Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mahiga katika hotuba yake aliliomba Bunge kupitisha kiasi cha shilingi150,845,419,000 ambapo katika kiasi hiki cha fedha shilingi142,845,419,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 8,000,000,000 imetengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
Bajeti hii ya mwaka 2017/2018 pamoja na mambo mengine imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu ya Wizara kama ifuatavyo;
- Kutangaza mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
- Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo;
- Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko;
- Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
- Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa;
- Kuendelea kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;
- Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo;
- Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu;
- Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu;
- Kuendelea kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama msaada;
- Kuendelea kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa;
- Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya Vikundi Kazi na Wataalam;
- Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika;
- Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki;
- Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia mfumo wa Confederation;
- Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki;
- Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
- Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi; na
- Kukamilisha kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje
Baadhi ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bungeni mjini Dodoma |
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akifurahia jambo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Peter Msigwa mara baada ya kuwasilisha hotuba ya bajeti Bungeni mjini Dodoma |
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima na Waziri Kivuli wa Wizara Mhe. Msigwa wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi na baadhi ya Wabunge. |
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima wakishirikishana jambo baada ya kuwasilisha hotuba ya Madirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma |
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akijibu hoja za wa Bunge Bungeni. |
Waziri Mhe.Dkt. Mahiga na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Wizara mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara Bungeni Mjini Dodoma
HOTUBA
YA MHESHIMIWA BALOZI DKT. AUGUSTINE PHILIP MAHIGA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA BAJETI YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA
MWAKA WA
FEDHA 2017/2018
Soma zaidi
Yaliyomo
|
AF
|
Adaptation Fund
|
AfDB
|
African Development Bank
|
AGOA
|
African Growth and Opportunity Act
|
APRM
|
African Peer Review Mechanism
|
BBC
|
British Broadcasting Corporation
|
CGTN
|
China Global Television Network
|
COMESA
|
Common Market for Eastern and Southern Africa
|
COP
|
Conference of Parties
|
DW
|
Deutsche Welle
|
EAC
|
East African Community
|
EPA
|
Economic Partnership Agreement
|
FAO
FIB
|
Food and Agriculture Organization
Force Intervention Brigade
|
GCF
|
Green Climate Fund
|
GEF
|
Global Environment Facility
|
GIZ
|
The Deutsche Gesellschaft für
Internationale Zusammenarbeit GmbH
|
GPEDC
|
Global Partnership for Effective Development
Cooperation
|
IAEA
|
International Atomic Energy Agency
|
IGAD
|
Intergovernmental Authority on Development
|
ILO
|
International Labour Organization
|
IMF
|
International Monetary Fund
|
IOM
|
International Organization for Migration
|
IORA
|
Indian Ocean Rim Association
|
KCB
|
Kenya Commercial Bank
|
KOICA
|
Korea International Cooperation Agency
|
LDCF
|
Least Developed Countries Fund
|
MINUSCA
|
United Nations Multidimensional Integrated
Stabilisation Mission in the Central African Republic
|
MK-ICC
|
Mt. Kilimanjaro International Convention Centre
|
MONUSCO
|
United Nations Organisation Stabilisation Mission in
the Democratic Republic of the Congo
|
NPT
|
Non – Proliferation Treaty
|
PSPF
|
Public Sector Pension Fund
|
RFI
|
Radio France International
|
RMB
|
Renminbi
|
SADC
SDGs
|
Southern African Development Community
Sustainable Development Goals
|
TAZARA
|
Tanzania-Zambia Railway Authority
|
TBC
|
Tanzania Broadcasting Corporation
|
TEHAMA
|
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
|
TMEA
|
Trademark East Africa
|
UKIMWI
|
Upungufu wa Kinga Mwilini
|
UNAMID
|
United Nations African Union Mission in Darfur
|
UNDP
UNDAP
|
United Nations Development Progamme
United Nations Development
Assistance Plan
|
UNEP
|
United Nations Environment Progamme
|
UNESCO
|
United Nations Educational Scientific and Cultural
Organization
|
UNFPA
|
United Nations Population Fund
|
UN-HABITAT
|
United Nations Human Settlement Programme
|
UNHCR
|
United Nations High Commission for Refugees
|
UNICEF
|
United Nations Children’s Emergency Fund
|
UN-ICTR
|
United Nations International Criminal Tribunal for
Rwanda
|
UNIDO
|
United Nations Industrial Development Organization
|
UNIFIL
|
United Nations Interim Force in Lebanon
|
UNISFA
|
United Nations Interim Security Force for Abyei
|
UNMISS
|
United Nations Mission in the Republic of South
Sudan
|
UNWTO
|
United Nations World Tourism Organization
|
UTT
|
Unit Trust of Tanzania
|
VoA
|
Voice of America
|
WHO
|
World Health Organization
|
WWF
|
World Wildlife Fund
|
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, baada ya Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuweka mezani Taarifa
ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara, naomba sasa kutoa hoja kwamba
Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango
na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa
mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha
Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa fadhila na
rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena katika Bunge lako
Tukufu kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu.
3.
Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia kuwashukuru na
kuwapongeza watoa hoja waliozungumza kabla yangu wakiongozwa na Mheshimiwa
Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na
Mheshimiwa Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango ambao kwa
hakika hotuba zao zimekuwa dira na msingi wa kuainisha masuala muhimu ya
Kitaifa na Kimataifa ambayo baadhi yake yanagusa majukumu ya Wizara yangu.
4.
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi wa Mhe. Balozi Adadi
Mohammed Rajab (Mb) na Makamu wake Mhe. Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis (Mb)
pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo. Miongozo na ushauri wao katika masuala
mbalimbali imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara
yangu.
5.
Mheshimiwa Spika, ninaposimama
mbele yenu kusoma hotuba hii nyuma yangu kuna kundi kubwa la watendaji na
watumishi wanaoniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa. Sina
budi kutoa shukrani zangu za dhati kwao kwa kuwa kwa kiasi kikubwa ndio
wamewezesha nisimame mbele yenu leo kuwasilisha hotuba hii. Kwa namna ya
kipekee kabisa, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Susan Alphonce Kolimba (Mb), Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Mhe. Balozi Dkt.
Aziz Ponary Mlima, Katibu Mkuu; Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu
Katibu Mkuu; Mabalozi; Wakurugenzi; na Wafanyakazi wengine wote kwa weledi,
umahiri na ufanisi wao katika kunisaidia kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa pongezi kwa Wabunge walioteuliwa na Mheshimiwa Rais
kulitumikia Taifa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, sina budi kutoa pongezi
maalum kwa Wabunge Wateule wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki. Ni
dhahiri kuwa kuchaguliwa kwao ni kielelezo cha kuaminiwa na Taifa letu. Ni
matarajio yetu kuwa watakuwa wazalendo, watatetea na kusimamia maslahi ya nchi
yetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kutunza misingi ya mshikamano
uliopo baina ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Dunia kwa
ujumla.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru
kwa dhati mke wangu mpendwa Mama Elizabeth Mahiga,
Watoto na familia yangu yote kwa ujumla kwa kunivumilia, kuniunga mkono na
kunipa utulivu wa kutosha kuniwezesha kutekeleza majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais katika
kujenga taifa na kutetea maslahi ya taifa letu nje na ndani ya nchi.
8.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, naungana na wabunge wenzangu kutoa salamu za pole
na rambirambi kwa familia za wabunge wenzetu wawili, Marehemu Hafidh Ally Tahir
na Marehemu Dkt. Elly Marko Macha waliotangulia mbele ya haki wakati
wakiendelea kulitumikia Taifa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, natumia fursa
hii kutoa salamu za pole na rambirambi kwa familia za wafanyakazi wenzangu
Wizarani, marehemu Hadija Mwichande na Marehemu Dkt. Cuthbert Leonard Ngalepeka
waliotutoka katika kipindi hiki. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu
awapumzishe mahala pema peponi. Amina.
9.
Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Mei,
2017 Taifa lilizizima kwa majonzi makubwa baada ya kupoteza watoto 32, walimu
wawili na dereva mmoja wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha kwa ajali mbaya ya
gari iliyotokea Wilayani Karatu. Kwa majonzi makubwa mno naomba nichukue fursa
hii kutoa salamu za pole kwa wazazi, walimu, Mkoa wa Arusha na Watanzania wote
kwa ujumla. Aidha, ninaomba nifikishe salamu za rambirambi kwa Bunge lako
Tukufu kutoka Balozi mbalimbali za nchi za Nje zilizopo hapa nchini na
mashirika mbalimbali ya kimataifa.
10. Mheshimiwa
Spika, kipekee
napenda kuwashukuru wasamaria wema Dkt. Steeve Mayor, Dkt. Jennifer Milby, Dkt.
Maanda Volker na Bw. Kelvin Negaard, raia wa Marekani kwa moyo wao wa upendo
waliouonesha kwa kuwahudumia marehemu na majeruhi wa ajali hiyo. Ninawashukuru
sana kwa msaada wao ambao haukuishia kwenye eneo la ajali bali pia walitafuta
usafiri wa kuwapeleka majeruhi nchini Marekani kwa matibabu zaidi kwa gharama
zao. Shukrani za dhati ziende pia kwa taasisi ya Bill Graham kwa kukubali kutoa
usafiri wa ndege kuwasafirisha majeruhi, wazazi, na wataalam wa afya wa
Tanzania hadi North Carolina na baadae kuchukuliwa na ndege maalum ya wagonjwa
wa dharura hadi Hospitali ya Mercy iliyopo Sioux City, Iowa, Marekani
wanapotibiwa hadi hivi sasa na hali zao zinaendelea vizuri. Hakika ukarimu na
upendo mkubwa waliouonesha kwa watoto hawa hautasahaulika katika mioyo ya
Watanzania.
11. Mheshimiwa
Spika
naishukuru pia Serikali ya Jamhuri ya Kenya kwa kututia moyo wakati wa tukio
hili la kuhuzunisha. Aidha, ninawashukuru watanzania wote waliojitolea kwa
namna moja ama nyingine katika mazishi na matibabu ya wahanga wa ajali hiyo. Tuendelee
kuwaombea majeruhi wapone haraka ili waweze kuendelea na masomo yao.
TATHMINI YA
HALI YA DUNIA
12. Mheshimiwa
Spika,
kabla sijatoa tathmini ya hali na mwelekeo wa siasa duniani na jinsi Tanzania
ilivyojipanga kushiriki, ningependa kulikumbusha Bunge lako Tukufu juu ya
misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje.
13. Mheshimiwa
Spika,
baada ya Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika kujikomboa kutokana na
ukoloni na ubaguzi wa rangi, Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania inaendelea
kujikita katika misingi ifuatayo;
1. Kulinda uhuru,
umoja na heshima ya nchi yetu;
2. Kuendeleza
ujirani mwema katika kanda yetu na kukuza umoja na ushirikiano barani Afrika;
3. Kuheshimu
kanuni ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine;
4. Kutofungamana
na upande wowote na kuchagua kwa hiari bila masharti marafiki katika Jumuiya ya
Kimataifa;
5. Kushirikiana
kikamilifu kimataifa na nchi, mashirika na taasisi mbalimbali katika nyanja za
diplomasia, siasa, uchumi, utaalam na teknolojia; na
6. Kukuza na
kutekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa viwanda katika Awamu hii ya
Tano.
14. Mheshimiwa
Spika,
katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kama ilivyoainishwa hapa, Serikali
ya Awamu ya Tano itazingatia mikakati na vipaumbele vifuatavyo:
1. Kuanzisha
mahusiano mapya ya kidiplomasia ambayo yataongeza tija kwa maslahi ya nchi
hususan maendeleo ya kiuchumi na teknolojia;
2. Kushiriki
kikamilifu katika kutafuta suluhu ya migogoro kwa njia ya amani kwa kuzungumza
moja kwa moja na wadau husika na kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya
kimataifa au kitaifa katika kutatua migogoro hiyo.
15. Mheshimiwa
Spika, kwa
kifupi Tanzania itaendelea na mkakati wake endelevu wa kutetea uhuru na haki
kimataifa huku ikizingatia vipaumbele vyake vya maendeleo na siasa yake ya
kutofungamana na upande wowote.
16. Mheshimiwa
Spika,
baada ya maelezo hayo ya kisera naomba kutoa tathmini ya hali ya dunia.
17. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/2017
dunia imeshuhudia ongezeko dogo katika kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika
mataifa ya magharibi yenye uchumi mkubwa hali inayochangia kuendelea kudorora
kwa biashara ya kimataifa. Aidha, Dunia imeendelea kushuhudia ongezeko la
machafuko ya kisiasa, migogoro ya kivita na vitendo vya kigaidi katika baadhi
ya mataifa. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wakimbizi na
wahamaji haramu. Kwa upande mwingine, mabadiliko ya tabianchi yamezidi kuleta
athari kubwa katika ikolojia na kutishia uhai wa viumbe na shughuli za
kibinadamu. Athari hii ni kubwa zaidi kwenye mataifa yanayoendelea kutokana na
uwezo mdogo wa mataifa hayo kukabiliana na changamoto hizo, hivyo kurudisha nyuma
juhudi za kujikwamua na umaskini. Matukio hayo ya kidunia yameibua hisia kuwa
ipo haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya jitihada mahsusi kukabiliana nayo ili
kuimarisha ustawi wa Dunia kwa ujumla. Baada ya kutoa tathmini hiyo ya
jumla, sasa naomba uniruhusu nitoe tathmini ya maeneo machache kama ifuatavyo:-
Hali ya Ulinzi na Usalama Duniani
(i)
Barani Afrika
18.
Mheshimiwa Spika,
hali ya Ulinzi na Usalama barani Afrika imeendelea
kuimarika kutokana na juhudi mbalimbali za usuluhishi na upatanishi
zinazoendelea kufanywa na Jumuiya ya Kimataifa. Ndani ya kipindi cha mwaka
mmoja dunia imeshuhudia kupungua kwa mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya
waasi, upinzani na magaidi katika nchi za Somalia, Afrika ya Kati na Nigeria.
Vilevile, hatua za upatanishi katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Lesotho na Sudan Kusini zinaelekea kuzaa matunda kutokana na
maendeleo mazuri ya majadiliano baina ya
pande zinazohasimiana. Kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Asasi
ya SADC ya Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama, Tanzania imepewa jukumu
la kusimamia utatuzi wa migogoro ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na Lesotho. Aidha, kupitia Chama Tawala cha CCM kwa kushirikiana na Chama cha
ANC cha Afrika Kusini, Tanzania imechangia katika kutafuta suluhu kwenye
mgogoro wa Sudan Kusini.
(ii)
Barani
Asia
19.
Mheshimiwa Spika,
hali ya usalama katika Rasi ya Korea imeendelea
kutetereka kutokana na vitendo vya pande mbili hasimu ambazo ni Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Korea kwa upande mmoja na Jamhuri ya Korea na Marekani
kwa upande mwingine. Hali ya kushutumiana kwa pande hizi inatokana na kila
upande kuhofia juu ya uwezekano wa uvamizi kutoka upande mwingine. Mpango wa
kutengeneza silaha za nyuklia pamoja na majaribio ya makombora ya masafa marefu
yanayofanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea kwa upande mmoja na
mazoezi ya kijeshi ya pamoja yanayofanywa na Jamhuri ya Korea na Marekani kwa upande mwingine, vimezidisha
hofu katika rasi hiyo na ukanda mzima. Endapo vita itatokea baina ya pande hizi
mbili italeta madhara makubwa si tu katika ukanda huo bali pia eneo lote la
Asia, Pasifiki na dunia kwa ujumla.
20.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mshirika
wa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia na kuhimiza matumizi salama ya
teknolojia hiyo. Hivyo, tutaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa
katika kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ili kuhakikisha hali ya
amani na usalama inaendelea kudumishwa duniani.
(iii) Barani Ulaya
21 Mheshimiwa
Spika, hali ya ulinzi na usalama katika eneo la Umoja wa Ulaya
imekumbwa na changamoto ya vitendo vyenye viashiria vya ugaidi pamoja na
wimbi kubwa la wakimbizi na wahamaji haramu.
Mashambulio ya kutumia milipuko ya mabomu katika miji ya London, Manchester, Paris, Brussels, Berlin na Stockholm yamezua
hofu na taharuki kubwa miongoni mwa wananchi wa nchi hizo. Mataifa hayo ya
Umoja wa Ulaya pia, yameendelea kushuhudia ongezeko kubwa la Wakimbizi kutokana
na migogoro ya kivita inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati hususan
nchi za Syria na Iraq.
Vilevile, idadi ya Wahamaji haramu wengi wao wakitokea mataifa ya Afrika
Magharibi na kuingia mataifa ya Umoja wa Ulaya nayo imeendelea kuongezeka. Hali
hiyo ya wasiwasi imesababisha kuibuka kwa vyama na vikundi vyenye siasa kali ya
ubaguzi katika Bara la Ulaya. Chaguzi za hivi karibuni huko Ufaransa na
Uholanzi zimefanikiwa kuleta ushirikiano kwa vyama vya wastani lakini tatizo
bado lipo.
(iv)
Amerika ya
Kusini na Kaskazini
22. Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama katika eneo la Amerika ya Kusini na Kaskazini
imeendelea kuwa shwari ikishuhudiwa kupungua kwa mapambano baina ya majeshi ya
Serikali na makundi yanayojihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika nchi
kama vile Mexico. Aidha, jitihada za upatanishi katika nchi ya Colombia zimechangia
kwa kiasi kikubwa kusitisha mapambano ya kivita kati ya Serikali ya nchi hiyo
na kundi la uasi lijulikanalo kama FARC.
Vilevile, katika nchi ya Venezuela, Serikali yenye mrengo wa kushoto
inakabiliwa na upinzani mkubwa na kusababisha hali nchini humo kuendelea kuwa
tete. Katika kunusuru hali hiyo, Papa Francis anajaribu kupatanisha.
Hali ya Uchumi Duniani
i).
Barani Afrika
23.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa zilizotolewa na Benki ya Dunia, uchumi wa Bara la Afrika kwa mwaka 2016
ulishuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2015. Sababu za kushuka kwa
ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuporomoka kwa bei ya mafuta katika mataifa
yanayozalisha na kuuza bidhaa hiyo kama vile Angola na Nigeria. Halikadhalika,
kushuka kwa bei ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika kwenye Soko la Dunia hususan
malighafi pia kumechangia kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Bara hili.
Hata hivyo, kwa mwaka 2017 uchumi wa Bara hili unatarajiwa kukua japo kwa kiasi
kidogo kutokana na kuimarika kwa bei ya mafuta na bei ya bidhaa katika soko la
Dunia.
ii). Barani Asia
24. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Bara
la Asia ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukikua kwa kasi kubwa kwa
wastani ukilinganishwa na ukuaji wa uchumi katika maeneo mengine duniani,
ulidorora kwa kiasi hasa kutokana na kupungua
kwa ukuaji wa uchumi wa nchi kama vile China uliosababishwa na kupungua
kwa mauzo ya bidhaa za nchi hiyo duniani. Hali hii, inafanya nchi kama China,
Japan, India na Korea Kusini kurekebisha kwa kiwango fulani cha misaada ya
uwekezaji na biashara na nchi zinazoendelea kama za Afrika.
iii).
