Saturday, November 21, 2020

PROF. KABUDI: TUTASHIRIKIANA NA TAIFA LOLOTE LINALOIHESHIMU TANZANIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema Tanzania itashirikiana na nchi yoyote duniani ambayo inatambua na kuheshimu Uhuru wa nchi na utu wa watu wake. 


Prof. Kabudi ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipozungumza na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zake tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. 

"Tutafanya kazi na nchi zote ambazo zinatuheshimu, zinatutambua kama Taifa huru, kutuheshimu sisi kama binadamu wa mataifa mengine, hatutakubali kudharauliwa, kutokuheshimiwa utu wetu na kudharauliwa kwa sababu ya misaada au pesa’, amesema Prof. Kabudi 

Ameongeza kuwa Tanzania itasikiliza taifa lolote duniani na kujadiliana nalo kwa heshima kwani mapungufu hayapo upande mmoja tu. 

"Tuko tayari kuwasikiliza na kujadiliana nao kwa heshima na kama wanadhani kuna kitu kimepungua kwetu na sisi tunadhani kimepungua kwao," amesema Prof. Kabudi. 

Amesema Tanzania haiwezi kumruhusu mtu yeyote atumie misaada ya fedha kuondoa uhuru wetu na kutokuthamini utu wetu. 

Amesema Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa na itaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kidunia kama vile kulinda amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutunza mazingira. 

"Hatutajitenga katika dunia hii, tutaendelea kujumuika katika kazi mbalimbali kama vile ulinzi wa amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuhifadhi mazingira,’ alisema na kuongeza kuwa tumekuwa bandari ya amani kwa wakimbizi sio tu kutoka Afrika bali duniani kote na tutaendelea kuwa hivyo," Ameongeza Prof. Kabudi. 

Prof. kabudi pia amewataka watumishi wa Wizara kusoma kitabu cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alichowaandikia watumishi wa wizara hiyo mwaka 1969 cha Usipayuke toa hoja ‘Don’t shout argue’ ili kutoa takwimu sahihi kwa wakati. 

Amesema jukumu la kuieleza dunia kuhusu takwimu za vitu mbalimbali ni la watumishi wa Mambo ya Nje na hawana budi kuhakikisha wanaliekeleza hilo kwa ufasaha. 

Mbali na kitabu hicho, Prof. Kabudi amewakabidhi wakurugenzi wa Idara mbalimbali Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hotuba za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati anafungu Bunge la 11 na hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 12 na kuwataka kusimamia na kutekeleza maagizo yote yaliyopo kwenye hotuba hizo pamoja na maelekezo ya Ilani ya CCM. 

Awali akimkaribisha Waziri kuzungumza na watumishi, Katibu Mkuu Wizara Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wibert Ibuge aliwapongeza watumishi utendaji mzuri wa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimpokea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipokuwa anawasili kwenye kikao cha wafanyakazi jijini Dodoma


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na watumishi (hawapo pichani) kwenye mkutano wa Waziri Prof. Kabudi na Watumishi wa Wizara ulifanyika Jijini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge Ilani ya CCM na nyaraka nyingine za utendaji  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akimkabidhi nyaraka Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora Balozi, Anisa Mbega


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akimkabidhi nyaraka Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Bibi. Caroline Chipeta  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akiongea na Watumishi wa wizara  katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma



Friday, November 20, 2020

TANZANIA YAAHIDI KUENDELEA KUISAIDIA CONGO KULINDA AMANI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kuisaidia Congo kulinda amani na kuhakikisha changamoto za  ulinzi na usalama zinazoikabili nchi hiyo zinatatuliwa ili kuimarisha hali ya amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika kwa njia ya video (Video Conference).

"Tanzania tutaendelea kusaidia juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo la mashariki mwa Congo - DRC kwani kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama kwa nchi hiyo kunahatarisha usalama wa eneo lote la Jumuiya nzima ya ICGLR nayo itakuwa salama," amesema Prof. Kabudi.

Ameongeza kuwa Congo Brazaville ilikuwa ikikabiliwa na uasi kutoka kundi la Ninja lililokuwa  likiisumbua Serikali  kwa miaka mingi hata hivyo hadi kufikia katikati ya mwaka 2019 uasi ulitulia kufuatia mazungumzo ya kusitisha  mapigano kati ya kundi hilo na Serikali.

Amesema Congo-Kinshasa na Congo-Brazaville ni muhimu katika eneo la maziwa makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali za misitu, maji na madini ambavyo vinahitajika sana duniani na kuongeza kuwa umuhimu zaidi unahitajika kutokana na ukweli kuwa kuna haja kubwa ya kutunza mazingira, kuzalisha nishati na kukuza uchumi wa dunia.

"Nchi hizi mbili za DRC na Congo Brazaville ni nchi muhimu sana katika eneo la Maziwa Makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali, baadhi ya rasilimali hizo kama misitu, maji na madini zinahitajika sana duniani kwa sasa kutokana na umuhimu wake, umuhimu ambao unatokana na haja ya kutunza na  kulinda mazingira, uzalishaji wa nishati na kukuza uchumi wa dunia," alisema n kuongeza kuwa Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama katika nchi hizi kunahatarisha usalama wa eneo lote la Maziwa Makuu ikiwemo na usalama wa dunia kutokana na uwezekano wa baadhi ya mataifa makubwa kugombea rasilimali hizo", alisisitiza Prof. Kabudi.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya ICGLR umepokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu Jumuiya hiyo , mbali na hali ya kisiasa na kiusalama katika Ukanda huo umeangalia pia suala la michango ya wanachama katika bajeti ya Sekretariat na Mfuko Maalum wa maendeleo, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi  kuhusu hali ya usalama wa Ukanda wa Maziwa Makuu na taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Afya.

Nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Kati, Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

Oktoba 2019, Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulifanyika nchini Congo Brazzaville.

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kumuaga Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Bw. Alex Mubiru ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru Bw. Mubiru kwa mema aliyoyafanya hapa nchini hasa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua kimaendeleo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akifuatilia Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika kwa njia ya video (Video Conference) jijini Dodoma

Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) 


Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa Bw. António Guterres akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)


Rais wa Jamhuri wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) 



 

Wednesday, November 18, 2020

BALOZI BRIGEDIA JENERALI WILBERT A. IBUGE ATOA SOMO KWA WABUNGE KUHUSU DIPLOMASIA NA ITIFAKI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada mbele ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa ajili ya kuwaweka sawa katika eneo la Itifaki na Diplomasia

Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiendelea kutoa mada kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania eneo la Itifaki na Diplomasia.

Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akitoa somo kwa Wabunge


Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiendelea kutoa somo kwa Wabunge



Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akitoa somo kwa Wabunge huku Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Akson na Katibu wa Bunge Bw. Stephen Kigaigai wakimsikilizaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ametoa somo la Diplomasia na Itifaki kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Ibuge ametoa somo hilo tarehe 16 Novemba 2020 katika semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Katika Semina hiyo, Balozi Brig. Gen. Ibuge aliwaeleza Wabunge hao kwa ujumla kuhusu dhana ya Itifaki; Itifaki ya Viongozi wa Kitaifa; Itifaki katika mawasiliano ya Viongozi; Itifaki ya mawasiliano rasmi na Balozi zilizopo hapa nchini.

Dhana nyingine ni pamoja na Itifaki ya upeperushaji Bendera na mipaka yake; Itifaki ya mavazi kwa viongozi pamoja na mambo mengine kuhusu Itifaki kwa Wabunge na Viongozi wote nchini.

Semina hiyo ililenga kuwajengea Wabunge uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya Diplomasia na Itifaki ikiwa ni moja ya masuala muhimu ya kuyafahamu kama zilivyo sheria na taratibu mbalimbali ambazo kwa namna moja ama nyingine watakutana nazo katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Kibunge.





Tuesday, November 17, 2020

WATUMISHI WA WIZARA WALIVYOMPOKEA WIZARANII MHE. PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI BAADA YA KUAPISHWA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi baada ya kuwasili Wizarani Mtumba akitokea Ikulu ya Chamwino alipoapishwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili cha Serikali ya awamu ya Tano tarehe 16/11/2020

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea shada la maua kutoka kwa mtumishi wa wizara alipokaribishwa Wizarani baada ya kuapishwa.


Matukio katika picha yakionesha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alipopokelewa na menejimenti na watumishi wa Wizara alipowasili Wizarani baada ya kuapishwa










 

 

 

 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Katibu Mkuu mara baada ya kuwasili
 

Katibu Mkuu  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kuzungumza na menejimenti ya Wizara baada ya kukaribishwa Wizarani

 


 Kikao kikiendelea

Monday, November 16, 2020

PROFESA KABUDI AKIAPISHWA KUWA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

 

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiapa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na Mhe. Dkt. Philip Mpango wakiapa, Ikulu Chamwino jijini Dodoma. Mhe. Dkt. Philip Mpango ameapa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango

Saturday, November 14, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.

Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika.

katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini  na Azimio la Sirte la mwaka 1999. 

Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.

Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka. 

Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono  mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa na nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.

Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufanikisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo. 

Viongozi hao pia wamejadiliana na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke alipokutana naye ofisini kwake jijini Dodoma.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Balozi Wang Ke akizungumza katika kikao hicho 






Friday, November 13, 2020

WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI WAHIMIZWA KUTANGULIZA MASLAHI YA TANZANIA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na kuwahimiza kutanguliza  maslahi ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Ibuge amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na Wabunge hao na kusisitiza kuwa maslahi ya Tanzania ni lazima yawe kipaumbele chao katika kutekeleza majukumu yao  ili kufanikisha ushiriki wa Tanzania kikamilifu katika mtangamano wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 “Endeleeni kushikilia msimamo wa kutanguliza maslahi ya Tanzania siku zote, muendelee kufanya kazi hiyo nzuri  kwenye masuala mengine yote yanayogusa maslahi ya nchi yetu,” amesema Balozi Ibuge na kuongeza kuwa nafasi yao kama wabunge wa Afrika Mashariki inatokana na uwepo wa jimbo lao ambalo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mtangamano huo.

Balozi Ibuge pia amewataka Wabunge hao kuwasiliana mara kwa mara na Serikali ili kupata maoni, ushauri na msimamo wa Serikali katika kujadili na kupitisha masuala mbalimbali ndani ya bunge hilo.

Balozi Ibuge amewataka wabunge hao kujiepusha na migogoro ndani ya Bunge na Jumuiya kwani kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kujiweka sawa katika nyanja za siasa na diplomasia na kuwapongeza kwa utendaji kazi wao na hasa jinsi walivyoshughulikia suala la Muswada binafsi wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Adam Kimbisa aliishukuru Wizara kwa kukutana nao kuwapa muongozo wa namna ya kushughulikia mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya Bunge na Jumuiya kwa ujumla.

Mhe. Kimbisa alimuahakikishia Katibu Mkuu kuwa Wabunge hao  wataendelea kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa katika hatua zote za mtangamano kupitia ushiriki wao katika Bunge la Afrika Mashariki.

 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ofisini kwake Jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika Picha ya pamoja na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma