Mhe. Mahiga alisema kuwa uamuzi huo
ambao haukuishirikisha Tanzania kwa namna yoyote umetolewa na Bodi ya MCC
ambayo imekutana Jijini Washington DC hivi karibuni.
Katika maelezo yake, Waziri Mahiga
alisema kuwa, Awamu ya Kwanza ya mpango huo ilitolewa na Marekani baada ya
Tanzania kukidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia,
kupambana na rushwa, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu.
Hata hivyo alieleza kushangazwa kwake
na uamuzi wa sasa wa nchi hiyo wa kuahirisha kuipatia Tanzania fedha za awamu ya pili ya mpango huo kwa
madai kuwa haikukidhi vigezo hususan kwa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na
kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mitandao ambayo wamedai inawanyima wananchi
uhuru wa kujieleza.
“Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa
Marekani wa kuinyima fedha za MCC kwa madai kuwa hatujakidhi vigezo ambavyo ni
vigezo hivyo hivyo walivitumia kutupatia awamu ya kwanza ya fedha hizo. Ni
matumaini yangu kuwa watatafakari upya uamuzi wao” alisema Balozi Mahiga.
Kuhusu, Zanzibar Balozi Mahiga
alifafanua kuwa ni nchi huru ambayo inaendesha mambo yake kwa uhuru hususan
masuala ya uchaguzi ambayo si ya muungano. Hivyo uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) ya kufuta uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba 2015 baada ya
kutokea kasoro huko Pemba, ulikuwa ni uamuzi wa Tume na unatakiwa kuheshimiwa.
Aidha, kuhusu Sheria ya Makosa ya
Mitandao ya Mwaka 2015 (Cyber Crime Act), Balozi Mahiga alieleza kuwa
nayo kwa kiasi kikubwa ilianzishwa ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi na
uhalifu mwingine wowote unaofanyika kupitia mitandao.
“Kwa mantiki hiyo, Tanzania haikupaswa
kuadhibiwa kwa kuangalia masuala hayo pekee wakati kwa muda mrefu Tanzania
imejijengea sifa ulimwenguni kote ya kufuata misingi ya demokrasia na utawala
bora,” alisisitiza Balozi Mahiga.
Akizungumzia uhusiano kati ya Tanzania
na Marekani, Waziri Mahiga alisema kuwa unaendelea kama kawaida kwani MCC ni
kipengele kimoja tu katika masuala mengine mengi ya ushirikiano kati ya nchi
hizi mbili.
“Marekani imekuwa ni mshirika mkubwa
wa maendeleo wa Tanzania ambapo kila mwaka huipatia nchi yetu msaada wa kiasi
cha Dola za Marekani milioni 700 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali
ikiwemo ya elimu na afya. Hivyo MCC ambayo ni mpango mwingine wa msaada kutoka
nchi hiyo ni sehemu ya mambo kadhaa tunayoshirikiana na Marekani” alifafanua
Dkt. Mahiga.
Akielezea athari zitakazotokana na
kukosekana kwa fedha hizo za Awamu ya Pili ya MCC, Mhe. Mahiga alisema kuwa kwa
kiasi fulani Tanzania itaathirika hususan katika eneo la usambazaji wa Nishati
ya Umeme Vijijini. Hivyo alisisitiza umuhimu wa Marekani kutafakari upya uamuzi
wao huo.
“Marekani inazitaka nchi zipambane na
kuondokana na umaskini. Umoja wa Mataifa nao umeanzisha Malengo ya Maendeleo
Endelevu ambayo yanalenga kupambana na umaskini. Hata hivyo nasikitika kuwa kuondolewa
kwa MCC Tanzania hakutaiwezesha kufikia malengo ya milenia wala dhamira njema
ya Marekani ya kuzitaka nchi zinazoendelea kuondokana na umaskini. Kwa maana
nyingine nasema ni Malengo ya Milenia na MCC dhidi ya Tanzania”, alieleza Dkt.
Mahiga.
Tanzania ni miongoni mwa nchi
zilizonufaika na Mpango wa kukabiliana na Changamoto za Milenia (MCC) ambapo katika
awamu ya kwanza ya mpango huo, Tanzania ilipatiwa kiasi cha Dola za Marekani
Milioni 698.
Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kufanikisha miradi ya
maendeleo katika uboreshaji wa maeneo ya miundombinu ya barabara za
Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Pia zilitumika kujenga mfumo wa maji
kwa miji ya Dar es Salaam na Morogoro. Vile vile fedha hizo zilitumika
kutandaza njia ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na
Tanzania Visiwani na pia kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na
baadhi ya barabra za Unguja kwa kiwango cha lami.
-Mwisho-