Saturday, March 21, 2015

Rais Kikwete ampongeza Rais Mpya wa Namibia Dkt.Hague Geingob

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Rais Mpya wa Namibia Dkt.Hage Geingob wakati wa sherehe za kuapishwa kwake zilizofanyika katika Uwanja wa michezo wa Uhuru wa Namibia jijini Windhoek Machi 21, 2015 .Sherehe za kumuapisha Rais huyo wa tatu wa Namibia ziligongana na maadhimisho ya miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo


================================================
NAMIBIA MACHI 21,2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Machi 21, 2015, ameungana na viongozi mbalimbali wa Afrika na wananchi wa Namibia katika kusherehekea miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa Rais wa Tatu wa Namibia, Mheshimiwa Dkt. Hage Gotfried Geingob.
Mheshimiwa Geingob alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba 28, mwaka jana, uliokipa ushindi mkubwa chama tawala cha SWAPO. 
Katika sherehe kubwa na ya kufana iliyofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Independence mjini Windhoek, Rais Kikwete ameshuhudia Namibia ikiadhimisha miaka 25 ya Uhuru wake na makabidhiano ya uongozi wa juu wa nchi hiyo kwa amani kwa mara ya pili katika historia yake. 
Mheshimiwa Dkt. Geingob ameapishwa rasmi na Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Peter Shivute saa sita na dakika 25 kwa saa za Afrika Mashariki, kiapo ambacho kilifuatiwa na kiapo cha Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu. 
Ujumbe wa Tanzania katika sherehe hizo uliwashirikisha pia marais wa zamani, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais Ben Mkapa, ambao wote waliwasili mjini Windhoek usiku wa jana kwa ndege maalum ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Rais Kikwete ambaye aliwasili Namibia jioni ya jana, Ijumaa, Machi 20, 2015, kwa ajili ya sherehe za leo, ameungana na viongozi wengine kushuhudia nchi nyingine mwanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikibadilisha viongozi wakuu kwa njia ya amani katika mwaka mmoja uliopita. 
Kabla ya sherehe ya leo ambako Rais Hifikepunye Lucas Pohamba amekabidhi urais wa Namibia kwa Rais mpya, Mheshimiwa Dkt. Hage G. Geingob, nchi nyingine ambazo zimebadilisha viongozi katika mwaka mmoja uliopita ni Malawi, Mozambique na Zambia. 
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine ambao wamehudhuria sherehe hizo ni pamoja na Mfalme Mswati wa Tatu wa Swaziland, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na SADC, Mheshimiwa Robert Mugabe wa Zimbabwe, Baba wa Taifa la Namibia, Mzee Sam Nujoma, Rais wa Angola, Mzee Jose Eduardo Dos Santos, Rais wa Equatorial Guinea Mheshimiwa Obiang Nguema, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Mheshimiwa Nkozana Dlamini Zuma, Rais wa Mozambique Mheshimiwa Felipe Nyusi na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta. 
Wengine ni Rais Khama Ian Khama wa Botswana, Rais Edgar Lungu wa Zambia, Rais wa Sudan Kusini Mheshimiwa Salva Kiir, Rais  Denis Sassou Ngwaso wa Jamhuri ya Congo, Waziri Mkuu wa Ethopia Mheshimiwa Haile Mariam Desaleny na Naibu Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Cyril Ramaphosa. 
Mbali na Mzee Mwinyi na Rais wa Tatu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, baadhi ya viongozi wa zamani waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja Rais Kenneth Kaunda wa Zambia, Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Rais Jerry Rawlings wa Ghana, Rais Festus Mogae wa Botswana. 
Sherehe hizo zimegawanywa katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ikiwa ni Sherehe za Miaka 25 ya Uhuru na sehemu ya pili ikiwa ni Sherehe ya kuapishwa kwa Rais Hage Gotfried Geingob, ambaye anakuwa Rais wa Namibia akifuata nyayo za Mzee Nujoma na Rais Pohamba. 
Rais Geingob ni kiongozi wa kitaifa wa miaka mingi katika Namibia, akiwa ameshikilia nafasi ya Uwaziri Mkuu mara mbili. Awali kabisa, Hage Gotfried Geingob alikuwa mwalimu wa lugha ya Kiingereza, kabla ya kujiunga na harakati za ukombozi wa Namibia chini ya chama cha SWAPO. 
Mwaka 1971, Mheshimiwa Geingob alikuwa mwakilishi wa chama cha SWAPO katika Umoja wa Mataifa na katika nchi za Marekani na mwaka 1975 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Umoja wa Mataifa (UN Namibian Institute) kwa ajili ya Namibia kilichokuwa mjini Lusaka, Zambia. 
Mheshimiwa Geingob alikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyotunga Katiba ya Namibia huru na mwaka 1989 alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama cha SWAPO kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka uliofuata 1990 ambao chama hicho kiliushinda kwa kura nyingi. 
Baada ya uchaguzi huo, Mheshimiwa Geingob alichaguliwa kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda, kabla ya kuchaguliwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, ambako alithibitisha kuwa kiongozi mwenye ufanisi na mwenye kuhakikisha mambo yanafanyika vizuri na kwa haraka. Aidha, alikuwa mwanzilishi wa Sera ya Maridhiano katika Namibia kufuatia uchaguzi mkuu huo wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo.
Ends

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.