Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika.
katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini na Azimio la Sirte la mwaka 1999.
Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.
Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka.
Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa na nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.
Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufanikisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.
Viongozi hao pia wamejadiliana na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.