Barani Ulaya
na Amerika
25.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Ulaya na Amerika uchumi umedorora hata hivyo kuna dalili za
kuanza kuimarika japo kwa kasi ndogo huku kukiwa na ongezeko kubwa la ukosefu
wa ajira kutokana na kupungua kwa biashara na uwekezaji pamoja na mzigo wa
madeni unaoendelea kuathiri uchumi wa baadhi ya nchi katika Umoja wa Ulaya. Kudorora
kwa uchumi wa nchi hizi kubwa kumeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi
katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
26. Mheshimiwa
Spika, katika medani za siasa, kumekuwa na chaguzi katika
nchi kadhaa kama vile Marekani, Ufaransa, Uholanzi na Austria ambapo katika
chaguzi zote hizo dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la wafuasi wa siasa zenye
mrengo wa kulia. Inatazamiwa
kuwa Serikali mpya zilizoingia madarakani na zinazofuata mrengo huo zitajikita
zaidi katika kuhamasisha maendeleo ya ndani na kupunguza kasi ya ukuaji wa
biashara na uchumi wa dunia kwa ujumla. Aidha, uamuzi wa kujitoa kwa Taifa la
Uingereza katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ni kielelezo cha siasa zenye mrengo
huo. Serikali mpya ya Marekani haijafafanua siasa yake ya uhusiano na Afrika.
Matamshi ya Rais wa Marekani kuhusu Afrika yamekuwa yakitofautiana na tawala
zilizopita. Hata hivyo, Serikali ya Marekani imeendeleza msaada kwa Tanzania
katika kupambana na maambukizi ya UKIMWI.
Mikakati ya kukabiliana na athari za
kuyumba kwa uchumi
27. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya kuyumba kwa hali ya uchumi duniani, Serikali
ya Awamu ya Tano imejipanga kutekeleza yafuatayo:-
a)
Kuendelea
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia ipasavyo matumizi ya
fedha za umma ili kuendelea kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;
b)
Kuendelea
kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo kwa kuzingatia Sera ya Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi ya
mwaka 2009 na Sheria ya Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi ya mwaka 2010.
Mkakati huu unasaidia kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha za kugharamia miradi ya
maendeleo;
c)
Kuendelea
kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuwekeza zaidi hapa nchini.
Jitihada hizi zinaenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara
nchini na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji;
d)
Kuendelea
kutafuta fursa za masoko ya bidhaa zetu, kukuza utalii wa ndani na
kushawishi watalii kutoka mataifa
mengine kutembelea nchi yetu ili kupanua wigo wa mapato na kupunguza athari
inayoweza kusababishwa na kuyumba kwa biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine;
na
e)
Kuendelea
kuhamasisha ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo itazalisha bidhaa na ajira kwa
wingi na kuongeza mapato yatokanayo na kodi.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA
MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
28.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kueleza utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha
2016/2017, naomba uniruhusu niainishe kwa ufupi majukumu ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-
i. Kubuni
na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje;
ii. Kusimamia
na Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali;
iii. Kusimamia
Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa;
iv. Kusimamia masuala yanayohusu
Kinga na Haki za wanadiplomasia waliopo nchini;
v. Kusimamia
na kuratibu masuala ya Itifaki na Uwakilishi;
vi. Kuanzisha
na Kusimamia Huduma za Kikonseli;
vii. Kuratibu
Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa;
viii. Kuratibu
na Kusimamia Masuala ya Watanzania Waishio Ughaibuni;
ix. Kuratibu
na Kusimamia Utekelezaji wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
x. Kuratibu na Kusimamia Miradi ya Maendeleo na Taasisi
zilizo chini ya Wizara; na
xi. Kusimamia
utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu.
29.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu hayo kwa mwaka 2016/2017, Wizara yangu
ilitengewa kiasi cha Shilingi 162,109,416,709.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 154,109,416,709.00 ni kwa
ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Katika fedha
zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, Shilingi
143,768,662,709.00 ni kwa ajili ya
Matumizi Mengineyo na Shilingi 10,340,754,000.00 ni kwa ajili ya
mishahara.
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017 Wizara ilitarajia kukusanya maduhuli kiasi cha Shilingi 24,001,150,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017, Wizara imefanikiwa kukusanya
kiasi cha Shilingi 19,773,333,502.00 sawa na asilimia 83 ya makusanyo yote ya maduhuli. Ni matarajio ya Wizara kuwa itafikia
malengo yake ya kukusanya maduhuli yaliyokadiriwa.
31.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017 Wizara
ilipokea jumla ya Shilingi
95,037,516,058.00 sawa na asilimia 59 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Kati
ya fedha hizo Shilingi 83,039,138,698.00 ni
kwa ajili ya bajeti ya Matumizi Mengineyo; Shilingi
8,509,062,360.00 ni kwa ajili
ya mishahara; na Shilingi 3,489,315,000.00
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
32.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa licha ya changamoto
mbalimbali za kibajeti. Katika kipindi hiki, Wizara imeendelea kuzingatia
sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya fedha za umma katika kudhibiti matumizi
na mapato ambapo kwa kudhihirisha hilo, Wizara pamoja na Balozi zote isipokuwa
Ubalozi mmoja zimepata Hati Safi ya
Ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2015/16. Nachukua fursa hii kuwashukuru Watendaji wa
Wizara na kuwahimiza waendelee kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo
mbalimbali ya matumizi ya fedha za umma wakati wote wanapotekeleza majukumu
yao.
33.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi jinsi Wizara
ilivyotekeleza majukumu yake katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017:-
KUBUNI NA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA SERA YA NCHI YA
MAMBO YA NJE
34.
Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje, Wizara yangu
kwa kushirikiana na Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na Sekta
binafsi iliratibu na kufanikisha ziara za viongozi wanaokuja nchini, mikutano
ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano, masuala ya ushirikiano kati ya
Tanzania na nchi rafiki, mikutano ya Bara la Afrika na nchi nyingine pamoja na
makongamano ya biashara yaliyofanyika ndani na nje ya nchi kama ifuatavyo:
India
35.
Mheshimiwa Spika,
Wizara
iliratibu ziara ya kitaifa ya Mhe. Nerendra Modi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
India iliyofanyika nchini mwezi Julai 2016. Pamoja na mambo mengine, Serikali
za Tanzania na India zilisaini Mkataba wa Mkopo wa Dola za Marekani milioni 92
kwa ajili ya mradi wa maji wa Zanzibar ambao umeanza kutekelezwa. Aidha,
utekelezaji wa makubaliano ya kuondoa hitajio la viza kwa raia wa India na
Tanzania wenye Pasi za Kidiplomasia na Pasi za Huduma umeanza tangu mwezi
Desemba 2016.
36.
Mheshimiwa Spika,
vilevile, Serikali ya India iliahidi kutoa mkopo
wenye riba nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza
mradi wa kusambaza maji katika miji 17 ya Kasulu, Ludewa, Manyoni, Mugumu,
Chunya, Sikonge, Makonde, Handeni, Makambako, Wanging’ombe, Kayanga, Songea,
Zanzibar, Geita, Kilwa Masoko na Njombe. Mnamo mwezi Machi 2017, Serikali hiyo
iliwasilisha rasmi uamuzi wake wa kutoa mkopo huo ambao utatolewa na Benki ya
Exim ya India kwa riba ya asilimia 1.5 na utalipwa kwa kipindi cha miaka 25.
Tayari benki hiyo imewasilisha nyaraka za masharti ya mkopo huo na Serikali
inaendelea na taratibu za uchambuzi.
China
37.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki
wa Tanzania katika Mkutano wa Waratibu wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China
na Afrika uliofanyika Beijing, China mwezi Julai 2016. Lengo la mkutano huo
lilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa Mpango Kazi uliopitishwa na Mkutano wa
Wakuu wa Nchi za China na Afrika uliofanyika Johannesburg, Afrika
Kusini mwezi Desemba 2015. Miradi inayopewa kipaumbele katika mpango kazi huo
inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege,
barabara, maji, mawasiliano, maeneo ya viwanda pamoja na vyuo vya ufundi.
Katika kufanikisha azma hiyo, China imeelekeza majimbo yake tajiri kuhamishia viwanda vyake barani
Afrika katika nchi zilizochaguliwa. Kwa upande wa Tanzania, jimbo la Jiangsu limeshaanza uwekezaji kwenye
viwanda vya nguo vilivyopo Dar es Salaam na Shinyanga na kutoa ajira kwa
Watanzania zaidi ya 1,630. Aidha, kampuni ya Tianhe Shiye kutoka jimbo hilo inatarajia kufanya uwekezaji katika
ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda utakaogharimu Dola za Marekani bilioni
mbili.
38. Mheshimiwa Spika, kupitia ushawishi wetu wa
kidiplomasia, China iliichagua Tanzania kuwa nchi ya kuzindulia mpango wake wa
Diplomasia ya Umma kati yake na Bara la Afrika. Wizara iliratibu uzinduzi wa
Kongamano la kwanza chini ya mpango huo, lililofanyika Jijini Dar es Salaam
mwezi Agosti 2016. Manufaa yaliyopatikana katika kongamano hilo ni
pamoja na kukuza mahusiano
na mawasiliano kati ya China na Tanzania kuanzia ngazi za Viongozi wa Serikali,
wataalam, wafanyabiashara, wawekezaji, wanamichezo na baina ya watu na watu.
Aidha, wasemaji wa Serikali na Taasisi zake walijengewa uwezo wa kutoa habari
za nchi kwa wakati bila kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kusimamia
vyombo vya habari kutopotosha umma kwa kutoa taarifa zinazopinga maendeleo ya
nchi au kupotosha utendaji wa Serikali.
39. Mheshimiwa
Spika, Mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja
ya Ushirikiano katika masuala ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na
China ulifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi
Oktoba 2016. Mafanikio ya
mkutano huo ni kuimarika kwa mahusiano kati ya nchi hizi mbili katika sekta za
biashara, uchumi na ufundi ambapo Serikali ya China ilikubali kuipa Serikali ya
Tanzania msaada wa kiasi cha RMB Yuan milioni 300 sawa na Shilingi bilioni 97. Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo itakayokubaliwa na pande zote mbili ikiwemo mradi wa vifaa vya
ukaguzi na usalama kwa ajili ya viwanja vya ndege.
40. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya
kikazi ya Mhe. Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China
nchini Tanzania iliyofanyika mwezi Januari 2017. Kufuatia ziara hiyo, Serikali
zote mbili zilikubaliana kuimarisha na kukuza uhusiano wa kiuchumi, kibiashara,
kiutamaduni na kijeshi pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo katika masuala
ya kimataifa kwa manufaa ya nchi zote mbili. Aidha, Wizara imesaini Mkataba wa
msaada wa fedha za China Yuan 2,000,000, sawa na Shilingi milioni 633 kwa ajili
ya ujenzi wa makazi ya wageni mashuhuri Chamwino, Dodoma. Kukamilika kwa ujenzi
wa makazi hayo kutatoa fursa kwa Wageni hao mashuhuri kupata mahali pa kufikia
panapoendana na hadhi ya nyadhifa zao. Aidha, kutokana na hatua ya Serikali
kuhamishia makao yake Dodoma, ujenzi huo utapunguza gharama ya malazi ya
viongozi kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja nchini kwa ziara rasmi au za
kikazi.
Kuwait
41.
Mheshimiwa Spika,
uhusiano kati ya nchi yetu na Kuwait unazidi kuwa mzuri.
Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara iliratibu na kufanikisha
ziara ya ujumbe wa Wataalam wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait uliokuja nchini
mwezi Desemba 2016, kwa lengo la kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa kwa
ufadhili wa Mfuko huo pamoja na kupokea maombi ya miradi mipya iliyowasilishwa
na Serikali ya Tanzania. Miradi mipya iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa
barabara ya Chaya-Nyahua, mkoani Tabora na mradi wa ukarabati wa Hospitali ya
Mnazi Mmoja, Zanzibar.
42. Mheshimiwa Spika, kufuatia
ziara hiyo pamoja na majadiliano ya wataalam, Bodi ya Mfuko wa Kuwait kwenye
kikao chake cha mwezi Februari 2017, imeidhinisha fedha za Kuwait kiasi cha Dinar 15,000,000 sawa na Shilingi
bilioni 110 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Barabara ya Chaya-Nyahua yenye
urefu wa kilometa 85.4. Mkataba wa mkopo huo ulisainiwa mwezi Machi 2017,
Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Dkt. Philip Isidory Mpango (Mb), Waziri wa
Fedha na Mipango alisaini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
43. Mheshimiwa Spika, vilevile,
Ubalozi wa Kuwait kwa kushirikiana na Wizara yangu umeanzisha kampeni
ijulikanayo kama “Maabara kwa Shule za Sekondari na Kisima kwa shule za
Msingi”. Miradi hii inalenga kusaidia kuwepo kwa maabara kwa shule za Sekondari
na Kisima kwa shule za msingi ambapo Ubalozi huo kupitia Taasisi mbalimbali
zisizo za Kiserikali za nchini Kuwait zitakuwa zinafadhili miradi hiyo. Hadi
sasa shule 27 zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga zimenufaika na
programu hiyo ambayo ni endelevu.
Umoja wa
Falme za Kiarabu
44.
Mheshimiwa Spika,
Wizara
imeendelea kushawishi wadau mbalimbali wa maendeleo hususan nchi marafiki
kuchangia utoaji wa huduma za kijamii. Kufuatia mazungumzo ya Wizara yangu na
Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za
Kiarabu mwezi Desemba 2016, Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia
Programu ijulikanayo kama Zayed Giving
Initiative imetoa Zahanati mbili zinazotembea ambazo zitatoa huduma bure ya
kupima na kutibu magonjwa yasiyoambukiza katika mikoa yote nchini kwa kipindi
cha mwaka mmoja. Zahanati hizo zilitoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam
mwezi Februari na Machi 2017 na sasa zipo Zanzibar tangu mwezi Aprili 2017
kabla ya kwenda mikoa mingine.
45.
Mheshimiwa Spika,
Vilevile,
Wizara iliratibu ziara ya Ujumbe Maalum wa Kiuchumi wa Mrithi wa Mfalme wa Abu
Dhabi ambaye ni Kaimu Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyofanyika mwezi
Oktoba 2016. Pamoja na mambo mengine, Ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana na
kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa Serikali.
46.
Mheshimiwa Spika, wakati wa
ziara hiyo, Tanzania iliwasilisha miradi mikubwa ya sekta ya Miundombinu ya barabara,
bandari, reli na viwanja vya ndege inayohitaji ufadhili kutoka Mfuko wa
Maendeleo wa Abu Dhabi ambao upo chini ya Mrithi huyo wa Mfalme. Mfuko huo
tayari umeidhinisha kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni
20 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi hadi Uvinza mkoani Kigoma
yenye urefu wa kilometa 51. Aidha, Mheshimiwa Rais amemualika Mrithi wa Mfalme
wa Abu Dhabi kufanya ziara rasmi nchini mwaka huu ikiwa ni njia mojawapo ya
kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili.
47.
Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu uliofanyika Abu
Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Desemba 2016. Katika mkutano huo,
masuala yaliyojadiliwa na kuwekewa maazimio ni pamoja na kuboresha uwekezaji na
biashara, nishati, ulinzi na usalama, usafiri wa anga, kuendeleza miundombinu,
elimu (kupatiwa nafasi za mafunzo) pamoja na kilimo na mazingira. Wakati wa
Mkutano huo,Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini mikataba miwili ya
Ushirikiano katika Sekta ya Anga; na Ushirikiano katika Sekta ya Utalii.
48.
Mheshimiwa Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Umoja wa
Falme za Kiarabu ni moja kati ya nchi muhimu za kimkakati katika biashara. Ili
kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili,
Wizara yangu inaendelea kuratibu majadiliano ya Mkataba wa Kutotoza Kodi mara
Mbili na Kukwepa kulipa Kodi (Avoidance
of Double Taxation and Tax Avoidance Agreement) na Mkataba wa Kuendeleza na
Kulinda Uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Agreement
on Promotion and Protection of Investments).
49.
Mheshimiwa Spika,
katika jitihada za kuimarisha biashara baina ya Tanzania
na Umoja wa Falme za Kiarabu, Tanzania imealikwa kushiriki kwenye maonesho
makubwa ya kibiashara yatakayofanyika Dubai mwaka 2020 (Dubai Expo 2020).
Naomba kutumia fursa hii, kuwashauri wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa
hiyo kwa kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo.
Qatar
50. Mheshimiwa Spika, uhusiano kati ya Tanzania na Qatar umeendelea kuwa mzuri. Kupitia uhusiano
huo, Wizara
imefanikiwa kupata msaada wa magari 10 ya wagonjwa kutoka Ubalozi wa Qatar
uliopo nchini. Magari hayo yalikabidhiwa
kwa Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto mwezi Desemba 2016. Magari hayo yamekuwa ya msaada mkubwa katika
kutoa huduma za afya.
51. Mheshimiwa Spika, Qatar ni miongoni mwa nchi zenye uzoefu mkubwa katika sekta ya gesi na
mafuta. Kwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi na mafuta, tumeona ni vyema
tukafungua ubalozi Doha ili kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya nchi hizi
hususan diplomasia yetu ya uchumi.
Iran
52.
Mheshimiwa Spika,
mwezi Septemba 2016, Wizara iliratibu ziara ya
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia
masuala ya Afrika. Kufuatia ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, Serikali ya
Iran ilikabidhi msaada
wa vifaa kwa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkokotoni, Zanzibar wenye thamani ya
Dola za Marekani 500,000. Aidha, Serikali ya Iran ilitoa ahadi ya kujenga
vyuo vya ufundi stadi vingine zaidi Unguja na Pemba pamoja na kutoa fursa za
Mafunzo kwa Watanzania katika sekta za Nishati ya Mafuta na Gesi.
53.
Mheshimiwa Spika,
pia napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Iran
imeonesha utayari wa kuifutia nchi yetu madeni yaliyolimbikizwa tangu miaka ya
1970 na kuwekeza hapa nchini katika viwanda vikubwa na vidogo.
Israel
54. Mheshimiwa Spika, uhusiano kati
ya Tanzania na Israel umeendelea kuimarika. Kufuatia kuimarika kwa uhusiano
huo, Serikali ya Israel imeahidi kutoa msaada wa
kujenga chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo
Dodoma ambacho ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
55. Mheshimiwa Spika, kupitia mradi wa Save the Child
Heart unaotekelezwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali
ya Israel imejitolea kufadhili mafunzo ya tiba ya moyo kwa madaktari wa Taasisi
hiyo ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi.
Hivi sasa, Taasisi hiyo inatoa huduma kwa Watanzania na vilevile inapokea
wagonjwa kutoka nchi za nje zilizo jirani. Kadhalika, Serikali ya Israel imetoa
msaada wa mchoro wa kituo cha maafa kinachotegemewa kujengwa eneo la Msalato
hapa Dodoma. Wataalam kutoka Israel wanategemewa kuja nchini mnamo mwezi Juni
2017 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakaowezesha
kuchora mchoro huo. Kujengwa kwa kituo hicho kinachotarajiwa kuwa na kiwango
cha kimataifa kitaongeza uwezo wa Dodoma kukabiliana na maafa ikizingatiwa kuwa
Dodoma inatarajia kupokea wageni wengi kutokana na azma ya Serikali kuhamia
Dodoma.
56.
