TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watumishi wa umma Zanzibar wapigwa msasa kutekeleza Mipango ya Serikali
Taasisi
za Umma zimeshauriwa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mipango
iliyojiwekea badala ya kutumia muda mwingi kupanga mipango
isiyotekelezwa.
Ushauri
huo umetolewa leo kwenye warsha ya kuwajengea uwezo watendaji wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuingiza Mpango kazi wa utelezaji wa APRM
kwenye mipango ya maendeleo ya nchi kama vile Dira ya Zanzibar 2020,
MKUZA III na Mipango ya Matumizi ya Muda wa Kati.
Warsha
hiyo ya siku mbili imeandaliwa na APRM Tanzania na inafanyika katika
Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 24 na 25 Agosti 2017.
Mgeni
Rasmi kwenye warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba,
Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Kubingwa Mashaka Simba
ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Haroun Ali Suleiman
aliwahakikishia washiriki kuwa Serikali ya Zanzibar imejipanga vema
kutekeleza changamoto zote zilizobainishwa kwenye ripoti ya APRM
iliyowasilishwa rasmi kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwezi Agosti 2017.
Bw.
Simba alieleza kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishachukua
hatua za kuimarisha Utawala Bora ikiwemo kuunda taasisi za kusimamia
suala hilo ambazo baadhi yao ni Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na
Tume ya Kupambana na Rushwa pamoja na ugatuzi wa madaraka.
Wadau
wanaoshiriki warsha hiyo walibainisha kuwa changamoto kubwa katika
taasisi za umma ni utekelezaji wa mipango iliyowekwa, Hivyo kuna umuhimu
wa APRM kuangalia namna ya kujenga uwezo wa watumishi katika kutekeleza
mipango ya Serikali kwa kuzingatia namna ya kupata rasilimali
zinazohitajika na zenye uwezo wa kutekekeza mipango iliyopo pamoja na muda
wa kutekeleza mipango hiyo.
Kwa
upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM, Tanzania, Bi. Rehema Twalibu
alisema warsha hiyo ni muhimu kwa watumishi wa Serikali ya Zanzibar kwa
kuwa itawapa uwezo wa kuandaa taarifa ya utekelezaji wa changamoto
zilizoainishwa kwenye ripoti ya APRM iliyowasilishwa miaka mitano
iliyopita kwa Wakuu wa Nchi zilizoridhia Mpango wa APRM.
Taarifa
ya utekelezaji itakayoandaliwa na Serikali ya Zanzibar itajumuishwa na
taarifa ya Tanzania Bara ili kupata ripoti moja ambayo inatarajiwa
kuwasilishwa na Mhe. Rais kwa Marais wenzake wanaounda APRM baadaye
mwaka huu.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Zanzibar, 24 Agosti 2017
|