Balozi Mbelwa akimkabidhi Balozi Liu zawadi ya majani ya chai na kahawa ya Tanzania
Picha na Reginald Philip
=================================
|
Tanzania na China kuendeleza
ushirikikiano katika Sekta ya Uwekezaji na Viwanda
Na Mwandishi Maalum
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha amaihakikishia Serikali ya China
kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu na kwamba inawaribisha
wawekezaji kutoka nchi hiyo.
Balozi Gamaha aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam
alipokutana na ujumbe wa Maafisa kutoka China ukiongozwa na Mkurugenzi wa Idara
ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Balozi Liu Songtian. Ujumbe
huo upo nchini kwa ziara ya kikazi ya kufuatilia hatua zilizofikiwa na Serikali
ya Tanzania juu ya uamuzi wa China wa kuzifanya nchi tatu za Afrika ikiwemo
Tanzania kuwa mfano katika masuala ya Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda.
Balozi Gamaha alisema kuwa moja ya vigezo muhimu
katika kuvutia wawekezaji ni pamoja na nchi kuwa na amani na utulivu wa
kisiasa, kigezo ambacho Tanzania inacho na itaendelea kukilinda.
“Pamoja na Tanzania kujiandaa na Uchaguzi Mkuu
mwaka huu, bado naamini hakuna kitu kinaweza kuvuruga amani iliyopo. Hivyo kitu
muhimu ni kuendeleza ushirikiano wetu uliopo ambao ni wa kuheshimiana na
kufaidishana na si wa kinyonyaji”, alisema Balozi Gamaha.
Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Balozi
Songtian alisema kwamba China ina nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania
katika masuala ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda kwa kuzingatia ushirikiano
uliopo pia ni miongoni mwa nchi nzuri zaidi kwa uwekezaji hapa duniani.
Aidha, Balozi Songtian aliongeza kuwa China ipo
tayari kushirikiana na Tanzania katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali
zinazojitokeza katika sekta ya uwekezaji ikiwemo miundombinu, teknolojia na
elimu ya ufundi ili hatimaye iendelee kiviwanda.
“Lengo langu ni kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha
Tanzania na China zinafanikiwa katika Sekta ya Uwekezaji. Hivyo upo umuhimu
mkubwa wa kusomesha watu wengi zaidi katika masuala ya Teknolojia na kuwa na
Vyuo vingi zaidi vya Ufundi hapa Tanzania ili hatimaye tufanikiwe katika sekta
ya Viwanda”, alisisitiza Balozi Songtian.
Aidha, Balozi Songtian alisema kuwa upo mpango wa
Serikali ya China chini ya Mpango wa Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) wa
kuwaalika Wajasiriamali wachanga wapatao 500 kutoka Afrika kwenda nchini humo
kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali yatakayowasaidia kuendeleza shughuli
zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Eneo Maalum la
Uwekezaji (EPZA), Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ambaye aliwasilisha mada
kuhusu Maeneo Maalum ya Uwekezaji hapa nchini, alisema kuwa Tanzania ni nchi
ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji na tayari kuna maeneo Maalum ya Uchumi
yametengwa kwa kazi hiyo. Maeneo hayo ni pamoja na Bagamoyo, Dar es Salaam
(Eneo la Benjamin William Mkapa) na Mtwara.
Pia, alieleza kuwa ili sekta ya uwekezaji nchini
ikue na kufikia maendeleo ya viwanda ni muhimu kuimarisha rasimaliwatu,
miundombinu ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, nishati ya
umeme na sekta za kibenki.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika
zilizochaguliwa na China kwa ajili ya kuwa mfano wa uwekezaji na maendeleo ya
Viwanda. Nchi zingine ni Ethiopia na Kenya.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.