Mheshimiwa Spika,
kwa mara ya kwanza tangu Taifa letu lipate uhuru,
Tanzania inafungua ubalozi Tel Aviv mwaka huu. Kwa kufungua Ubalozi huo,
Tanzania itanufaika kwa kushirikiana na Israel katika kupata utaalam wa kilimo
cha umwagiliaji, TEHAMA, ulinzi na utalii.
57. Mheshimiwa Spika, Tanzania itaendelea kushiriki katika mijadala ya kimataifa kuhusu suala la
haki za Wapalestina.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
58.
Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa
Joseph Kabange Kabila, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alifanya ziara ya
Kitaifa nchini mwezi Oktoba 2016. Kufuatia ziara hiyo, nchi hizi mbili
zilisaini Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi ambayo
yatawezesha kushirikiana katika kufanya utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa
Tanganyika. Aidha, makubaliano yamefikiwa juu ya wafanyabiashara wa nchi hiyo
kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yao. Hatua hii
itaongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa
kiwango cha mizigo.
Morocco
59.
Mheshimiwa Spika,
mwezi Oktoba 2016,
Mfalme Mohamed VI wa Morocco alifanya ziara ya Kitaifa nchini. Morocco ni nchi ya tano barani Afrika yenye
uchumi mkubwa. Hivyo, katika kutekeleza diplomasia yetu ya uchumi, hatuna budi
kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi hiyo.
60.
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako Tukufu litakumbuka kuwa, wakati wa ziara ya
Mfalme wa Morocco, wafanyabiashara wapatao elfu moja waliambatana na kiongozi
huyo hatua ambayo ilitoa fursa kwa wafanyabiashara wetu hapa nchini kukutana na
wafanyabiashara hao kwa lengo la kuanzisha mahusiano ya kibiashara. Kutokana na ziara hiyo, nchi hizi mbili
zilisaini jumla ya Mikataba 23 ya Ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, usafiri
wa anga, nishati, utalii, viwanda, fedha na bima. Pia, wakati wa
ziara hiyo, Mfalme wa Morocco alitoa ahadi ya kujenga uwanja mkubwa wa kisasa
wa mpira wa miguu hapa mjini Dodoma. Hadi hivi sasa eneo utakapojengwa uwanja
huo limeshapatikana na timu ya wataalam kutoka nchini Morocco imeshafika kwa
ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa uwanja huo.
Zambia
61. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Kitaifa ya Mheshimiwa
Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambia iliyofanyika hapa nchini mwezi
Novemba 2016. Wakati wa ziara hiyo, nchi hizi zilikubaliana kuimarisha
mahusiano ya kidiplomasia na uchumi hususan kuongeza ufanisi wa utendaji wa
Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia na bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda
Zambia. Kufuatia ziara hiyo, Wakuu wa Nchi hizi mbili waliagiza sheria
inayounda Mamlaka ya TAZARA ifanyiwe mapitio na pande zote kwa ajili ya
kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo. Kufuatia agizo hilo, ujumbe wa Tanzania
ukiongozwa na Mheshimiwa George Mcheche Masatu, Mwansheria Mkuu wa Serikali ulifanya
ziara nchini Zambia na kufanya mazungumzo na wenzao nchini humo. Katika
muendelezo wa mazungumzo hayo, mnamo Mwezi Februari 2017 ujumbe wa Zambia
ulifanya ziara nchini kama sehemu ya kuendeleza majadiliano ya namna ya
kuboresha Sheria ya Mamlaka ya TAZARA na hivi sasa majadiliano bado yanaendelea
kwa kuwahusisha wadau wengine. Aidha, Mheshimiwa Lungu alipata fursa ya
kujionea maboresho yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo
kuahidi kushawishi wafanyabiashara nchini mwake kuendelea kutumia Bandari hiyo.
Kenya
62. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya
Tanzania na Kenya uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016. Katika
mkutano huo, masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa,
usalama na biashara yalijadiliwa. Mkutano huo ulizidi kuimarisha mahusiano
yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya.
Malawi
63.
Mheshimiwa Spika, Mkutano
wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi
ulifanyika Lilongwe, Malawi mwezi Februari 2017. Katika mkutano huo masuala
mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa, usalama,
usafirishaji, nishati, uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe na biashara
yalijadiliwa na makubaliano kufikiwa. Tanzania na Malawi zilifanikiwa kutia
saini mikataba miwili ya Huduma za Anga na Mashauriano ya Kidiplomasia. Mkutano
huu ulizidi kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Malawi. Aidha,
napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba, mazungumzo ya kutafuta suluhu
ya mgogoro wa mpaka katika ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi chini ya
usuluhishi wa Mhe. Joaquim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji na Mwenyekiti wa
Jukwaa la Viongozi na Wakuu wa Nchi Wastaafu wa Umoja wa Afrika, akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu
wa Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini yanatarajiwa
kuanza tena wakati wowote hivi karibuni. Wizara inasubiri kupata tarehe rasmi
ya kuanza kwa mazungumzo hayo kutoka Ofisi ya Rais Mstaafu Mhe. Chissano.
Uganda
64. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri
ya Uganda alifanya ziara ya Kitaifa nchini mwezi Februari 2017. Kufuatia ziara
hiyo, nchi hizi mbili zilitia saini hati ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia
na kisiasa. Halikadhalika, zilikubaliana kuimarisha mahusiano katika sekta ya
biashara na uwekezaji; uchukuzi; mafuta na nishati. Viongozi wa nchi hizi mbili
waliagiza kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano
ifikapo mwezi Aprili 2017.
65.
Mheshimiwa Spika, Mkutano
wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda
ulifanyika Jijini Arusha mwezi Aprili 2017. Katika mkutano huo, masuala
mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa, usalama,
usafirishaji, nishati na biashara yalijadiliwa na makubaliano kufikiwa. Aidha,
Mkataba wa Ubia wa Mradi wa Umeme wa Murongo - Kikagati ulisainiwa na Mawaziri
wa Nishati wa pande zote mbili kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa mitambo ya
kufua umeme. Vilevile, Tanzania na Uganda zilitia saini Mkataba wa Ushirikiano
katika Sekta ya Anga.
Ethiopia
66. Mheshishimiwa Spika, ziara ya
kitaifa ya Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn, Waziri Mkuu wa
Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia ilifanyika nchini mwezi Machi
2017. Ziara hiyo imeimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi zetu mbili
katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi na kijamii. Tanzania na Ethiopia
zilikubaliana kushirikiana katika maeneo 15 ambayo
ni kufungua
kituo kikubwa cha kuhifadhi mizigo cha bandari kavu; Ushirikiano katika Sekta ya Anga; Ushirikiano wa
Kijeshi; Matumizi ya maji ya Mto
Nile; Ushirikano katika Sekta ya
Nishati; na Ushirikiano katika Sekta ya Mifugo
na bidhaa za Ngozi. Maeneo mengine ni Kuondolewa kwa hitajio la Visa Rejea kwa raia wa Ethiopia;
Ethiopia kufungua Ubalozi wake Tanzania;
Ushirikiano katika sekta ya madini; Kuendeleza lugha ya Kiswahili; Ushirikiano katika Sekta ya Utalii; Ushirikiano katika Sekta ya Michezo; Ushirikiano kwenye Sekta ya Fedha;
na Ushirikiano katika Sekta ya Mawasiliano.
67. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu itashirikiana na Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali pamoja na
sekta binafsi katika kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Afrika Kusini
68. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa
Zuma, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini alifanya Ziara ya Kitaifa nchini mwezi
Mei 2017. Ziara hiyo imetoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali
yanayohusu nchi hizi mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa. Katika
ziara hiyo, Mheshimiwa Zuma aliambatana na ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya
80 hatua ambayo ilitoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kubadilishana nao
uzoefu. Kwa kipindi kirefu, Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana
katika sekta za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kupitia ziara hiyo, mikataba ya
makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu,
sayansi, teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo ilisainiwa.
Cuba
69. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2016, Mheshimiwa
Salvador Antonio Valdés Mesa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba alifanya ziara
nchini. Mheshimiwa Mesa akiwa nchini alifanya mazungumzo na Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
na viongozi wengine wa Serikali. Kufuatia mazungumzo hayo, Serikali ya Cuba iliahidi
kuendelea kuleta madaktari wa binadamu hapa nchini ili kuwajengea uwezo
wataalam wetu wa Sekta ya Afya. Kwa sasa
kuna madaktari 24 kutoka Cuba ambao wanatoa huduma za kitabibu na mafunzo
katika hospitali na vyuo vya afya vilivyopo nchini. Madaktari hao wamesambazwa
Zanzibar na katika Mikoa ya Dar es Salaam, Ruvuma, Pwani na Mbeya.
Czech
70.
Mheshimiwa Spika,
Wizara
iliratibu ziara ya Mhe. Ivan Jancarek, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri
ya Czech hapa nchini mwezi Septemba 2016. Wakati wa ziara hiyo Tanzania na
Czech zilikubaliana kuimarisha ushirikiano uliopo na kuongeza maeneo mapya ya
ushirikiano, katika sekta za elimu, biashara na uwekezaji. Aidha, Serikali ya
Czech iliahidi kufadhili wanafunzi wa Kitanzania kusoma katika vyuo vikuu vya
nchi hiyo na kujenga kiwanda cha kuzalisha viuatilifu vya wadudu wanaoshambulia
mazao ya mihogo na migomba. Vilevile, Serikali hiyo iliahidi kujenga kiwanda
cha kutengeneza viatu na samani ambacho kitaendeshwa kwa ubia kati yake na
Jeshi la Magereza.
Finland
71. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Mhe.
Kai Mykkänen, Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Jamhuri ya
Finland iliyofanyika nchini mwezi Novemba 2016. Pamoja na mambo mengine, Mhe.
Mykkänen alishiriki katika uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya
Umeme jijini Dar es salaam. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Finland kwa gharama ya Shilingi bilioni
74.6. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 63.56 zimetolewa na Serikali ya
Finland na Shilingi bilioni 11.03 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Uswisi
72.
Mheshimiwa Spika,
Wizara
iliratibu ziara ya Balozi Manuel Sager, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la
Uswisi iliyofanyika mwezi Februari, 2017. Balozi huyo, alitembelea hospitali ya
Rufaa ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara na kuzindua Jengo la Wagonjwa wa Nje
ambalo limejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi. Ujenzi wa jengo hilo
unatarajiwa kuongeza ubora wa huduma za afya na kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.
Canada
73. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha uliopita,
majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Canada kuhusu
uhuishwaji wa msaada wa Serikali ya Canada katika Mfuko wa Afya yalikamilika.
Serikali ya Canada iliridhia kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia Mfuko huo
ambapo itachangia kiasi cha Dola za Canada milioni 87.3 sawa na Shilingi
bilioni 141.9 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2020.
Hadi kufikia mwezi Aprili 2017, Serikali hiyo ilikuwa imetoa kiasi cha Dola za
Canada milioni 19, sawa na Shilingi bilioni 30.9 kuchangia mfuko huo.
Uturuki
74. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Racep Tayyip Erdogan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki alifanya ziara
ya kitaifa nchini mwezi Januari 2017. Kufuatia ziara hiyo, masuala mbalimbali
yalijadiliwa kati ya Tanzania na Uturuki. Miongoni mwa masuala hayo ni mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa uliozinduliwa
na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwezi Aprili 2017. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu
itahusisha ujenzi wa kipande cha reli kuanzia Dar-es-Salaam hadi Morogoro kwa
kutumia fedha za ndani. Mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Kampuni ya YAPI
Merkez ya Uturuki na MOTA-ENGEL AFRIKA ya Ureno. Kwa kutambua kuwa gharama za
kutekeleza mradi huo ni kubwa, Wizara inaendelea kuratibu upatikanaji wa fedha
kutoka kwenye mashirika ya kimataifa, taasisi za fedha na nchi rafiki kwa ajili
ya kufanikisha utekelezaji wa awamu nyingine za mradi huo. Awamu hizo
zitajumuisha kipande cha kutoka Morogoro kwenda Dodoma na baadae Mwanza na
Kigoma na hatimaye kuunganisha na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kukamilika kwa mradi huu kutakuza biashara,
uwekezaji, ajira na kuongeza pato la taifa.
Japan
75.
Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Ushirikiano
kati ya Tanzania na Japan uliofanyika Jijini Dar es salaam mwezi Agosti 2016.
Lengo la mkutano huo lilikuwa kupitisha miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya
Japan katika mwaka 2016 hadi 2017. Jumla ya miradi 18 kutoka sekta za nishati,
ujenzi wa barabara na maboresho ya bandari iliwasilishwa kwa Serikali ya Japan
ili kuombewa ufadhili. Hadi kufikia mwezi Mei 2017, jumla ya miradi mitano (5)
ilikuwa imekubaliwa wakati miradi 13 majadiliano bado yanaendelea. Miradi
iliyokubaliwa ni: Mradi wa kuimarisha uwezo katika upangaji na utekelezaji wa
programu ya kuendeleza kilimo wilayani; Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu
uendelezaji wa sekta ya viwanda; Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu
uendelezaji wa kongani za viwanda; Mradi wa usimamizi wa rasilimali ya maji
yaliyo chini ya ardhi Zanzibar; na Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu maji
kwa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar.
76.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Sita wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika uliofanyika kwa mara ya kwanza
barani Afrika nchini Kenya mwezi Agosti 2016. Nchi 48 za Afrika zilishiriki
katika Mkutano huo. Matokeo ya mkutano huo ni pamoja na azma ya Serikali ya
Japan:
i.
Kutoa
kiasi cha Dola za Marekani bilioni 30 kwa Bara la Afrika ambazo zitatolewa kwa
njia ya misaada, mikopo na uwekezaji katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Kati
ya kiasi kilichoahidiwa, Dola za Marekani bilioni 10 zitatolewa kwa ajili ya
ujenzi wa miundombinu kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika. Miundombinu hii ni
pamoja na barabara, umeme na mipango miji;
ii.
Kutoa
mafunzo kwa vijana takribani 30,000 katika fani mbalimbali kama vile uendeshaji
na usimamizi wa viwanda, ufundi, shughuli za kiuchumi na elimu ya biashara;
iii.
Kutoa
walimu wa kujitolea wapatao 20,000 kwa ajili ya kufundisha masomo ya hisabati
na sayansi ili kuwajengea uwezo wanafunzi katika masomo hayo;
iv.
Kuongeza
Dola za Marekani bilioni 2 kwenye Mfuko wa Kukuza Biashara na Uwekezaji; na
v.
Kuanzisha
Japan - Africa Public-Private Economic
Forum ili kukuza majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kati ya
Afrika na Japan.
Jamhuri ya Korea
77.
Mheshimiwa Spika, mwezi Julai 2016 Wizara iliratibu mkutano kati ya Ujumbe kutoka Jamhuri
ya Korea ulioongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Exim ya Korea na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Serikali ya Jamhuri ya
Korea iliahidi kuipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 300 kwa
ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi
2020. Aidha, nchi hiyo iliichagua Tanzania kuwa moja ya nchi za kipaumbele
katika ushirikiano wake na nchi za Afrika.Vilevile, kutokana na mahusiano mazuri
yaliyopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea,
Wizara iliratibu programu maalum ya upatikanaji wa walimu wa kujitolea wa
masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka nchi hiyo kwa ajili ya kuja kufundisha nchini. Mwezi Agosti 2016 Wizara iliwapokea
walimu 10 ambao wamepangwa kufundisha katika shule za Sekondari za Zanaki,
Benjamin William Mkapa na Jangwani zilizopo Dar es Salaam.
78.
Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti 2016
Wizara iliratibu ziara ya Wabunge kutoka Jamhuri ya Korea waliofika nchini kwa
ajili ya kufanya mazungumzo na Dkt. Tulia Ackson (Mb), Naibu Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Madhumuni ya ziara hii yalikuwa ni kukuza na
kuendeleza ushirikiano kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Bunge la Jamhuri ya Korea.
79. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, kama sehemu ya maadhimisho ya
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia, Serikali ya Jamhuri ya
Korea imeifahamisha Wizara yangu kuwa inawasiliana na Bunge la nchi yao ili kuikaribisha
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kutembelea Bunge
la nchi hiyo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
80.
Mheshimiwa Spika, halikadhalika mwezi Septemba 2016, Wizara iliratibu ziara ya ujumbe kutoka Taasisi ya
Ushirikiano katika masuala ya Kilimo kati ya Jamhuri ya Korea na Afrika
iliyoanzishwa mwaka 2010. Taasisi hiyo inajishughulisha na utafiti wa mazao ya
kilimo na dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mazao. Tafiti za Taasisi hiyo
hufanyika kwa kushirikiana na maafisa ugani wa nchi husika kwenye mazao
mbalimbali kama vile mpunga, mihogo, nyanya na mengineyo. Nchi wanachama hupata
fursa za kupata mafunzo, kubadilishana uzoefu na utafiti kupitia mikutano na
makongamano mbalimbali yanayoandaliwa kila mwaka na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza
uzalishaji katika sekta ya kilimo.
81.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa miradi inayotekelezwa na taasisi hiyo ni Africa Rice ambao ni mradi mkubwa wa
utafiti katika zao la mpunga wenye lengo la kukuza teknolojia katika uzalishaji
wa zao hilo ili kupunguza umaskini na kuhakikisha usalama wa chakula. Kutokana
na ziara hiyo Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeanza hatua
za awali za kujiunga na Taasisi hiyo ili kupata utaalam zaidi utakaowezesha
kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.
82.
Mheshimiwa Spika, vilevile,Wizara iliratibu ziara ya wajumbe kutoka Jamhuri ya Korea kwa ajili ya
kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa Maji Taka katika Jiji la Dar es Salaam
mwezi Septemba 2016. Wajumbe hao walikutana na kufanya mazungumzo na Wizara ya
Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam. Mradi
huu ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya
Korea kwa Dola za Marekani milioni 9.9. Kukamilika kwa mradi huo kutapunguza
adha ya maji taka na kuhakikisha usalama wa afya kwa wakazi katika Jiji la Dar
es Salaam.
83.
Mheshimiwa
Spika, mwezi Aprili 2017 nilifanya
ziara ya kikazi ya kwanza Barani Asia kwa kutembelea Jamhuri ya Korea nikiwa
kama Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wakati wa ziara
yangu nilifanya mkutano na mwenyeji wangu Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya
Nje wa nchi hiyo na tulizungumzia masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi
zetu, ikiwemo hali ya sasa ya ushirikiano wa kiuchumi na miradi ya maendeleo.
Aidha, tulijadili kuhusu hali ya Rasi ya Korea ambapo Tanzania tuliendelea
kusisitiza msimamo wetu wa kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika
kuhakikisha amani na usalama katika Rasi hiyo inapatikana. Nilifanya ziara hiyo
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano
ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
84. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka 25,
Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa
ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto
Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa mita 275
pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 48; na Ujenzi
wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,
Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600. Vilevile, Serikali
ya Korea imefadhili ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto iliyopo Chanika, Dar
es Salaam yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 ambayo inatarajiwa
kufunguliwa hivi karibuni. Aidha, Watanzania
zaidi ya 1,000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali
nchini Korea.
