Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) zimekubaliana kuboresha mfumo utakao weka ulinzi bora na usalama ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akithibitisha
kuhusu mashirikiano ya mfumo wa kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amemuwakilisha
Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika
mkutano huo amesema kuwa kamati ya utatu inayoshughulika na usalama ndani ya
jumuiya ya SADC imekutana kwa dharura ili kuweza kuangalia namna ya kukabiliana
na matishio ya ugaidi yanayotishia sana hali ya amani na usalama katika nchi
zilizopo ukanda wa SADC ikiwemo Msumbiji, Congo DRC na Tanzania.
Mkutano
huo wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,
Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya
Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji
umefanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020 mjini Gaborone, Botswana ambapo
pamoja na mambo mengine umeangalia masuala mbalimbali yanayohusu amani, ulinzi
na Usalama ndani ya SADC.
"Tumeangalia
kwa undani mapendekezo mapya ya mfumo wa ulinzi katika enao la DRC ambapo nchi
tatu zinazoshiriki katika kuimarisha Ulinzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo ambapo nchi tatu zinashiriki kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC
(Tanzania, Malawi na Afrika Kusini) kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa
zitaendelea kuimarisha masuala ya amani, Ulinzi na usalama Nchini DRC kwa
kutumia mfumo mpya utakao weka ulinzi bora na amani nchini DRC," Amesema
Mama Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza
kuwa, kupitia mkutano huo pia limejadiliwa suala la hali halisi ya usalama
ndani ya nchi wanachama ndani ya SADC na kuona jinsi ya kutumia usalama wetu
kwa ajili ya kujenga uchumi wa ukanda wetu wa kusini mwa Afrika
Kwa
upande wake Rais wa Botswana, Dkt. Mokgweetsi Masisi ambae pia alikuwa
Mwenyekiti wa Mkutano huo amezipongeza nchi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania pamoja na Visiwa vya Shelisheli kwa kufanya chaguzi ambazo zilikuwa
huru, haki na amani na kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano huo wa kuwa na
demokrisia ya uhuru, amani na haki.
"Matokeo
ya chaguzi hizo ni mfano mzuri kwetu sisi kama nchi wanachama wa SADC kujifunza
mfano kutoka kwa wenzetu," Amesema Dkt. Masisi.
Dkt.
Masisi ameongeza kuwa pamoja kufanya chaguzi huru haki na za amani, kuna mambo
ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa SADC kama vile, Ugaidi, uhalifu
wa kimtandao na vikundi vya waasi jambo ambalo limepelekea wakuu wan chi na
serikali kukutana hapa (Botswana) na kujadili namna ya kukabiliana na
changamoto hizo kwa kuwa changamoto hizi siyo za nchi moja moja bali na
kuzitaka nchi zote kuungana na kukabiliana na vikundi hivyo vya kigaidi.
"Mtakumbuka
kuwa katika mkutano wetu wa SADC uliofanyika mwezi wa nane mwaka huu tulitoa
ripoti iliyoonesha kuwa na baadhi ya ugaidi kwa baadhi ya nchi zetu za SADC,
pamoja na ripoti kuonyesha kuwa kuna hali ambayo siyo shwari kwa baadhi ya nchi
wananchama, kuna haja ya kuungana pamoja na kuhakikisha kuwa vikundi hivi vya
kigaidi vinatokomezwa katika ukanda wetu wa SADC," Amesema Dkt. Masisi.
"Ni
jukumu letu sote kuipa ushirikiano Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo hasa upande
wa Mashariki mwa DRC na kuhakikisha kuwa amani ya nchi hiyo inalindwa kwa
kutokomezwa kwa vikundi vya kigaidi vinavyochangia kutoweka kwa amani nchini
humo, na ndiyo maana leo tumekutana hapa ili tuweze kuona na jinsi gani ya
kumsaidia mwenzetu DRC," Ameongeza Dkt. Masisi
Pamoja
na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama inawajibika kukuza amani na usalama katika
eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi Wanachama mwongozo
kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.
Ni
mara ya kwanza kwa Wakuu wan chi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC - TROIKA) kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa Homa
Kali ya Mapafu (Covid-19).
Mkutano
huo ulihudhuriwa na, Rais wa Botswana Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi, Rais wa
Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Cyril
Ramaphosa, Rais wa Malawi Mhe. Lazarus Chikwera, Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi, Makamu wa Rais wa jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya
Msumbiji Bw. Jaime Neto aliyemuwakilisha Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi wakati wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano
wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na
amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji uliofanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020,
mjini Gaborone Botswana
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi wakati wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano
wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na
amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji uliofanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020,
mjini Gaborone Botswana
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.