Mhe. Membe na Mhe. Simmonds katika picha ya pamoja. |
Mhe. Membe akizungumza na Mhe. Simmonds kuhusu masuala ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. |
Ujumbe ulioambatana na Mhe. Simmonds. |
Mhe. Simmonds akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo. |
Na Rosemary Malale, New York
TANZANIA
YAIPONGEZA UINGEREZA KWA KUANZISHA HUDUMA YA VIZA ZA HARAKA KWA WATANZANIA
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ameishukukuru na
kuipongeza Serikali ya Uingereza kwa kuanzisha huduma mpya itakayowawezesha
Watanzania kupata viza za kuingia nchini humo kwa haraka.
Huduma hiyo ambayo
ilitangazwa na nchi hiyo hivi karibuni kupitia Balozi wa Uingereza nchini
Tanzania, Mhe. Diana Melrose ni moja ya mipango ya nchi hiyo ya kuimarisha
uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Huduma hiyo hukamilika kwa takribani siku tano hadi kupata viza.
Akizungumza hivi
karibuni na Naibu Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Mambo ya Nje na Jumuiya
ya Madola, Mhe. Mark Simmonds Mjini New York, Marekani wakati wa Kikao cha 68
cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mhe. Membe alisema kuwa anaishukuru nchi
hiyo kwa kuichagua Tanzania katika mpango huo ikiwa ni mshirika wake muhimu wa
maendeleo na kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa haraka katika
siku za hivi karibuni hivyo itarahisisha na kuimarisha biashara baina ya nchi
hizi mbili.
Aidha, Mhe. Membe
aliongeza kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakijishighulisha na biashara
mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Uingereza hivyo mpango huo wa viza za
haraka utawasaidia kuimarisha biashara zao badala ya kukatishwa tamaa na
mlolongo mrefu wa kufuatilia viza uliokuwepo hapo awali.
“Tunaishukuru sana
Serikali ya Uingereza kwa kuanzisha huduma hiyo ya utoaji viza za haraka, hata
hivyo bado tunaiomba ifikirie tena uwezekano wa kurejesha huduma ya utoaji viza
Jijini Dar es Salaam badala ya kufuatilia viza hizo Nairobi nchini Kenya”, alisema
Waziri Membe.
Aidha, aliomba
kiwango cha nyongeza kilichowekwa cha shilingi laki mbili na nusu kwa ajili ya
kukamilisha mchakato wa viza hiyo ya haraka kipunguzwe kwani ni kikubwa kwa
Watanzania.
Akizungumza kwa
upande wake, Mhe. Simmonds alisema kuwa Uingereza itaendelea kuimarisha
ushirikiano na Tanzania hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Mkutano huo wa Mhe.
Waziri Membe na Mhe. Simmonds ulihudhuriwa na Wajumbe wengine akiwemo Mkurugenzi
wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Dora Msechu.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.