TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara
ya Waziri Mkuu wa India nchini Tanzania
Serikali ya India imeahidi
kuipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya kipaumbele ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu
ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020.
Hayo yameelezwa
leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mara baaada ya kufanya mazungumzo na mgeni
wake, Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi. Mhe. Modi aliwasili nchini jana
kwa ziara ya Kitaifa ya Siku mbili.
Rais Magufuli alieleza
kuwa Tanzania na India zina uhusiano mzuri wa kihistoria ambao umekuwa na faida
za kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili. Alitoa mfano namna India
ilivyofadhili ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 178.
Aidha, Rais
Magufuli aliishukuru Serikali ya India kwa kuridhia kutoa kiasi kingine cha
Dola za Marekani milioni 92 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kisiwani
Zanzibar. Rais Magufuli alielezea pia
kuridhishwa na kiwango cha biashara kati ya Tanzania na India ambacho kimekuwa
kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Alisema kwa mwaka 2009, Tanzania iliiuzia India
bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 187, kiwango hicho
kimeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.29 mwaka 2015.
Viongozi hao wakiwa katika
mazungumzo rasmi, walikubaliana kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo
za kilimo, viwanda, afya, nishati na madini.
Kwa upande wa Kilimo, Rais
Magufuli alitoa wito kwa wakulima wa Kitanzania kuongeza uzalishaji wa mazao ya
jamii ya kunde hususan dengu kwa kuwa yana soko kubwa nchini India. Alisema
India ni soko kubwa la mazao hayo na
imeahidi kusaidia pembejeo za kilimo ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.
Kwa upande wa viwanda,
mashirika ya viwanda vidogo ya India na Tanzania yamewekeana saini mkataba
ambapo mashirika hayo yatafanya tathmini nchi nzima ya kubaini rasilimali
zilizopo katika maeneo mbalimbali na aina ya viwanda vidogo vinavyoweza
kuanzishwa kwenye maeneo hayo. Baada
ya tathmini hiyo, Serikali ya India itatoa mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga
antamizi (incubators) za viwanda vidogo nchi nzima. Kupitia antamizi hizo,
wananchi watapatiwa mafunzo maalum ya uzalishaji wa bidhaa, biashara na usimamizi
wa fedha na baadaye kupewa mitaji kwa ajili ya kuanza shughuli za biashara.
Kwa upande wa sekta ya Afya,
Rais Magufuli alimuomba Waziri Mkuu wa India kushawishi wawekezaji kuja
kuwekeza nchini katika uzalishaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba. “Nimemuomba
Mhe. Modi na amekubali kuleta wawekezaji kuzalisha madawa na vifaa tiba hapa nchini.
Hiyo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matumizi ya fedha za kigeni kutokana
na uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli
ameshukuru Serikali ya India kwa kuipatia Hospitali ya Bugando mashine maalum
kwa ajili ya kupima ugonjwa saratani. Mashine hiyo inatarajiwa kuwasili nchini
wakati wowote kuanzia sasa.
Kuhusu sekta ya nishati na
madini, viongozi hao walikubaliana kushirikiana katika kuendeleza sekta hiyo
hapa nchini. Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia ikiwemo Helium
na madini. Hivyo ni vizuri tukishirikiana na wenzetu kuendeleza sekta hiyo.
Rais Magufuli alihitimisha
taarifa yake kwa kueleza kuwa wameazimia kushirikiana na India katika ngazi za
kitaifa, kikanda na kimataifa kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine,
mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanafanyika
ili liwe na uwiano mzuri wa uwakilishi. Aidha, wameahidi kusaidiana katika
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo ni tishio kubwa kwa
maendeleo endelevu ya dunia ya sasa.
Waziri Mkuu wa India
alikuwa katika ziara yake ya pili barani Afrika tangu kuchaguliwa kwake mwaka
2014 ambapo alitembelea nchi za Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na atahitimisha
ziara yake nchini Kenya.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
10 Julai 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.