85. Mheshimiwa
Spika, kwa
upande wa Zanzibar, Jamhuri ya Korea imefadhili ujenzi wa shule ya Sekondari ya
Tumaini iliyopo Kwarara, Unguja. Aidha, Jamhuri ya Korea imekubali kuisaidia
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar vitendea kazi kwa lengo la kuijengea
uwezo mamlaka hiyo. Vilevile, Serikali ya nchi hiyo kupitia shirika lake la
Maendeleo la KOICA inatarajia kutekeleza mradi wa kilimo cha mpunga kwa njia ya
umwagiliaji Pemba na Unguja wenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 50.
86. Mheshimiwa
Spika, katika ziara yangu nilipata
pia fursa ya kukutana na Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Korea kwa lengo la kuwasilisha ombi la kujengewa
uwezo Serikali yetu katika masuala mbalimbali ya kiutendaji. Aidha, nilitumia
nafasi hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini kwa baadhi
ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea. Vilevile, nilitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya
Korea kwa ajili ya kujifunza uendeshaji wa Chuo hicho pamoja na kuimarisha
ushirikiano wakidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.
87.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mambo mengine Jamhuri ya Korea imeahidi
kuendelea kuisadia nchi yetu katika maeneo mbalimbali itakayohitaji kujengewa
uwezo, kuhamasisha wafanyabiashara kuwekeza nchini na kuimarisha ushirikiano wa
vyuo vyetu vya diplomasia.
Ushiriki wa Tanzania katika Makongamano ya Biashara
88.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi
ya Sekta Binafsi katika kuratibu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika
majukwaa ya kibiashara na uwekezaji ya kimataifa. Faida za majukwaa hayo ni
kufungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wa kitanzania na kuimarisha mahusiano
ya kibiashara na kuvutia uwekezaji nchini hususan katika sekta ya viwanda.
89.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa, majukwaa ambayo Wizara imeyafanikisha kwa kushirikiana na
wadau hao ni Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na India
lililofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Julai 2016; Jukwaa la Biashara kati ya
Tanzania na Rwanda lililofanyika Kigali mwezi Septemba 2016; Kongamano la Pili
la Biashara kati ya Tanzania na Misri lililofanyika Cairo mwezi Septemba 2016;
Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lililofanyika Lubumbashi mwezi Septemba 2016;
Kongamano la Pili la Biashara kati ya Tanzania na Comoro lililofanyika Zanzibar
mwezi Oktoba 2016; Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na
Israel lililofanyika Tel Aviv mwezi Novemba 2016; Kongamano la Biashara kati ya
Tanzania na Zambia lililofanyika Lusaka mwezi Machi 2017; Kongamano la Biashara
kati ya Tanzania na Mauritius lililofanyika Port Louis mwezi Machi 2017; Kongamano
la Biashara kati ya Tanzania na Czech lililofanyika Prague mwezi Mei 2017; na
Kongamano la Biashata kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Rome mwezi Mei
2017.
Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mambo ya
Nje ya Mwaka 2001
90.
Mheshimiwa
Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali
imeanza zoezi la kupitia Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 ili iweze kuendana
na mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yametokea ndani na nje ya
nchi. Ili kuwa na Sera inayokidhi mahitaji ya sasa na baadae, Wizara imeunda
Timu ya Wataalam inayojumuisha Wanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na
Chuo cha Diplomasia; Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali; pamoja na Sekta
Binafsi. Timu hiyo imeanza kufanya tathmini ya Sera hiyo kwa lengo la kupima
mafanikio yaliyopatikana; kubaini mapungufu; changamoto zilizojitokeza wakati
wa utekelezaji wake; na kuainisha namna ya kuzitatua.
91.
Mheshimiwa
Spika, Sera nzuri na inayotekelezeka kwa kiasi kikubwa
inategemea ushiriki wa wadau mbalimbali wakati wa uandaaji wake. Kwa kutambua
umuhimu huo, Timu hiyo imekusanya maoni kutoka pande zote za Muungano kwa
kuzingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo Viongozi
Wakuu Wastaafu; Mawaziri; wanadiplomasia; wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; wafanyabiashara mashuhuri; wajasiriamali
wadogo; watoa huduma; Asasi Zisizo za Kiserikali na wananchi kwa ujumla. Maoni
hayo yalipatikana kutoka Zanzibar na mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Mwanza,
Arusha, Ruvuma, Mbeya, Kigoma na Kagera.
92.
Mheshimiwa
Spika, kukamilika kwa tathmini hiyo kutawezesha kuandaliwa
kwa rasimu ya Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje ambayo itazingatia maoni ya wadau.
Naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine kutoa ushirikiano
kila wakati Timu ya Wataalam itakapohitaji kuwaona kwa ajili ya kupata maoni
yenu katika hatua inayofuata ya kuandaa rasimu ya Sera hiyo.
KUSIMAMIA MIKATABA NA MAKUBALIANO YA KIMATAIFA
93. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara iliratibu na kusimamia kusainiwa kwa Mikataba
12 na Hati za Makubaliano 28 baina ya Tanzania na nchi mbalimbali. Mikataba na
Makubaliano hayo ni kiashiria kikubwa katika kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina ya nchi yetu na nchi nyingine, mashirika ya Kikanda na
Kimataifa katika kuongeza kasi ya kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na
kutangaza utalii. Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa
mikataba hiyo kwa kuzingatia maslahi ya nchi yetu.
94.
Mheshimiwa Spika, orodha ya Mikataba na
hati za Makubaliano zilizosainiwa katika kipindi hicho ni kama inavyooneshwa
kwenye Kiambatisho Na. 1.
KUSIMAMIA MASUALA YANAYOHUSU KINGA NA HAKI ZA
WANADIPLOMASIA WALIOPO NCHINI
95.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali nchini ili
kuhakikisha kuwa jamii za kibalozi zinazowakilisha nchi zao na mashirika ya
kimataifa hapa nchini, zinapata haki zao kama ilivyoainishwa katika Sheria za
Kimataifa hususan Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka
1961. Aidha, Serikali inaendelea kutoa wito kwa Mabalozi, Wanadiplomasia, Wakuu
wa Mashirika ya Kimataifa na wafanyakazi wote wenye kinga kuendelea kuheshimu sheria,
kanuni na taratibu za nchi pamoja na Mkataba wa Vienna.
KUSIMAMIA NA KURATIBU MASUALA YA ITIFAKI NA
UWAKILISHI
96.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu ziara za viongozi
mbalimbali wa kitaifa kwenda nje na masuala ya itifaki na uwakilishi kwa
mabalozi na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
97. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeratibu ziara za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Baadhi
ya ziara za viongozi hao zilifanywa katika nchi za China, Djibout, Ethiopia, Indonesia,
India, Jordan, Kenya, Mauritius, Swaziland na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ziara hizi
zimeendelea kuwa na mafanikio makubwa siyo tu katika kukuza na kuimarisha
mahusiano baina yetu na nchi hizo pamoja na mashirika ya kimataifa bali
zimeendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha fursa za kiuchumi pamoja na
kuisaidia kupata ufadhili katika miradi mikubwa ya maendeleo.
98.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Wizara
imeendelea kuandaa na kuratibu sherehe za kuwasilisha hati za utambulisho za
Mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini. Miongoni
mwao ni Mabalozi wa nchi za Italy, Saudi Arabia, Morocco, Zambia, Cuba, Iran,
Burundi, Jamhuri ya Korea, Somalia, Ireland, Canada,
Thailand, Austria, Uingereza, Sudan, Slovakia, Ukraine, Ghana, Hungary, Belarus,
Guinea, Botswana, Niger, Mauritius, Cyprus, Bangladesh, Nepal, Gabon, Ecuador,
New Zealand na Congo Brazaville.
KUANZISHA
NA KUSIMAMIA HUDUMA ZA KIKONSELI
99.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwenye balozi
zetu nje na kutoa viza kwa raia wa kigeni wanaotembelea nchini; kurahisisha upatikanaji wa viza kwa maafisa na watendaji
wa Serikali, Vyama vya Siasa na Taasisi nyingine zinazostahili huduma hiyo;
Kushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili
Watanzania waishio nje ya nchi; na kutatua matatizo na kulinda maslahi ya
Watanzania wanaofanya kazi kwenye Balozi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa
hapa nchini.
KURATIBU MASUALA YA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA KIMATAIFA
A. Ushirikiano wa Kikanda
Umoja wa
Afrika
100. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Januari 2017. Katika
Mkutano huo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Wakuu wa
Nchi na Serikali walijadili na kupitisha maazimio kadhaa. Miongoni mwa maazimio
yaliyopitishwa ni:-
i. Umoja wa
Afrika kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya amani na usalama katika nchi
mbalimbali zenye migogoro barani Afrika zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, Libya, Burundi na Sudan Kusini;
ii. Nchi ambazo
hazijaanza kutekeleza Makubaliano ya kutumia asilimia 0.2 ya ushuru wa forodha
kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka nje ya Afrika kwa ajili ya Kuchangia Umoja
wa Afrika, zilipewa muda wa kujipanga hadi mwaka 2018;
iii. Nchi wanachama
zitafute fedha kwa ajili ya kutekeleza uondoshwaji wa vikwazo visivyo vya
kibiashara barani Afrika; na
iv. Ombi la nchi
ya Morocco kujiunga na Umoja huo.
101.
Mheshimiwa Spika, pembezoni mwa
Mkutano huo, Mheshimiwa Rais alikabidhi zawadi ya kinyago chenye kuashiria
Umoja kilichowekwa katika Jengo la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika
lililopewa jina la Julius Nyerere Peace
and Security Building. Jengo hilo lilizinduliwa mwezi Oktoba 2016 na kupewa
jina hilo kutokana na mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere katika masuala ya amani na usalama barani Afrika.
102.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano
huo, Mheshimiwa Rais pia alipata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali na
kujadili masuala yanayohusu mahusiano ya nchi yetu na ya Kimataifa. Viongozi aliokutana nao ni pamoja na
Mheshimiwa Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia; Mheshimiwa Prof.
Arthur Peter Mutharika, Rais wa Malawi; Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais
wa Jamhuri ya Uganda; Mhe. Abdel Fattah el-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya
Misri; Mheshimiwa Danny Antoine Rollen Faure, Rais wa Jamhuri ya Shelisheli; na
Mheshimiwa Antonio Gutteres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yake
na viongozi hao yalilenga katika kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kufungua
fursa katika nyanja za uwekezaji, biashara na utalii.
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC)
103.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea
kushiriki kikamilifu katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Wizara iliratibu
ushiriki wa nchi yetu katika masuala ya
siasa, ulinzi, usalama na utangamano wa Jumuiya hiyo kama ifuatavyo:-
Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama
katika Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
104.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika mwezi Agosti 2016 Mbabane, Swaziland,
Tanzania ilikabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,
Ulinzi na Usalama ijulikanayo kama Organ Troika
kwa kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017. Hii ni mara ya tatu kwa nchi
yetu kupewa jukumu hilo adhimu kutokana na imani waliyonayo nchi wanachama kwa
nchi yetu na uzoefu wetu katika utatuzi wa changamoto za kisiasa, kiulinzi na
kiusalama katika Ukanda huo. Kutokana na nafasi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa
Asasi hiyo, Wizara imeratibu na kuongoza ushiriki wa
Viongozi na Wajumbe mbalimbali kwenye utatuzi wa migogoro ndani ya Ukanda huu
ikiwemo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Falme ya Lesotho na Madagascar kama
ifuatavyo:-
i.
Ujumbe wa
Mawaziri wa Asasi ya Utatu ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama nchini Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo
105.
Mheshimiwa Spika, kufuatia kutetereka
kwa hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Septemba 2016
na kutokana na Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama,
nilipewa jukumu na Mheshimiwa Rais, kuongoza Ujumbe Maalum wa Mawaziri wa Utatu
wa Asasi hiyo nchini DRC. Ziara ya kwanza ya Ujumbe wa Mawaziri ilifanyika
mwezi Oktoba 2016, ambapo ujumbe ulikutana na wadau mbalimbali wa kisiasa
nchini humo na kusisitiza umuhimu wa kutafuta makubaliano kwa njia ya
majadiliano. Aidha, ujumbe huo uliunga
mkono Majadiliano ya Kitaifa yaliyokuwa yakiendelea nchini humo, yaliyosimamiwa
na Umoja wa Afrika chini ya uwezeshaji wa Mhe. Edem Kodjo, Waziri Mkuu Mstaafu
wa Togo. Majadiliano haya ndiyo yaliyofanikisha kufikiwa Makubaliano ya wadau wa siasa nchini DRC ya mwezi
Oktoba 2016.
106.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa
makubaliano ya mwezi Oktoba 2016 hayakuhusisha vyama vyote vya upinzani nchini
humo, juhudi za kushirikisha wadau wengine ambao hawakutia saini makubaliano
hayo ziliendelea chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki ambapo mwezi Desemba
2016 wadau wa siasa nchini humo walitia saini Makubaliano mapya. Makubaliano
hayo yanatoa mwongozo wa kuundwa kwa Serikali shirikishi ya Mpito ambayo
itaongoza nchini humo hadi Uchaguzi Mkuu utakapofanyika mwezi Desemba 2017. Katika
kutekeleza makubaliano hayo, mwezi Aprili
2017,
Mheshimiwa Rais Kabila alimteua Bw. Bruno Tshibala, kutoka chama cha Upinzani
cha Union for Democracy and Social
Progress (UDPS) kuwa Waziri Mkuu na mwanzoni mwa mwezi Mei 2017, Baraza
Jipya la Mawaziri lilitangazwa.
107.
Mheshimiwa Spika, kufuatia maendeleo
haya chanya, niliongoza ziara ya pili ya Ujumbe wa Mawaziri wa Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama nchini DRC mwezi Aprili 2017. Katika ziara hiyo, tumeweza
kuona jitihada anazozifanya Mheshimiwa Rais Kabila katika kipindi hiki cha
kuelekea maandalizi ya Uchaguzi Mkuu nchini humo. Hivi sasa, zoezi la
uandikishaji wapiga kura linaendelea na jumla ya wananchi milioni 23
wamekwishaandikishwa kati ya milioni 40 wanaotarajiwa kuandikishwa.
108.
Mheshimiwa Spika, kwa nafasi yetu ya Uenyekiti wa SADC tuna wajibu wa kuendelea kuunga
mkono juhudi hizi ili kuhakikisha amani na usalama vinatawala nchini DRC.
ii. Kamati ya Uangalizi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika nchini Lesotho
109.
Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa
Siasa, Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimteua Mhe. Jaji Mstaafu Frederick
Werema, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi ya SADC nchini Lesotho.
Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka nchi za Double Troika ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Msumbiji,
Swaziland na Tanzania, ilipewa jukumu la kufuatilia utekelezaji wa maamuzi
mbalimbali ya Wakuu wa Nchi na Serikali yanayolenga kurejesha amani ya kudumu
nchini humo.
110.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Kamati imefanya ziara tatu nchini
Lesotho, ambapo pamoja na mambo mengine, imebaini kwamba maagizo
yanayotolewa na Wakuu wa Nchi na Serikali kwa Serikali ya Lesotho
hayajatekelezwa ipasavyo huku hali ya kisiasa nchini humo ikiendelea
kutetereka. Itakumbukwa kuwa, Mfalme wa Lesotho alifikia uamuzi wa kuvunja
Bunge la nchi hiyo baada ya Wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na
Serikali. Kwa muktadha huo, Kamati ya Uangalizi ya SADC nchini Lesotho imetoa
pendekezo la kupeleka Waangalizi nchini Lesotho ili kufuatilia kwa karibu
utekelezaji wa mageuzi na hatua za kuiwezesha nchi hiyo kurudi katika hali ya
utulivu na amani huku ikijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi Juni 2017.
iii. Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Zambia na
Jamhuri ya Shelisheli
111.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea
kudumisha misingi ya demokrasia na amani katika Kanda, Wizara iliratibu na
kuongoza Timu ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu katika nchi za Zambia na
Shelisheli.
112.
Mheshimiwa Spika, Uchaguzi
Mkuu nchini Zambia uliofanyika mwezi Agosti 2016, ulihusisha vyama tisa
vilivyotoa wagombea wa Urais. Uchaguzi huo uliendeshwa kulingana na Katiba ya
Zambia ya mwaka 2016 ambapo Mheshimiwa Edgar Lungu alitangazwa mshindi na
kuapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo tarehe 16 Agosti 2016. Timu ya waangalizi
ilielezea kuridhika kwake na uchaguzi huo na kuwa ulikidhi vigezo vilivyowekwa
na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika vya kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
113.
Mheshimiwa Spika, nilipewa
heshima ya kuongoza Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika katika Uchaguzi Mkuu wa Wabunge wa
Jamhuri ya Shelisheli uliofanyika mwezi Septemba 2016. Katika uchaguzi huo
wagombea kutoka vyama vitatu vya siasa na wagombea huru watatu walishiriki
kugombea majimbo 25 ya uchaguzi katika nchi hiyo. Chama Tawala cha Parti Lepep kilipata majimbo 10 na
muungano wa vyama vya upinzani wa LDS
ulipata majimbo 15. Uchaguzi huo
uliokuwa huru na wa haki, ulifanyika kwa amani na utulivu na ulikidhi vigezo vilivyowekwa na Jumuiya. Kutokana na chama tawala kupata
ushindi mdogo katika uchaguzi huo, mwezi Oktoba 2016 aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Shelisheli Mheshimiwa James Alix Mitchel, alitangaza kujiuzulu wadhifa wake na
nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Mheshimiwa Danny Faure. Mheshimiwa
Faure aliapishwa tarehe 16 Oktoba 2016 kuwa Rais wa nchi hiyo.
iv. Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Siasa na
Diplomasia
114.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki Mkutano
wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Siasa na Diplomasia uliofanyika Jijini Dar es
Salaam mwezi Februari 2017. Katika Mkutano huo, Mawaziri wenye dhamana ya
masuala ya Mambo ya Nje, Diplomasia na Siasa walipokea na kujadili taarifa za
masuala ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo na Falme ya Lesotho. Vilevile, Mawaziri
walipokea na kujadili taarifa za tathmini za maombi ya Burundi na Comoro
kujiunga katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambapo Mawaziri
walikubaliana kwamba kwa kuwa Comoro imekidhi vigezo karibu vyote vilivyowekwa
na SADC, inaweza kujiunga isipokuwa kwa Burundi inayohitaji kufanyiwa uchambuzi
na mjadala wa kina.
v.
Mafunzo ya
Raia kuhusu Usuluhishi wa Migogoro
115.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa
maazimio ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni
kuanzisha program za kuwajengea uwezo watumishi katika masuala ya usuluhishi na
upatanishi wa migogoro. Kutokana na azimio hilo, Wizara iliratibu na kushiriki
katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi katika masuala ya utatuzi na
usuluhishi wa migogoro yaliyoandaliwa na SADC. Jumla ya watumishi 30 kutoka
Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali walishiriki mafunzo hayo. Hatua hiyo
imewezesha nchi yetu kuongeza idadi ya wataalam wa masuala ya usuluhishi na
upatanishi wa migogoro kwa njia ya amani.
vi.
