyofanyika jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Ufalme wa Sweden nchini Mhe. Charlotta Ozaki Macias yaliyofanyika jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Mwakilishi Mkazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu Duniani (ICRC) Bw. Bart Vermeiren wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara na ICRC.
Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Ufalme wa Sweden nchini Mhe. Charlotta Ozaki Macias yakiendelea. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Ufalme wa Sweden nchini Mhe. Charlotta Ozaki Macias wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara na Ubalozi. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.