Kuendeleza Viwanda katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
116.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya kuwa na uchumi wa viwanda, Wizara imeratibu ushiriki wa Tanzania katika
uandaaji wa Mkakati wa Jumuiya wa Kuendeleza Viwanda 2016 – 2063 na Mpango Kazi
wa utekelezaji wake. Mkakati huo unalenga kuziwezesha nchi wanachama ikiwemo
Tanzania, kuweka nguvu ya pamoja katika kukuza viwanda hivyo na kuziwezesha
nchi kushiriki zaidi katika mnyororo wa thamani kikanda na kimataifa. Mpango
Kazi wa Utekelezaji wa Mkakati huo uliidhinishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali
katika Mkutano wa Dharura uliofanyika Mbabane Swaziland mwezi Machi 2017 ambapo
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
vii. Ajira kwa Watanzania
katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
117.
Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi za ajira katika Sekretariati ya SADC, Wizara
ilifanikiwa kuzishawishi nchi Wanachama kuongeza muda wa mkataba wa Dkt.
Stergomena Laurent Tax, mtanzania ambaye kwa sasa ndiye Katibu Mtendaji wa
Jumuiya. Wakuu wa Nchi na Serikali waliridhia nyongeza ya mkataba wake kwa
kipindi cha pili na cha mwisho katika mkutano wao uliofanyika Mbabane,
Swaziland mwezi Machi 2017. Aidha, katika mkutano huo, Mhe. Jaji Mstaafu Regina
Rweyemamu aliteuliwa kuwa kati ya Majaji saba wanaounda timu ya Majaji wa
kuhudumia Mahakama ya Masuala ya Kiutumishi ya Jumuiya kwa kipindi cha miaka
miwili kuanzia Agosti 2017. Kufuatia ajira ya Mheshimiwa Jaji Mstaafu
Rweyemamu, idadi ya Watanzania walioajiriwa katika Sekretariati ya Jumuiya
imefikia 18.
Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari
ya Hindi
118.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa
kwanza wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na bahari
ya Hindi uliofanyika mjini Jakarta, Indonesia mwezi Machi 2017. Mkutano huo
umefanyika wakati Jumuiya ikiadhimisha miaka 20 ya kuanzishwa kwake. Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
alimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali walisaini
Makubaliano ya Jakarta ambayo yamebainisha mikakati, mipango na maazimio
yanayolenga kuongeza kasi ya maendeleo kwa nchi wanachama kwa kuanisha
mafanikio na changamoto za Jumuiya. Mkutano huo pia uliidhinisha Mpango Kazi wa
utekelezaji wa Makubaliano hayo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017 hadi
2021.
119.
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi huo umejumuisha maeneo ya vipaumbele vya Jumuiya ambavyo ni Biashara na
Uwekezaji, Usafiri wa Bahari, Uvuvi, Menejimenti ya Udhibiti wa Majanga,
Taaluma, Sayansi na Teknolojia, Utalii na Utamaduni, Uchumi Bahari na masuala
ya Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Kila Nchi mwanachama inatakiwa
kuchagua eneo moja au zaidi ambalo itatoa uongozi katika utekelezaji wake.
Wakati wa Mkutano huo, Tanzania ilionesha nia ya kutoa uongozi katika eneo la
Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Hata hivyo, taarifa rasmi za uchaguzi wa maeneo
hayo zitawasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa Maafisa Waandamizi
utakaofanyika nchini Indonesia, mwezi Julai 2017.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
119. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
ina dhamana ya kuratibu na kusimamia shughuli za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa mujibu wa Ibara ya 8 Ibara
ndogo ya 3 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka
1999. Kwa mantiki hiyo, Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania kwa
kutekeleza kikamilifu majukumu mbalimbali kwa lengo la kusimamia maslahi mapana
ya kitaifa katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-
a.
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha
i.
Biashara na
Uwekezaji katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki
120. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
katika kuandaa Taarifa ya Mwenendo wa Biashara na Uwekezaji katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya mwaka 2015 ikiwa na lengo la kufanya tathmini ya
utekelezaji wa Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Ripoti hiyo inabainisha
kuwa, utekelezaji wa Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umekuwa na
mafanikio katika kukuza biashara ya bidhaa na uwekezaji miongoni mwa Nchi wanachama.
121. Mheshimiwa Spika, biashara ya bidhaa miongoni
mwa Nchi Wanachama imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 4,483.6
mwaka 2011 hadi kufika Dola za Marekani
milioni 5,069.7 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 13. Kwa upande wa
Tanzania biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka
Dola za Marekani milioni 787.1 mwaka 2011 hadi kufikia Dola za Marekani milioni
1,203.6 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 53.
122. Mheshimiwa Spika, mauzo ya Tanzania kwenye Soko la Afrika Mashariki yameendelea kuongezeka
mwaka hadi mwaka kutoka Dola za Marekani milioni 409.0 mwaka 2011 hadi Dola za
Marekani milioni 924.9 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 126 wakati
manunuzi yalipungua kutoka Dola za Marekani milioni 378.1 mwaka 2011 hadi Dola
za Marekani milioni 278.1 mwaka 2015 sawa na punguzo la asilimia 26.5. Bidhaa
zilizouzwa kwa wingi ni pamoja na visimbuzi, kamba za katani, mbogamboga,
matunda, tangawizi, chai, karatasi, vyakula vya mifugo na sabuni.
123. Mheshimiwa Spika, malengo ya Umoja wa Forodha ni pamoja na kukuza biashara ya bidhaa na
kuchochea uwekezaji miongoni mwa Nchi Wanachama, na ndio maana tuna kampuni
kutoka nchi wanachama zilizowekeza Tanzania na kampuni za Tanzania zilizowekeza
kwenye Nchi nyingine Wanachama. Baadhi ya kampuni kutoka Tanzania ni Bakhresa,
Mount Meru, Benki ya CRDB na Bank M. Aidha, kampuni zilizowekeza hapa kwetu ni
pamoja na Benki ya KCB na NAKUMAT. Uwekezaji unaovuka mipaka unachangia kukuza
biashara na ajira miongoni mwa nchi wanachama. Katika mwaka 2016, Tanzania
iliandikisha Jumla ya miradi 6 kutoka nchi za Kenya, Uganda na Rwanda yenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 2.5.
ii.
Uondoaji wa Vikwazo Visivyo
vya Kiforodha
124.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo
vya Kiforodha kwa lengo la kukuza biashara baina ya Nchi Wanachama na kupunguza
gharama za kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika barabara
Kuu ya Kati, Tanzania imeendelea kutumia vituo vitatu katika kupima uzito wa malori yanayotumia barabara
hiyo vilivyopo Vigwaza,
Nyuki na Nyakahura.
125. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki,
jumla ya Vikwazo Visivyokuwa vya Kiforodha 116 katika Jumuiya viliondolewa.
Kati ya hivyo, vikwazo vinavyoihusu Tanzania vilivyoondolewa ni:- Kodi ya asilimia 1.5 kwa ajili
ya maendeleo ya reli kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka Nchi Wanachama;
kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya taratibu za uingizaji na uuzaji wa
bidhaa; kodi kwa bidhaa za maonesho ya 40 ya Sabasaba kutoka kwenye Nchi
Wanachama; na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufunga ofisi mapema
(saa 9 Alasiri) na hivyo kukwamisha ukaguzi wa mizigo katika bandari kavu.
126. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa Tanzania pekee ni pamoja na
kuimarisha uwezo wa Kamati ya Kitaifa ya Uondoaji Vikwazo visivyo vya forodha
na kuiwezesha kufanya vikao kila mwezi badala ya kila robo ya mwaka kama
ilivyokuwa awali hivyo kupunguza malalamiko ya vikwazo hivyo kukaa muda mrefu
bila kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
iii. Mapitio
ya Wigo wa Pamoja wa Ushuru wa Forodha na Sheria ya Uasilia wa Bidhaa
127. Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kusimamia mapitio ya Wigo wa Pamoja wa
Ushuru wa Forodha na Sheria ya Uasilia wa Bidhaa. Katika kukamilisha azma hiyo, Nchi Wanachama
zimekamilisha Hadidu za Rejea, kupendekeza vigezo vitakavyotumika katika kuweka
kiwango cha ushuru wa forodha katika bidhaa zinazotoka nje ya Jumuiya na
kuandaa Mpango Kazi wa kukamilisha kazi hiyo.
128. Mheshimiwa Spika, Wajumbe
wa Tanzania wanaoshiriki katika zoezi hilo wanatoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Shirikisho la wenye
Viwanda Tanzania. Zoezi hili ni muhimu na linagusa mustakabali wa nchi yetu
katika kuendeleza viwanda, uwekezaji na kukuza biashara. Hivyo, natoa wito kwa
sekta binafsi kushirikiana kikamilifu na kikosi kazi hiki, ili kutoa taarifa
zitakazowezesha mapitio yatakayofanyika kuwa na tija kwa ustawi wa taifa letu.
b.
Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja
129.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki kwenye
utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Mafanikio ya
utekelezaji wa Itifaki hiyo kwa upande wa Tanzania ni pamoja na kuandaa na
kuanza kutumia Kanuni Mpya za Uhamiaji za mwaka 2016; utaratibu wa ushirikiano
kati ya taasisi zinazotoa huduma mipakani na Sheria ya Ajira za Kigeni ya mwaka
2015 ambayo imezingatia matakwa ya Itifaki ya Soko la Pamoja.
c.
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha
130.
Mheshimiwa Spika, Nchi Wanachama zimekamilisha Sera ya Mikataba ya Kodi
ambayo itatumika kuandaa Modeli ya Mikataba ya Kodi itakayotumiwa na kila nchi
mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika majadiliano yanayohusu kodi na
nchi nyingine. Hii itawezesha kuleta uwiano wa viwango vya kodi vinavyotozwa na
nchi wanachama kwa wawekezaji kutoka nje ya Jumuiya.
d.
Ushirikiano Baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanda Nyingine
131. Mheshimiwa Spika, Mkutano 17
wa Dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika
mwezi Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba 2016 ulipokea na kujadili suala la
Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya
Ulaya (EAC-EU Economic Partnership
Agreement –EPA). Baada ya majadiliano ya kina, Viongozi Wakuu wa Nchi
walikubaliana kuendelea na mashauriano ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za
EPA zilizokuwa zimebainishwa. Katika kutekeleza makubaliano ya Viongozi Wakuu wa Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu EPA, Wizara
ilishirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufanya uchambuzi wa
ndani wa kina na kuandaa mapendekezo ya msimamo wa nchi. Uchambuzi uliofanyika ulionesha kuwa Mkataba huo siyo rafiki kwa ustawi wa Taifa letu hasa katika
utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi
ya uchumi wa Viwanda.
132. Mheshimiwa Spika, kufuatia maombi
ya Bunge
lako Tukufu, Serikali iliwasilisha Mkataba huo Bungeni. Baada ya majadiliano,
Bunge lilitoa Azimio la kuishauri Serikali isisaini Mkataba huo.
133. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa
18 wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini
Dar es salaam mwezi Mei 2017, suala la Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya
Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki lilijadiliwa. Viongozi Wakuu wa
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kuwa Rais wa Jamhuri ya
Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya kuongoza ujumbe kwenda Umoja wa Ulaya
kwa lengo la kutafuta muafaka wa namna ya kuondoa changamoto zilizopo katika
Mkataba huo. Aidha, ujumbe huo unalenga kushawishi Umoja wa Ulaya kutoiadhibu
Kenya wakati majadiliano ya kutafuta muafaka yakiendelea.
134. Mheshimiwa Spika, Viongozi hao pia
walikubaliana kuwa, endapo Juhudi za kupata muafaka kuhusu changamoto za
Mkataba wa EPA kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya hazitazaa
matunda ndani ya kipindi cha miezi sita, utaangaliwa uwezekano wa nchi
zitakazokuwa tayari kuendelea na Mkataba wa EPA kwa mujibu wa ibara 7(e) ya
Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohusu kanuni ya ‘‘Variable
Geometry’’.
135. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri wa Eneo
Huru la Biashara la Utatu wa COMESA-EAC-SADC uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi
Oktoba 2016. Mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa ya maeneo yaliyosalia
katika majadiliano ya awamu ya kwanza ambayo ni Uondoaji wa Ushuru wa Forodha;
Uasilia wa Bidhaa; na Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara. Vilevile, Mkutano
ulipokea na kuridhia baadhi ya viambatisho vya Mkataba huo vinavyohusu Vikwazo
Visivyo vya Kiforodha; Ushirikiano katika Masuala ya Forodha; Uwezeshaji
Biashara; Biashara ya Bidhaa zinazopita kwenda nchi nyingine; Vikwazo vya
Kiufundi vya Kibiashara na Afya ya Wanyama na Mimea. Baraza la Mawaziri pia
lilipokea taarifa ya utiaji saini Mkataba huo ambapo jumla ya nchi 18 tayari
zilikuwa zimesaini. Kufuatia hatua hiyo, Baraza la Mawaziri liliagiza nchi
ambazo hazijasaini kufanya hivyo na zile ambazo zimesaini ziendelee na taratibu
za kuridhia. Tanzania imeshasaini Mkataba huo na taratibu za kuridhiwa zinaendelea.
136. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
Kongamano la 14 la AGOA lililofanyika Washington DC, Marekani mwezi Septemba
2016. Kaulimbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Kuimarisha Ushirikiano wa
Kibiashara na Uwekezaji kati ya Marekani na Afrika”. Masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na: Biashara na masuala ya
wafanyakazi; Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa AGOA; Namna ya kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu; Kuvutia uwekezaji ili kuhakikisha
Mpango wa AGOA unatumika ipasavyo;
Uwiano wa usalama na biashara kimataifa;
Mkataba wa urahisishaji biashara; Uwezeshwaji wa upatikanaji wa mitaji kwa
wajasiriamali wadogo na wa kati; na Mikakati ya kunufaika na mpango wa AGOA.
137. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania
katika Majadiliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika. Hadi sasa nchi za Umoja wa Afrika zimepitisha
kanuni za kuendesha majadiliano, hadidu za rejea za vikundi kazi
vitakavyoshiriki katika majadiliano ya maeneo yenye utaalam mahsusi, pamoja na
kupitisha mpango kazi wa namna ya kukamilisha majadiliano ya uanzishwaji wa
Eneo Huru la Biashara la Afrika.
e.
Sekta za Uzalishaji
138. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika majadiliano ya Rasimu ya Muswada wa Sheria ya
Afya ya Wanyama na Mimea wa Jumuiya yaliyofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba
2016. Muswada huo unalenga kuwa na sheria itakayoziwezesha nchi
wanachama kutekeleza sera, taratibu na mikakati iliyobainishwa kwenye Itifaki
ya Afya ya Wanyama na Mimea ya Jumuiya, kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na
usalama wa chakula cha Binadamu na Wanyama.
139.
Mheshimiwa Spika,
Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano ya
Rasimu ya Mkataba wa kukuza na kuinua Viwanda Vidogo na vya Kati katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Mkataba huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kutatua changamoto na kutoa kipaumbele kwa maendeleo
ya viwanda vidogo na vya kati katika
Jumuiya. Miongoni mwa masuala ambayo yamepewa kipaumbele katika kuinua Sekta hii muhimu ni:- mazingira rafiki ya
ulipaji kodi; uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo kwa kurasimisha biashara
zisizo rasmi; utoaji wa mikopo kwa riba nafuu; na kuanzisha vituo vya kuwajengea uwezo wajasiriamali. Aidha, katika
hatua ya utekelezaji wa Sera na Mkakati wa kuendeleza Viwanda wa Afrika Mashariki, nchi wanachama
zinaendelea na majadiliano ya Rasimu ya
muswada wa Uendelezaji wa Viwanda katika Jumuiya.
140.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu na kushiriki katika Maonesho ya 17 ya Juakali/Nguvukazi kwa mwaka 2016
yaliyofanyika Kampala, Uganda mwezi Desemba 2016. Maonesho haya yalijumuisha
wajasiriamali zaidi ya mia saba kutoka nchi wanachama na yalikuwa na kaulimbiu
isemayo “Nunua bidhaa za Afrika
Mashariki, Jenga Uchumi wa Afrika Mashariki”.
141.
Mheshimiwa Spika, Jumla ya Wajasiriamali 138 kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar walishiriki maonesho hayo ambapo Tanzania ilifanikiwa kutoa washindi
watatu ambao ni Bi. Margareth Kiondo katika bidhaa
za vinyago; Tegoe’s Honey Group
katika bidhaa za asali; na katika bidhaa za nguo mshindi alikuwa Bi. Fridah
Tarimo. Washindi hao wote walitunukiwa vyeti
vya ubora wa bidhaa katika maonesho hayo.
142.
Mheshimiwa Spika, Wajasiriamali
wengi walitumia fursa hiyo kutangaza, na kuuza bidhaa zao, kubadilishana ujuzi,
teknolojia na uzoefu katika fani mbalimbali za uzalishaji wa bidhaa pamoja na
utafutaji wa masoko na pia kujenga mahusiano ya kibiashara baina yao.
143.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika utekelezaji wa miradi na programu za
Jumuiya ya Afrika Mashariki za Uendelezaji wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma
za Jamii kama ifuatavyo:
i.
Vituo vya Kutoa
Huduma kwa Pamoja Mipakani
144. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu na kushiriki katika ujenzi na uendeshaji wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani. Katika
Kituo cha Rusumo kilichopo mpakani mwa Tanzania na Rwanda limefunguliwa Tawi la
Benki ya NMB ndani ya jengo la Kituo hicho lililoanza kutoa huduma mwezi Julai
2016. Kufunguliwa kwa Tawi hilo kumeongeza ufanisi katika kutoa huduma kituoni
hapo. Aidha, mnamo mwezi Februari 2017 ulifanyika utafiti wa kuangalia matokeo
ya kuanzisha Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Huduma kwenye Kituo hicho. Matokeo ya
awali ya Utafiti huo uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan yanaonesha
kuwa muda wa kukamilisha taratibu kwa malori ya mizigo yanayovuka mpaka kupitia
Kituo hicho umepungua kutoka wastani wa siku moja hadi saa moja na nusu. Kwa
sasa malori zaidi ya 200 yanavuka mpaka kupitia Kituo hicho kwa siku
ikilinganishwa na wastani wa malori 90 kabla ya utaratibu wa Mfumo huo kuanza
kutumika mwezi Machi 2016.
145.
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Afrika
imetoa msaada wa Dola za Marekani 525,120 kwa lengo la kuwezesha uendeshaji wa Kituo cha Namanga kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya. Fedha hizo ni
kwa ajili ya ununuzi wa samani
na vifaa vya TEHAMA; kuwajengea uwezo
wa utekelezaji wa Mfumo huo Watalaam wa Taasisi zinazotoa huduma mpakani; na
kutoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa Kituo hicho. Mwezi
Novemba 2016, Wizara iliratibu makabidhiano ya vifaa vya TEHAMA vilivyonunuliwa
kupitia msaada huo. Vifaa hivyo ni pamoja na
komputa 80, swichi 8, printa 32 na scanner
20.
146. Mheshimiwa Spika, vilevile,
kuhusu Kituo cha Tunduma kilichopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, Mkataba wa
Ujenzi kati ya Mkandarasi Kampuni ya
Nadhra Engineering Construction Company Limited na taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA), ambayo ni
mfadhili wa ujenzi wa Kituo hicho ulisainiwa mwezi Oktoba 2016. Ujenzi wa Kituo
hicho ulianza mwezi Novemba 2016 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2018.
ii. Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara
147. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu ya Usimamizi
wa Miradi ya Barabara za Afrika Mashariki uliofanyika Mombasa, Kenya mwezi
Desemba 2016. Pamoja na mambo mengine, nchi wanachama zilionesha kuridhishwa na
hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili/Taveta – Voi,
ikiwemo sehemu ya Sakina - Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 ambayo ujenzi
wake utakuwa wa kipindi cha miaka miwili na nusu kuanzia mwezi Februari 2016.
148. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Wataalam wa
Kikanda inayosimamia utekelezaji wa
Mradi wa kuwezesha Sekta ya Uchukuzi na Biashara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki
uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2016. Katika Mkutano huo,
Tanzania iliwasilisha miradi ya kipaumbele katika sekta za Bandari, Nishati, Reli, Barabara na Anga ili
ijumuishwe katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo. Aidha, nchi
wanachama zinaendelea na majadiliano ya Rasimu ya Mfumo wa Sheria wa Matumizi
ya Mtaala wa Mafunzo ya Madereva wa Magari ya Biashara katika Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
149.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki majadiliano ya
Mpango wa Miaka 5 wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi na Biashara kwa Njia ya
Barabara kwenye eneo huru la biashara la utatu wa COMESA – EAC – SADC
uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Novemba 2016. Mpango huo unalenga kuwianisha sera, sheria, kanuni na mifumo ya
kitaasisi kwenye sekta ya uchukuzi kwa njia ya barabara kwenye nchi zote 19
Wanachama wa Utatu huo.
iii. Sekta ya
Mawasiliano
150. Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki katika kuandaa Rasimu ya
Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Posta kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mkakati huo una lengo la kuboresha Huduma za
Mawasiliano zinazotolewa kwa njia ya Posta kwa kuzingatia mabadiliko ya
teknolojia kwenye sekta hiyo. Majadiliano kuhusiana na mkakati huo yanaendelea
kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.
151. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Ziara ya Kamati ya Mawasiliano,
Biashara na Uwekezaji ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyofanyika
jijini Dar es Salaam mwezi Februari 2017. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia
hatua zilizofikiwa kuhusiana na uwianishaji wa gharama za maunganisho ya simu
za mkononi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamati hiyo ilikutana na
Wataalam wa Sekta ya Mawasiliano hapa nchini. Aidha, ili kuleta ufanisi katika
utekelezaji wa Mpango huo, wadau wa mawasiliano walipendekeza Nchi Wanachama kuweka Mitambo ya kufuatilia na kupambana na uhalifu wa
kimtandao na Jumuiya
ya Afrika Mashariki kufanya utafiti wa kubainisha faida na changamoto za mfumo
huo.
iv. Sekta ya
Elimu
152.
Mheshimiwa Spika, Wakuu wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wao wa 18
uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2017 walitoa Tamko la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Eneo Moja la
Elimu ya Juu (Declaration on the
Establishment of the East African Community Common Higher Education Area).Tamko
hilo lina lengo la kuhakikisha mafanikio ambayo hadi sasa yamepatikana katika
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye elimu ya juu yanawianishwa
ili kuwa na mfumo mmoja wenye kuwezesha utolewaji wa elimu na mafunzo yenye
viwango bora vitakavyotambulika baina ya Nchi Wanachama. Wakuu wa Nchi
wameliagiza Baraza la Mawaziri la Jumuiya kufanya mageuzi yanayohitajika katika
Elimu na Mafunzo ili kufikia lengo hili.
153.
Mheshimiwa Spika, kila mwaka Wanafunzi wa Sekondari wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki huandaliwa shindano la kuandika Insha na washindi watano hutunukiwa
vyeti pamoja na zawadi na Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mada ambayo wanafunzi huandikia Insha hulenga
kuwajengea uelewa wa Mtangamano wa Afrika Mashariki. Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wao wa 18 uliofanyika Jijini Dar es
Salaam mwezi Mei 2017 walitoa vyeti pamoja na zawadi kwa washindi wa Shindano
la Insha la Jumuiya la mwaka 2016. Kwa
upande wa Tanzania mshindi alikuwa ni Alex Mbogo kutoka Shule ya Sekondari
Kibaha, Mkoa wa Pwani.
154. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo uliofanyika Nairobi, Kenya
mwezi Oktoba 2016. Katika Mkutano huo Nchi Wanachama ziliidhinisha Mpango
Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Majukumu ya Kamisheni ya Kiswahili ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la Mpango Mkakati huo ni kuratibu na kukuza
matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kuzijengea uwezo taasisi zinazojihusisha na utafiti wa Kiswahili.
v.
Sekta ya
Jinsia na Maendeleo ya Jamii
155.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika
Kongamano la Pili la Watoto la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofanyika
Nairobi, Kenya mwezi Agosti 2016.
Lengo la Kongamano hilo lilikuwa ni kuwakutanisha pamoja Watoto wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli zinazowahusu na
kuwajengea uwezo wa kutambua haki zao. Katika
Kongamano hilo, Sera ya Mtoto ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inalenga kulinda haki za watoto ilizinduliwa rasmi.
Katika Kongamano hilo, watoto wawili na mwangalizi wao mmoja kutoka Tanzania
walishiriki.
vi.
Sekta
ya Kazi na Ajira
156. Mheshimiwa Spika, Wizara
iliratibu Mkutano wa kuandaa Mpango wa
Pamoja wa Kubadilishana Wafanyakazi Vijana miongoni mwa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba 2016. Mpango huo
unalenga kutekeleza Ibara ya 10 ibara ndogo ya 8 ya Itifaki ya Soko la Pamoja
la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika mpango
huo, nchi Wanachama zinajadili mpango wa kubadilishana vijana waajiriwa katika
nchi za Jumuiya hiyo.
Kukamilika kwa Mpango huo kutatoa fursa kwa vijana wetu kujijengea uwezo na
kupata uzoefu katika fani mbalimbali.
vii.
Sekta ya Afya
157. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea na uratibu wa
ukamilishwaji wa Sera ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sera hii
iliidhinishwa na Mkutano wa 35 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika
Arusha mwezi Aprili 2017. Msingi Mkuu wa Sera hii ni kutoa mwongozo katika
kukabiliana na changamoto katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
huduma za afya zinaboreshwa hasa katika upatikanaji wa dawa zenye ubora,
kuhimiza utoaji huduma za afya kwa kuzingatia misingi ya maadili, sheria na
kujali utu. Aidha, Sera hii inatoa mwongozo wa kuandaa mikakati ya kukabiliana
na magonjwa ya mlipuko ya binadamu na wanyama. Vilevile, itachochea ukuaji wa
ubunifu na tafiti za kisayansi na pia kuzalisha
wataalam wenye uwezo na weledi katika masuala ya Afya.
viii. Miradi na Programu za Mazingira
158.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 17 wa
Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria pamoja na Maadhimisho
ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria
yaliyofanyika Kisumu, Kenya mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Nchi
Wanachama zilizindua Mpango Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Dhana ya
Idadi ya Watu, Afya, na Mazingira wa mwaka 2016 – 2021. Mpango Mkakati huo utaongoza Asasi za Kiraia, Washirika wa
Maendeleo na Sekta binafsi katika kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa dhana
hiyo wakati wa utekelezaji wa miradi yao.
159. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Kongamano la Utafiti
wa Kisayansi na Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria lililofanyika Jijini Mwanza
mwezi Februari 2017. Kongamano hilo lilifunguliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na maazimio
mengine, Kongamano hilo liliazimia Jumuiya ya Afrika Mashariki iendelee na
maandalizi ya awamu ya tatu ya Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria
kwa kuanza kutafuta rasilimali fedha.
g.
Utekelezaji wa
Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama
160. Mheshimiwa Spika, katika mkutano
wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika
jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhi Uenyekiti wa
Jumuiya hiyo kwa Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.
Hii ni kufuatia Tanzania kushika nafasi hiyo kwa vipindi viwili mfululizo.
Katika kipindi cha Uenyekiti wa Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipiga
hatua kubwa katika utekelezaji wa programu na miradi yake mbalimbali.
161. Mheshimiwa
Spika,
miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuanza kwa utekelezaji wa
Himaya Moja ya Forodha ikiwa ni utekelezaji wa Itifaki ya Jumuiya ya Umoja wa
Forodha. Utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha umewezesha kupunguza muda wa
kusafirisha mizigo na abiria baada ya vituo 11 kati ya 15 vya kutoa huduma kwa
pamoja kujengwa. Kwa upande wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara
na reli zinazounganisha mataifa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili – Taveta - Voi kati ya
Tanzania na Kenya unaendelea ambapo kipande cha kutoka Sakina hadi Tengeru ujenzi
wake unaendelea. Ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Tabora – Mwanza
na Tabora – Kigoma – Keza – Msongati itakayounganisha Tanzania na nchi za
Burundi na Rwanda umeanza. Aidha, katika kipindi hicho Jamhuri ya Sudan Kusini
ilikamilisha taratibu za kisheria zilizoiwezesha kuwa Mwanachama kamili wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya
Hati za Kuridhia Mkataba wa Kujiunga na Jumuiya hiyo mwezi Septemba 2016.
162. Mheshimiwa
Spika, Mkataba
wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeainisha Shirikisho la Kisiasa
kuwa ni hatua ya mwisho ya mtangamno wa Afrika Mashariki na unatekelezwa hatua
kwa hatua kuanzia Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja kisha Umoja wa Fedha na
hatimaye Shirikisho la Kisiasa. Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya
katika Mkutano wao wa Kawaida wa 18 wameidhinisha Jumuiya kuanza na mfumo wa Confederation kama hatua ya kipindi cha
Mpito cha kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Aidha,
wameagiza Baraza la Mawaziri kuunda timu ya wataalam wa masuala ya katiba ili
kuandaa Rasimu ya Katiba itakayoiwezesha Jumuiya kuanza kutekeleza mfumo huo.
163. Mheshimiwa
Spika,
kufuatia kukamilika kwa kipindi cha utumishi cha Dkt. Enos Steven Bukuku,
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mipango na Miundombinu, Mkutano wa
18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama ulimteua na kumuapisha Injinia Stephen Daud Malekela
Mlote kutoka Tanzania kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Vilevile, mkutano huo ulimteua Jaji Dkt. Charles Oyo Nyawello kutoka Jamhuri ya
Sudan Kusini kuwa jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki katika Mahakama ya
Awali.
164. Mheshimiwa
Spika,
jitihada za usuluhishi wa Mgogoro wa Kisiasa Nchini Burundi zinaendelea chini
ya Mwezeshaji Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kukamilika awamu ya mashauriano na
wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Burundi, Mwezeshaji ameainisha maeneo
kadhaa ya msingi ambayo yatakuwa sehemu ya majadiliano.
165. Mheshimiwa
Spika, maeneo
hayo ni usalama na kumaliza vitendo vya uvunjifu wa amani; utawala wa sheria na
kumaliza ukiukwaji wa haki za binadamu;
hali ya utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa Arusha wa Mwaka 2000; masuala
ya demokrasia; masuala ya kijamii na binadamu, madhara ya uchumi
yaliyosababishwa na mgogoro huo; uhusiano wa nchi hiyo na majirani zake pamoja
na Jumuiya za Kimataifa; na utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano Maalum kuhusu
Burundi wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya Kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa. Maeneo hayo yatawasilishwa katika
awamu ya kwanza ya majadiliano ambayo inahusisha viongozi na wadau muhimu kisiasa
nchini Burundi ili kuainisha yale ambayo wanakubaliana. Wadau wengine kama
asasi za kijamii, viongozi wa kidini, makundi ya wanawake na vijana
watashirikishwa katika awamu ya pili ya usuluhishi ili kujadili maeneno ambayo
yatakosa muafaka katika awamu ya kwanza.
166. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
katika Mkutano wa 7 wa Dunia wa Masuala
ya Uchaguzi sanjari na Programu ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Marekani wa mwaka
2016 uliofanyika katika majimbo ya Washington DC, Maryland na Virginia mwezi Novemba
2016. Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kujenga uelewa na kuimarisha
usimamizi/uendeshaji na uangalizi wa uchaguzi kwenye Kanda mbalimbali ikiwemo
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Mkutano huo ulikuwa ni fursa kwa wajumbe na
Jumuiya ya Afrika Mashariki kujifunza na kubadilishana uzoefu na Kanda nyingine
kuhusu namna ya kuendesha chaguzi za kidemokrasia na kuimarisha amani na
usalama wakati wa uchaguzi.
h. Uwianishaji
wa Vibali vya Kazi na Ukaazi katika Nchi Wanachama
167. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika
majadiliano ya uwianishwaji wa madaraja ya vibali vya kazi/ukaazi na ada ya
vibali kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kuzingatia kuwa
suala la vibali vya kazi Tanzania Bara na
Zanzibar linashughulikiwa na Wizara tofauti, Tanzania imepewa muda hadi
kufikia mwezi Septemba 2017 kuwianisha
Sheria na Kanuni zinazohusiana na utoaji wa vibali vya kazi na tozo za ada kati
ya Tanzania Bara na Zanzibar kabla ya kukamilisha majadiliano hayo katika ngazi
ya Jumuiya. Wizara inaendelea kuratibu majadiliano ya ndani kuhusu suala hili.
i.
Maandalizi ya Pasi Mpya ya Kusafiria ya Kimataifa ya Afrika
Mashariki
168. Mheshimiwa
Spika Wizara iliratibu na kushiriki katika
Mkutano wa Wakuu wa Uhamiaji kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
uliofanyika mjini Moshi mwezi Novemba 2016. Mkutano huo ulifanya tathmini ya
hatua iliyofikiwa na Nchi Wanachama katika kukamilisha maandalizi ya kuanza
matumizi ya Pasi Mpya ya Kusafiria ya Kimataifa ya Afrika Mashariki ifikapo
mwezi Aprili 2017.
169. Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huo ilibainika kuwa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo katika hatua tofauti za
maandalizi ya kutoa Pasi hizo. Nchi za Burundi na Kenya zimekamilisha
maandalizi ya kutoa pasi hizo, wakati Tanzania, Uganda na Rwanda zinaendelea
kukamilisha taratibu za utekelezaji. Hivyo, ilipendekezwa muda wa kuanza kutoa
Pasi hizo usogezwe mbele kutoka mwezi Aprili 2017 hadi mwezi Desemba 2017.
j.
Mapambano Dhidi ya Ugaidi, Uharamia, Biashara Haramu ya
Binadamu na Dawa za Kulevya
170. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
katika Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Kupambana na Ugaidi uliofanyika Entebbe,
Uganda mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Nchi Wanachama zilibadilishana
uzoefu kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi, kuweka mfumo mmoja wa kurekodi
na kubadilishana taarifa na mienendo ya ugaidi. Aidha, nchi wanachama
zilikubaliana kuhuisha sheria za kupambana na ugaidi katika Jumuiya kwa lengo
la kuwa na tafsiri moja na kiwango sawa cha adhabu.
171.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Kikanda wa
kupambana na uharamia katika Bahari ya Hindi ambao unahusisha pia Kanda za
SADC, COMESA na IGAD. Majukumu ya utekelezaji wa Mkakati huo yamegawanywa
kikanda ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki imepangiwa jukumu la kuhifadhi
watuhumiwa wa uharamia watakaokamatwa, kuendesha mashtaka dhidi yao na
kuwafunga watakaopatikana na hatia na kisha kuwarejesha nchini mwao mara baada
ya kumaliza vifungo.
172.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hilo, Jumuiya ya Afrika Mashariki iliandaa
mafunzo mwezi Aprili 2017 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Waendesha Mashtaka na
Wanasheria kuhusu namna ya kushughulikia kesi za uharamia na kuendesha mashtaka
dhidi ya watuhumiwa wa uharamia.
173. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu utekelezaji wa
Mkakati wa Kikanda wa Kupambana na Biashara haramu ya Binadamu. Nchi Wanachama
zimebaini kuwa tatizo la biashara haramu ya binadamu katika Jumuiya limekuwa
likiongezeka kila mwaka na kwamba wahanga wakubwa wa biashara hiyo ni wanawake
na watoto huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni umaskini. Nchi Wanachama
zimekubaliana kuhuisha sheria za kupambana na biashara hiyo na kuimarisha
mawasiliano kuhusiana na mienendo ya wahusika katika biashara hiyo.
174. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu utekelezaji wa Mkakati
wa Kikanda wa Kupambana na dawa za kulevya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
ambapo Nchi Wanachama zilibadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali. Maeneo
hayo ni pamoja na njia na mbinu mpya za usafirishaji na uzalishaji wa dawa za
kulevya; kubainisha maeneo ambayo ni kitovu cha uzalishaji wa dawa za kulevya
hasa bangi; na kuainisha malighafi za viwanda zinazotumika kuzalisha dawa za
kulevya. Aidha, Nchi Wanachama zimekubaliana kuhuisha sheria za kupambana na
dawa za kulevya, kuanzisha kanzidata ya kutunza taarifa za watuhumiwa na
kuandaa Mkakati wa kuelimisha umma juu ya madhara ya dawa hizo.
k.
Mafunzo kwa Maafisa Kadeti
175. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
Mkutano wa Wakufunzi wa Vyuo vya Maafisa Kadeti wa Majeshi ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Kigali, Rwanda mwezi Machi 2017.
Mkutano huo, uliandaa na kuwianisha baadhi ya masomo ambayo yatatumika kama
rejea kwa vyuo vyote vya Maafisa Kadeti kwenye Nchi Wanachama wa Jumuiya.
Aidha, Wakuu wa Vyuo hivyo walikubaliana masuala yatakayofundishwa kwenye
masomo ili kuleta ulinganifu katika mafunzo hayo.
l.
Zoezi la Pamoja la Kijeshi la Afrika Mashariki
176. Mheshimiwa
Spika, Wizara iliratibu na kushiriki
katika maandalizi ya zoezi la Pamoja la Kijeshi la Afrika Mashariki la Kamandi
ya pamoja ya kijeshi lililofanyika Bujumbura, Burundi mwezi Februari 2017.
Zoezi hili pia limepangwa kufanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2017.
Lengo la zoezi hilo ni kujenga uwezo wa majeshi yetu katika Operesheni za
kulinda Amani, kupambana na Ugaidi, kukabiliana na Majanga na Uharamia.
177. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika maandalizi ya
Rasimu ya awali ya majadiliano ya Uundaji wa Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatua hiyo ni utekelezaji wa
matakwa ya Itifaki ya Ushirikiano katika Ulinzi ya Jumuiya ambapo Nchi
Wanachama zinatakiwa kukamilisha majadiliano hayo ndani ya mwaka mmoja tangu
kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo. Tayari, Baraza la Mawaziri la Jumuiya limeidhinisha
Rasimu hiyo kama Mwongozo wa Majadiliano ya Mkataba huo.
Bunge
la Afrika Mashariki
178. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki katika Mikutano
ya Bunge la Afrika Mashariki. Katika Mikutano hiyo, Bunge la Tatu la Afrika Mashariki lilipitisha Miswada minne ya Sheria.
Miswada hiyo itawasilishwa kwa Wakuu wa Nchi Wanachama kwa hatua stahiki.
Miswada hiyo ni:-
i.
Muswada
wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Kukabiliana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu
katika Jumuiya wa mwaka 2016;
ii.
Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa
Malipo/Maslahi kwa Viongozi Maalum wa Viungo/Taasisi za Jumuiya wa mwaka 2015;
iii.
Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Utawala wa
Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; na
iv.
Muswada wa Sheria
wa Afrika Mashariki wa Usawa wa Kijinsia wa mwaka 2016.
B. Ushirikiano wa Kimataifa
Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo
Endelevu
179. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka jana,
nililifahamisha Bunge lako Tukufu kuhusu Umoja wa Mataifa kupitisha Ajenda ya
mwaka 2030 iliyobeba Malengo ya Maendeleo Endelevu. Utekelezaji wa malengo hayo
Kimataifa ulianza rasmi mwezi Januari 2016 na yatafanyiwa tathmini kila baada
ya miaka mitano na hatimaye tathmini ya mwisho mwaka 2030.
180. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017,Wizara
yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini imeendelea
kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya Serikali kuhusu Malengo ya
Maendeleo Endelevu. Lengo ni kuhakikisha kuwa umma na makundi yote kwenye jamii
yanafahamu nafasi yao kwenye utekelezaji wa Malengo hayo. Hadi sasa Wizara
yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa
nchini tumeweza kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikoa ya Mbeya, Kagera,
Kilimanjaro, Kigoma, Dar es Salaam na Dodoma. Aidha, elimu hiyo pia ilitolewa
Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja. Zoezi hili ni endelevu kwa nchi
nzima, hivyo litaendelea kufanyika ili kuhakikisha kila mdau anashiriki
ipasavyo katika kutimiza malengo ya ajenda hii. Kwa upande wa Bunge, kama
ambavyo tuliwahi kutoa elimu kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa mchakato wa
kuundwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu mwezi Machi 2015, Wizara yangu kwa
kushirikiana na wadau wengine muhimu tutaendelea kutoa elimu kwa Wabunge kadri
itakavyohitajika ili kufanikisha utekelezaji wake.
181. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za
Serikali imeendelea kuratibu na kushiriki katika Mikutano mbalimbali ya
Kimataifa kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya
pamoja na nchi na wadau wengine juu ya namna bora ya kushirikiana katika
kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu. Baadhi ya Mikutano hiyo ni:- Jukwaa
la Kisiasa la Ngazi za Juu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu lililofanyika
New York, Marekani mwezi Julai 2016; Mkutano wa Ngazi ya Juu wa “Global Partnership for Effective Development
Cooperation – GPEDC” uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba hadi Desemba
2016; Mkutano wa Kimataifa kuhusu Usafiri Endelevu uliofanyika Ashgabat, Turkmenistan mwezi Novemba, 2016.
Mikutano mingine ni Mkutano
wa Shirika la Posta Duniani uliofanyika Istanbul, Uturuki mwezi Septemba hadi
Oktoba 2016; Mkutano wa Tatu wa
Shirika la Makazi Duniani uliofanyika Quito, Equador mwezi Oktoba 2016; Mkutano wa
Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa kuhusu Uendeshaji wa Shughuli
za Kimaendeleo uliofanyika New York,
Marekani mwezi Februari hadi Machi 2017; na Mkutano wa 61 wa Umoja wa Mataifa wa Kamisheni ya
Hali ya Wanawake Duniani uliofanyika New York, Marekani mwezi Machi 2017.
182. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na
mikutano hiyo ambayo imetoa fursa kwetu kusimamia kikamilifu maslahi mapana ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii.
183. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji
wa Mpango wa Pili wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ambao unatekelezwa
kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwezi Juni 2021. Katika kipindi cha utekelezaji
wa mpango huo, Tanzania itafaidika na miradi yenye thamani ya jumla ya Dola za
Marekani bilioni 1.3 ambapo asilimia 8 ya fedha hizo zitatumika kwa miradi ya
Zanzibar. Utekelezaji wa mpango huo unawiana na vipaumbele vilivyoainishwa
katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 - 2021); na Mpango wa
Pili wa Kupunguza Umaskini Zanzibar wa mwaka 2016 – 2021; Ajenda ya Afrika ya
2063; na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030.
Kikao cha 71 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
184. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Kikao cha 71
cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika New York, Marekani kuanzia
mwezi Septemba hadi Desemba 2016. Tanzania ilitumia Kikao hicho kueleza
misimamo yake kwenye masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa Saharawi Magharibi;
kuwa na Taifa la Palestina sambamba na Israel salama; na kukabiliana na
mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, kupitia kikao hicho tuliijulisha Jumuiya ya
Kimataifa juu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
katika kutatua migogoro ya kisiasa inayozikabili nchi jirani; kupambana na
ugaidi pamoja na dawa za kulevya. Vilevile, tulitoa taarifa kuhusu jitihada
mbalimbali zinazofanywa katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili nchi,
Bara la Afrika na dunia kwa ujumla katika kutokomeza umaskini; kupambana na
rushwa; na dawa za kulevya. Aidha, Tanzania ilisisitiza kuendelea kusimamia usawa
wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kama sehemu ya mkakati endelevu wa
kuheshimu na kulinda haki za binadamu kwa ujumla pamoja na haki za watoto na
walemavu.
185. Mheshimiwa Spika, wakati wa Kikao hicho, pia ulifanyika Mkutano
maalum kuhusu masuala ya Wakimbizi na Wahamaji uliolenga kutafuta namna bora ya
kukabiliana na tatizo hilo. Tanzania ilitumia fursa hiyo kuieleza dunia
changamoto zinazolikabili Taifa katika kuhifadhi wakimbizi na kuzishukuru nchi
marafiki na mashirika ya kimataifa kwa ushirikiano katika kusaidia kutunza
wakimbizi waliopo nchini. Pamoja na kwamba Tanzania inao wajibu wa kutunza wakimbizi kama mshirika wa mikataba
ya kimataifa na sera za wakimbizi, tulitumia Mkutano huo kuitaka Jumuiya ya
Kimataifa nayo kuwajibika zaidi katika suala hili kwa kuendelea kushirikiana na
nchi yetu pamoja na nchi nyingine za Afrika katika kuhudumia wakimbizi na jamii
za Watanzania zinazozunguka kambi za wakimbizi. Kwa mara nyingine, Tanzania
iliihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa itaendelea kuheshimu mikataba ya
kimataifa na kikanda inayoipa nchi yetu wajibu wa kupokea na kuhifadhi
wakimbizi.
186. Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kutumia fursa hii kuzishukuru kwa
dhati nchi marafiki na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa kwa kuendelea kutuunga
mkono katika kuhifadhi wakimbizi. Nchi kama Marekani, Canada, Australia na
Norway zimekuwa zikipokea wakimbizi wanaohifadhiwa nchini kwa ajili ya kuwapa
uraia kwenye nchi zao kama njia mojawapo ya kuwasaidia wakimbizi, hivyo
kusaidia kupunguza gharama za kuwahifadhi wakimbizi hao. Kwa sasa programu ya
kuhamisha wakimbizi 50,000 wenye uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kupatiwa uraia wa nchi hiyo kwa kipindi cha
miaka kumi kuanzia mwaka 2015 hadi 2025 inaendelea vizuri.
Ushiriki kwenye
Operesheni za Kulinda Amani Duniani
187. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na
kufuatilia ushiriki wa Tanzania kwenye Operesheni za Kulinda Amani. Hadi sasa,
Tanzania ina jumla ya walinda amani 2,279 kwenye Misheni sita za Umoja wa
Mataifa ambazo ni: MONUSCO, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; UNAMID, Darfur;
UNIFIL, Lebanon; UNMISS, Sudan Kusini; UNISFA, Abyei; na MINUSCA, Jamhuri ya
Afrika ya Kati.
188. Mheshimiwa Spika, katika ushiriki wetu kwenye operesheni hizi, Tanzania
imeendelea kuaminika na kuheshimika katika Jumuiya ya Kimataifa. Kutokana na
sifa hii, Watanzania wenye ujuzi waliteuliwa kwenye Kamandi za juu kwenye
Misheni mbalimbali zikiwemo MONUSCO – FIB katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo na UNAMID ya Darfur, Sudan. Ushiriki huo umezidi kuwajengea Wanajeshi
wetu uzoefu katika medani za kimataifa na kuongeza maarifa na mbinu mbalimbali
za kijeshi ikiwemo kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa vya kijeshi.
189. Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuuhakikishia uongozi wa Umoja wa Mataifa kuwa, Tanzania
itaendelea kuhakikisha kuwa askari wetu wanaheshimu sheria, kanuni, taratibu na
maadili ya kulinda amani katika misheni hizo.
190.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Wizara iliratibu na kufuatilia ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya
kuhifadhi masalia na kumbukumbu za kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda katika
eneo la Laki Laki, Arusha. Kwa kutambua umuhimu wa suala hili, Serikali
imechangia eneo lenye ukubwa wa ekari 16 kwa ajili ya shughuli za ujenzi na
eneo la ekari tano kati ya hizo tayari limejengwa majengo matatu ambayo ni
Jengo la Mahakama; Jengo la Kuhifadhi Kumbukumbu, Maktaba, Kantini; na Jengo la
Utawala.
191.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa Mataifa umechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 8.8 ambazo
zimetumika kugharamia ujenzi wa majengo hayo ambayo mojawapo linaongoza Afrika
Mashariki na Kati kwa kuwa na Maktaba kubwa na ya kisasa kuhusu masuala ya
sheria hususan sheria za kimataifa kuhusu uhalifu. Napenda kutumia nafasi hii
kuwakaribisha Wanazuoni kutoka ndani na nje ya nchi kutumia rasilimali
zinazopatikana kwenye Maktaba hiyo ili kujijengea uwezo na kuelimisha umma juu
ya athari za matukio ya uhalifu kupitia tasnia hii ya sheria. Idara za Sheria,
Mahakama na Vitivo vya Sheria Vyuo Vikuu mnakaribishwa kutumia maktaba hii kwa
shughuli mbalimbali hasa tafiti.
192. Mheshimiwa Spika, nafurahi kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa,
majengo hayo ambayo yalizinduliwa rasmi na Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi
Novemba 2016, yalijengwa na Wakandarasi wa Tanzania baada ya kushindanishwa na
Kampuni nyingine za Kimataifa.
193. Mheshimiwa Spika, katika hatua
nyingine, Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Kisiasa,
Ulinzi na Usalama ilipewa jukumu la kuwasilisha ombi maalum kwenye Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa kuhusu kuiongezea muda Misheni ya Kulinda Amani Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ijulikanayo kama MONUSCO - FIB. Maamuzi haya yalifikiwa
kwa kuzingatia umuhimu wa vikosi hivyo katika kulinda amani na usalama nchini
humo na kwa kuzingatia hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, inayochangiwa na kuongezeka kwa vikundi vya uasi pamoja
na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2017.
194. Mheshimiwa Spika, nilipewa
jukumu na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuongoza Ujumbe Maalum wa Tanzania kuwasilisha ombi hilo
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hivyo, tarehe 28 Machi 2017,
niliwasilisha ombi hilo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, New York,
Marekani. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tarehe 31 Machi 2017,
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha kwa kauli moja Azimio la
kukiongezea muda kikosi cha kulinda Amani cha MONUSCO-FIB. Kwa namna ya kipekee
kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kuzishukuru nchi wanachama wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na nchi
wanachama wa SADC kwa ujumla wake kwa imani walioionesha kwa Tanzania kwa kuipa
jukumu la kusimamia suala hili na kusaidia kulifanikisha.
195. Mheshimiwa Spika, kufanikiwa
kwa suala hili, sio tu Tanzania inakuwa imetekeleza majukumu yake kama
Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Kisiasa, Ulinzi na Usalama, bali
pia inatekeleza moja ya nguzo za Sera yake ya Mambo ya Nje inayosisitiza
ujirani mwema
196. Mheshimiwa Spika, kuongezewa
muda kwa vikosi vya MONUSCO-FIB ni hatua muhimu kwa kuwa inatoa nafasi ya
kutafuta suluhu ya hali ya kisiasa ili kurejesha amani na usalama katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha, kuwepo kwa amani na usalama katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutaongeza fursa za biashara na faida nyingine
za kiuchumi na kijamii baina ya nchi hiyo na nchi za SADC na Maziwa Makuu,
hivyo kuinua uchumi wa ukanda huu na ule wa nchi moja moja.
Misaada na Mikopo kutoka Mashirika ya
Kimataifa
197. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi
yetu na mashirika ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kuendelea kunufaika na
ushauri wao na mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali
ya maendeleo, kipaumbele kikiwa katika miradi mikubwa ya miundombinu ya
barabara, reli, nishati na maji.
198. Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha,Viongozi mbalimbali wa
mashirika ya fedha walifanya ziara za kikazi hapa nchini. Viongozi hao ni Mhe.
Dkt. Frannie Léautier, aliyekuwa Makamu wa Rais Mwandamizi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika; na Bw. Amadou Hott, Makamu wa Rais wa Benki hiyo
anayeshughulikia masuala ya nishati. Viongozi hao walifanya mazungumzo na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na viongozi wengine wa Serikali kuhusu namna ya kusaidia
kuendeleza Miundombinu ya barabara, reli na nishati. Ziara hizo zilifuatiwa na ziara ya
Wakurugenzi nane (8) wa Idara mbalimbali za Benki hiyo waliyoifanya hapa nchini
mwezi Februari hadi Machi 2017 kwa lengo la kujadiliana kwa kina na Serikali
namna bora ya kutekeleza maboresho ya sekta ya miundombinu na nishati. Miongoni
mwa miradi ambayo ilijadiliwa ni ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme Malagarasi
na Kakonko huko Kigoma; pamoja na njia ya kusafirisha umeme kuunganisha Ukanda
wa Kaskazini Magharibi kwenye Gridi ya Taifa.
199. Mheshimiwa Spika, Wakurugenzi
hao pia, walifanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na kufanya tathmini ya
miradi ya ujenzi wa barabara za Mahonda – Mkokotoni (Kilomita 31);
Fuoni-Kombeni (Kilomita 8.6); Pale – Kiongele (Kilomita 4.6); na Matemwe –
Muyuni (Kilomita 7.6) zinazofadhiliwa na benki hiyo.
200. Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2017, Mhe. Dkt. Jim Yong Kim, Rais wa
Benki ya Dunia alifanya ziara ya kikazi nchini, ambapo pamoja na mambo mengine,
alifanya mazungumzo na Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushiriki katika kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma
katika eneo la Ubungo. Wakati wa uzinduzi wa mradi huo, mikataba mikubwa mitatu
(3) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 780 ilisainiwa kati ya Benki ya
Dunia na Serikali. Kiongozi huyo pia, aliahidi kuendelea kuisaidia Tanzania
kupata mikopo ya riba nafuu kwenye sekta mbalimbali. Mikopo hiyo inatarajiwa
kufikia kiasi cha Dola za Marekani kati ya bilioni tatu (3) na nne (4) katika kipindi
cha miaka mitatu ijayo. Ujio wa viongozi hao wa ngazi za juu wa mashirika ya
fedha ni ishara ya ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na Mashirika hayo na
pia ni ishara ya kukubalika kwa sera za kiuchumi zinazosimamiwa na Serikali ya
Awamu ya Tano. Hivyo, kuimarika kwa ushirikiano huo kunatuhakikishia kuendelea
kupata fedha za kuendeleza miundombinu ambayo ni kichocheo kikubwa cha ustawi
wa sekta nyingine za kiuchumi kama vile kilimo na biashara na hatimaye kusukuma
azma ya kukuza viwanda na kuongeza ajira.
201. Mheshimiwa Spika, pamoja na kudumisha ushirikiano na mashirika ya
fedha, Wizara yangu imeendelea pia kushirikiana na Umoja wa Mataifa na
mashirika mengine ya kimataifa yanayolenga kuboresha huduma za kijamii. Katika
mwaka huu wa fedha, Viongozi Wakuu wa Umoja wa Mataifa na Mashirika yake
walitembelea Tanzania. Viongozi hao ni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la
Idadi ya Watu; Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira; na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Wahamaji. Kwa ujumla ziara hizo zilitoa nafasi kwa Tanzania kujadiliana
na Viongozi hao namna wanavyoweza kuisaidia nchi kuendeleza na kuboresha utoaji
wa huduma katika sekta za Afya, Mazingira na Uhamaji. Mfano, Shirika la Umoja
wa Mataifa la Idadi ya Watu limeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya jumla
ya Dola za Marekani 831,000 unaojumuisha magari manne (4) ya wagonjwa, magari
mawili (2) ya huduma na vifaa tiba
202. Mheshimiwa Spika, vilevile, kufuatia ombi la Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa akiwa njiani kuelekea New York, Marekani, alipita kwa muda
mfupi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
tarehe 9 Machi 2017 na nilifanya naye mazungumzo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais.
203. Mheshimiwa Spika, Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliipongeza Tanzania kwa uwezo wake wa kutekeleza kanuni za utawala bora
ndani ya nchi na pia kudumisha amani Barani Afrika hususan katika Ukanda wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Mheshimiwa Guterres alimpongeza Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa kwa jitihada zao katika kutatua migogoro ya kisiasa
katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha, alipongeza
juhudi za Tanzania za kuendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka nchi hizo. Tanzania ingependa
kuona hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo katika nchi zinazotuzunguka
ili kuzuia kuongezeka kwa wakimbizi.
Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa
Paris
204.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 22 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa
Mabadiliko ya Tabianchi (COP 22) uliofanyika Marrakech, Morocco, mwezi Novemba
2016. Mkutano huo ulikuwa ni wa kwanza tangu kupitishwa kwa Makubaliano ya
Paris mwezi Desemba 2015 na ulijikita katika kujadili utekelezaji wa
Makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwezi Novemba 2016. Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi
zinazoathirika na mabadiliko ya tabianchi, imesaini Makubaliano hayo yanayoweka
mikakati ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzijengea nchi
uwezo wa kukabiliana na athari hizo. Kwa sasa, Tanzania ipo katika hatua za
maandalizi ya kuridhia Makubaliano hayo.
205.
Mheshimiwa Spika, pamoja na masuala mengine, Mkutano wa COP 22 ulijadili
umuhimu wa mifuko ya kimataifa inayofadhili miradi ya uhifadhi wa mazingira na
ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika kutekeleza Makubaliano ya Paris.
Mifuko hiyo ambayo Tanzania imekuwa ikinufaika nayo ni pamoja na Green Climate Fund (GCF), Global Environment
Facility (GEF), Adaptation Fund (AF) na Least
Developed Countries Fund (LDCF). Tunaishukuru Mifuko hii kwa misaada
inayotoa kwa Tanzania, na tunazishukuru nchi zinazochangia fedha kwenye Mifuko
hii. Tunaendelea kutoa wito kwa nchi zilizoendelea kuendelea kuongeza michango
kwenye mifuko hiyo ili nchi maskini ambazo hazijasababisha tatizo hili ziweze
kutekeleza mipango na miradi ya kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko
hayo.
206.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira, inaendelea kuhamasisha sekta ya umma na sekta binafsi kufuatilia kwa
karibu ufadhili unaotolewa na mifuko hiyo kwenye miradi ya kupambana na
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uhifadhi wa mazingira ili kuiokoa
nchi na rasilimali zake na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
207.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania itaendelea kushirikiana na vyombo vya kimataifa
hususan vile vya Umoja wa Mataifa katika kulinda mazingira ya wanyamapori na
misitu kwa ajili ya utalii hususan matumizi endelevu ya maji ya Mto Ruaha na
Mto Mara.
Mfuko wa Dunia wa Masuala ya Afya
208. Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilishiriki kwenye Mkutano wa Tano wa
Mfuko wa Dunia wa Masuala ya Afya ujulikanao kama Global Fund uliofanyika Montreal, Canada mwezi Septemba 2016. Lengo
la Mkutano huo lilikuwa ni kuhamasisha nchi zilizoendelea na mashirika
mbalimbali ya kimataifa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 13 kwa
ajili ya kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu katika nchi
zinazoendelea. Mkutano huo, ulifanikiwa kuchangisha kiasi cha
Dola za Marekani bilioni 12.9, fedha ambazo zitatumika kusaidia nchi
nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kupambana na magonjwa hayo katika
kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.
209. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuzishukuru nchi na
mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa kuchangia mfuko huo ili kuzisaidia nchi
zinazoendelea kupambana na magonjwa hayo. Aidha, napenda kutoa wito kwa nchi na
mashirika mengine kuiga mfano huo. Nichukue nafasi hii tena kuishukuru Serikali
na watu wa Marekani kwa msaada wa hivi karibuni kwa Tanzania wa Dola za
Marekani milioni 526 kwa ajili ya kuendelea kupambana na maambukizi ya virusi
vya UKIMWI.
KURATIBU NA KUSIMAMIA MASUALA YA WATANZANIA WAISHIO
UGHAIBUNI
210. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza azma ya Serikali ya
kuwahamasisha na kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni katika kuchangia
maendeleo nchini. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliandaa Kongamano la Tatu la Diaspora
lililofanyika Zanzibar mwezi Agosti 2016, ambapo Diaspora kutoka zaidi ya nchi
20 duniani walishiriki. Makongamano hayo yamekuwa yakileta hamasa kubwa kwa
Diaspora kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo nchini kupitia uwekezaji
katika sekta za elimu, afya, miundombinu, uchukuzi, utalii, nishati na madini.
Vilevile, Wizara iliratibu ushiriki wa Taasisi za Umma na Binafsi kwenye
Kongamano la kuadhimisha Siku ya Tanzania yenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji
kwenye sekta ya maliasili na utalii, lililofanyika Texas, Marekani mwezi Mei
2017.
211. Mheshimiwa Spika, Wizara pia
imeendelea kukusanya na kutunza kumbukumbu za Watanzania wanaoishi ughaibuni na
kuwahimiza kusajili Jumuiya zao katika Ofisi za Balozi zilizo karibu nao.
Usajili huo utaiwezesha Serikali kukamilisha kanzidata itakayopatikana katika
Tovuti maalum ya Diaspora, ili taarifa za Diaspora zenye kuonesha takwimu
sahihi za idadi yao, elimu, ujuzi na maarifa waliyonayo zisaidie Serikali
kuwashirikisha kikamilifu katika kuleta maendeleo nchini.
212.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
imeendelea kutoa elimu kwa Watanzania
waishio ughaibuni ili kuhakikisha wanazitambua haki na fursa zilizopo. Tunawakumbusha
kila mara kuendelea kuijengea taswira nzuri nchi yetu kwa kuishi na kufuata
sheria za nchi husika, tunawapa taarifa za fursa zilizopo kwa sasa ndani ya nchi
yetu, changamoto na mafanikio pamoja na kuhamasisha
uwekezaji. Halikadhalika, tunasikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa
kushirikiana na Serikali za nchi walizopo pamoja na Wizara za sekta husika.
213.
Mheshimiwa Spika, mathalan katika
eneo la umiliki ardhi, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi ilitoa ufafanuzi kupitia Ofisi za Balozi zetu na maeneo
ya uwakilishi kuhusiana na umiliki wa ardhi. Walifahamishwa kuwa, kulingana na
Sheria ya uraia namba 6 ya mwaka 1995 na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999,
Mtanzania ambaye ameukana uraia wake anapoteza hadhi ya kuwa raia wa Tanzania
na hivyo hataruhusiwa kumiliki ardhi nchini. Hata hivyo, kupitia Taasisi ya
Uwekezaji, Watanzania hao bado wana fursa ya kuwekeza nchini kulingana na
sheria na miongozo ya uwekezaji iliyopo nchini.
KUSIMAMIA UTAWALA NA MAENDELEO YA UTUMISHI
WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU
Uwezo uliopo katika Wizara
214. Mheshimiwa Spika, Wizara ina jumla ya watumishi
487ambapo watumishi 107 wapo kwenye Balozi zetu na watumishi 380 wapo Makao
Makuu.
Mafunzo
215. Mheshimiwa Spika, katika
kuendelea kuwajengea uwezo watumishi waliopo, Wizara kwa kushirikiana na
wafadhili imeendelea kugharamia mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi ndani na
nje ya nchi. Katika kipindi hiki, watumishi 77 walihudhuria mafunzo ya muda
mfupi na watumishi 14 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu katika shahada ya
Umahiri.
Uteuzi
216. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha
kuwa nchi yetu inakuwa na uwakilishi nje, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Mabalozi
ili kujaza nafasi zilizo wazi katika vituo vya Beijing, Paris, Brussels,
Muscat, Rome, New Delhi, Pretoria, Nairobi, Brasilia, Maputo, Kinshasa,
Kampala, Abuja, Moroni na Geneva. Aidha, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa
Mabalozi wa vituo vipya katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan,
Qatar na Uturuki.
KURATIBU NA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO NA TAASISI ZILIZO CHINI YA
WIZARA
Miradi ya Maendeleo ya Wizara
217.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara iliidhinishiwa
bajeti ya maendeleo kiasi cha Shillingi bilioni 8. Miradi iliyopangwa
kutekelezwa ni ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara ambalo ni sehemu ya Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kiasi cha Shilingi bilioni 2.3; kukamilisha ukarabati jengo la
ghorofa tisa litakalotumika kwa ajili ya ofisi na makazi katika Ubalozi wa
Tanzania Maputo, Msumbiji kiasi cha Shilingi bilioni 1.3; kukarabati makazi ya Balozi na
watumishi yaliyopo Stockholm, Sweden kiasi cha Shilingi bilioni 2.2; kukarabati majengo mawili
yanayomilikiwa na Serikali yaliyopo Khartoum, Sudan kiasi cha Shilingi bilioni
1.8; na kuboresha mfumo wa mawasiliano
kati ya Wizara na Balozi za Tanzania nje kiasi cha Shilingi milioni 321.5.
218. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia
mwezi Mei 2017, Wizara imepokea Shilingi bilioni 3.4 za bajeti ya maendeleo
sawa na asilimia 43.6. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi bilioni 2.1 ni kwa
ajili ya kukarabati makazi ya Balozi na watumishi yaliyopo Stockholm, Sweden na Shilingi
bilioni 1.3 zimetumika kwa ajili ya kumlipa mkandarasi anayekamilisha kazi ya
ukarabati wa jengo la Ofisi na makazi lililopo Maputo, Msumbiji. Wizara
inaendelea kufuatilia fedha za maendeleo ziliozosalia ili kuweza
kutekeleza miradi iliyopangwa.
219. Mheshimiwa
Spika, kuna taasisi
tatu ambazo Wizara yangu ina jukumu la kuzisimamia ambazo ni Chuo cha
Diplomasia kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha,
ambacho pia kinasimamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
kilichopo Dar es Salaam. Naomba nichukue fursa hii kutoa taarifa ya taasisi
hizo kama ifuatavyo:-
Chuo
cha Diplomasia
220. Mheshimiwa
Spika, baada ya
kupata ithibati na kutambuliwa rasmi na Baraza la Ithibati la Elimu ya Ufundi,
Chuo sasa kimejikita katika kutoa Programu za Diplomasia ya Uchumi ili kwenda sambamba
na Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa
nchi ya uchumi wa viwanda. Aidha, Chuo kimeanza kutoa kozi za muda mfupi na
muda mrefu za utatuzi wa migogoro.
221. Mheshimiwa
Spika, katika
kutekeleza mipango na malengo yake ya kujiimarisha na kujitanua ili kukipa
uwezo na kujitegemea, Chuo kilijikita katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka
Mitano 2012/2013 – 2016/2017. Kipaumbele cha Mpango Mkakati huo ni kuboresha
miundombinu ya Chuo ili kwenda sambamba na utekelezaji wa matakwa ya Baraza la
Ithibati la Elimu ya Ufundi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Chuo hakikupewa
fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo lakini Wizara kwa kutambua
hilo ilitumia mahusiano mazuri yaliyopo kati yake na wadau mbalimbali kukiwezesha
Chuo hicho kupata misaada ya vitendea kazi. Kupitia juhudi hizo, nchi ya Jamhuri
ya Korea ilikipatia Chuo hicho msaada wa
kompyuta 150. Vilevile, Ubalozi wa Kuwait nchini ulisaidia kufanya ukarabati wa
Maktaba ya Chuo hicho.
222. Mheshimiwa
Spika, ili kuhakikisha
mazingira ya Chuo yanaboreshwa, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara yangu
imetenga fedha za bajeti ya maendeleo kwa ajili ya Chuo ili kuboresha
miundombinu yake. Hatua hiyo itawezesha Chuo kuongeza program, udahili na uwezo
wa kujitegemea.
Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano Arusha
223. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
wa fedha 2016/2017 hadi kufikia Machi 2017 Kituo kimeweza kuwa mwenyeji wa
Mikutano 274 ambayo 54 ni ya kimataifa na 220 ya kitaifa. Aidha, katika kipindi
hicho, Kituo kimefanikiwa kupata mapato kiasi cha Shilingi 10,155,779,694.00 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali
vya mapato. Vilevile, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa, kwa mwaka wa
fedha 2015/2016 Kituo kimeendelea kupata hati safi ya ukaguzi.
224. Mheshimiwa
Spika, katika
kipindi cha mwaka 2017/2018, Kituo kimepanga kuingiza mapato kiasi cha Shilingi 16,920,100,686.00 kutokana na
vyanzo vyake mbalimbali. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere kinategemewa kuingiza kiasi cha Shilingi 4,047,100,000.00.
225. Mheshimiwa
Spika, ili kuongeza
wigo wa utoaji huduma, AICC inategemea kukopa kiasi cha Shilingi bilioni 2.12 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa upanuzi wa
Hospitali ya AICC baada ya kupata kibali cha Wizara ya Fedha na Mipango. Kituo
pia kinaendelea kufanya taratibu za kuwezesha kujengwa Kituo mahsusi cha
mikutano kitakachoitwa Mt. Kilimanjaro
International Convention Centre (MK-ICC). Kituo hicho ndicho kitakuwa
suluhisho sahihi la mahitaji ya mikutano ya kimataifa na maonesho hapa nchini.
Vilevile, Kituo kinaendelea na mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa
Kituo cha mikutano Dodoma.
226. Mheshimiwa
Spika, baada ya
Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (UN-ICTR)
kufunga shughuli zake na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhamishia baadhi ya
shughuli zake katika jengo lao jipya, kwa sasa Kituo cha AICC kina nafasi ya
kutosha kuweza kupokea taasisi nyingine za Kitaifa na Kimataifa. Hivyo, ninatumia nafasi hii kukaribisha
taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zitakazopenda kuweka makao yao Jijini
Arusha kutumia nafasi hizo za ofisi zilizo wazi.
Mpango
wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika
227. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu
utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande
wa Tanzania (APRM Tanzania) kwa mujibu wa miongozo ya Wakuu wa Nchi na Serikali
wa Afrika kama ifuatavyo:
i.
Kushiriki
katika Mkutano wa Bunge la Afrika uliojadili Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Barani Afrika uliofanyika Sharm el Sheikh, Misri mwezi Oktoba
2016. Katika Mkutano huo, Wajumbe
walieleza kuridhishwa kwao na hatua zilizofikiwa na Tanzania katika kudumisha
amani na utulivu, kulinda haki za binadamu, kudumisha Muungano, maendeleo ya
kiuchumi, matumizi ya lugha moja ya Kiswahili na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.
APRM Tanzania pia ilipata fursa ya kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali
katika kutatua changamoto mbalimbali zilizobainishwa kwenye ripoti hiyo;
ii.
Kusimamia
utekelezaji wa mpango wa kuondoa changamoto za utawala bora zinazoihusu nchi
yetu zilizobainishwa kwenye Ripoti ya APRM. Mkazo umewekwa katika kukamilisha
ripoti ya utekelezaji wa mpango huo kwa upande wa Zanzibar ili kupata ripoti
moja ya nchi itakayowasilishwa kwenye Kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Afrika;
iii.
Kushiriki
katika Mkutano wa kutafuta Wajumbe Wapya wa Jopo la Watu Mashuhuri la Mpango wa
Afrika wa Kujitathmini katika Utawala Bora uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini
mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Balozi Ombeni Yohana Sefue,
Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu alichaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo
hilo. Wajumbe wengine waliochaguliwa
wanatoka katika nchi za Algeria, Misri, Nigeria na Msumbiji;
iv.
Kutoa
taarifa kwa wananchi kuhusu matokeo ya
tathmini ya utawala bora kwa nchi yetu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na
pia kwa kutumia majukwaa mengineyo; na
v.
Kuisaidia
Serikali kuimarisha Mfumo wa Kujitathmini Kiutawala Bora.
CHANGAMOTO
ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA
FEDHA 2016/2017 NA NAMNA YA KUZIPATIA UFUMBUZI
228.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na kuwepo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha
2016/17, zipo changamoto mbalimbali ambazo Wizara imekabiliana nazo wakati wa
kutekeleza majukumu yake. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kutumia fedha
nyingi za bajeti kugharamia pango kwa ajili ya ofisi na makazi balozini; Kasi ndogo
ya ubadilishaji wa Sheria za nchi ili kuendana na matakwa ya Itifaki ya Soko la
Pamoja la Afrika Mashariki; Kasi ndogo ya sekta binafsi kutumia fursa za
biashara na uwekezaji zitokanazo na Mtangamano wa Afrika Mashariki na masoko ya
kimataifa; na uelewa mdogo wa Watanzania kuhusu masuala ya Mtangamano.
229. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto
hizi Wizara inaendelea kutekeleza mpango
wake wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi Balozini kwa
kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazotolewa na Serikali na kwa
kushirikisha Mifuko ya Uwekezaji iliyopo nchini katika kutekeleza baadhi ya
miradi yake ya maendeleo; kuruhusu kasi ya ubadilishaji sheria za nchi ili ziendane
na matakwa ya Itifaki ya Soko la Pamoja; na kuzihimiza Taasisi za Serikali
kutoa kipaumbele na kuongeza kasi ya ubadilishaji wa sheria zilizoainishwa ili
kuwawezesha Watanzania kunufaika ipasavyo na fursa za Soko la Pamoja la Afrika
Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda.
230. Mheshimiwa
Spika,kwa kutambua umuhimu wa kipekee wa
kutoa elimu kwa Umma wa Watanzania juu
ya fursa zinazotokana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania ni
mwanachama, Wizara imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali za fursa zinazopatikana
nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa muktadha huu,Wizara imeendelea kutumia vyombo vya
habari vya umma, binafsi na vya kimataifa kama vile TBC1, Capital, Clouds, Radio One, BBC, CGTN, VoA, RFI, DW na
Bloomberg kutoa Elimu kwa Umma kuhusu fursa zinazotokana na Jumuiya za Kikanda
na Kimataifa. Aidha, Wizara imeendelea pia kutumia machapisho, Tovuti yake na
Mitandao ya kijamii kama vile Tweeter na Blog ili kuweza kuwafikia wadau wengi
zaidi.
231.
Mheshimiwa Spika, katika
kuimarisha mawasiliano baina ya Wizara na wadau wake, Wizara ilianzisha
utaratibu wa kuzungumza na Waandishi wa Habari kila wiki. Malengo ya mikutano hii ni kuueleza umma masuala
mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara ikiwemo maazimio yanayofikiwa kwenye
mikutano mbalimbali ya kimataifa na kikanda, ziara za viongozi wanaotembelea
nchini na pia kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Wizara. Jumla ya
mikutano 70 kati ya Wizara na Waandishi wa Habari kutoka vyombo vyote vya
habari ilifanyika ndani ya mwaka huu wa fedha.
232. Mheshimiwa Spika, ni matumaini yangu kuwa juhudi hizi zitapanua uelewa wa
Wananchi kuhusu utendaji wa Wizara kwa ujumla pamoja na kuwahamasisha kutumia
fursa zilizopo katika Jumuiya mbalimbali za kikanda na Kimataifa.
MALENGO YA
WIZARA KWA MWAKAWA FEDHA 2017/2018
233.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, pamoja na mambo mengine, Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepanga kutekeleza malengo makuu
muhimu kulingana na majukumu yake kama ifuatavyo:
i.
Kutangaza
mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake
ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
ii.
Kuendelea
kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi
wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa
mipango yetu ya maendeleo;
iii.
Kuendelea
kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia
wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za
kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko;
iv.
Kusimamia,
kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya
nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
v.
Kufuatilia
utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa;
vi.
Kuendelea
kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta
wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;
vii.
Kuendelea
kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo;
viii.
Kuongeza
uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea
kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa
kadri hali ya fedha itakavyoruhusu;
ix.
Kujenga
mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali
vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu;
x.
Kuendelea
kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na
hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya
mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali
zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile
ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi
zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama
msaada;
xi.
Kuendelea
kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia
maendeleo ya taifa;
xii.
Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano
katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya
Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya
Vikundi Kazi na Wataalam;
xiii.
Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na
maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la
Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya
Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xiv.
Kuratibu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea
kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xv.
Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili
kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya
ya Afrika Mashariki;
xvi.
Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha
Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC
pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika;
xvii.
Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji
wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege
na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xviii.
Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha
katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xix.
Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya
Bunge la Afrika Mashariki;
xx.
Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu
ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
kuzingatia mfumo wa Confederation;
xxi.
Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya
kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xxii.
Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba
wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki;
xxiii.
Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya
kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xxiv.
Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xxv.
Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini
ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
xxvi.
Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa
miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark
East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta
binafsi; na
xxvii.
Kukamilisha
kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje.
SHUKRANI
234. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee
naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru Mabalozi, Wawakilishi wa taasisi za Umoja
wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa
kupitia nchi zao katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa
na Serikali ya Awamu ya Tano.
235. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Tano imeendelea kupata mafanikio
makubwa kutokana na mchango wa wadau na washirika wa maendeleo kutoka nchi na
asasi mbalimbali za kitaifa, kikanda, kimataifa pamoja na sekta binafsi. Naomba
nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na
Afrika Kusini, Algeria, Australia, Austria, Brazil, Canada, China, Cuba, Denmark, Finland, Hungary, India, Italia,
Ireland, Israel, Iran, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Malaysia, Marekani, Malta, Misri, Morocco, New Zealand, Norway, Oman, Poland, Qatar, Saudi Arabia, Sweden, Singapore, Thailand, Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi,
Uingereza, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ureno, Urusi, Uswisi na
Uturuki.
236. Mheshimiwa Spika, vilevile, shukrani ziwaendee Umoja wa Ulaya, AfDB, African Capacity Building Facility, Benki ya Dunia, IAEA, IMF, Investment Climate Facility for Africa, UNDP na Mashirika mengine yote ya Umoja wa Mataifa, TradeMark East Africa, The
Association of European Parliamentarians with Africa na WWF pamoja na Mifuko na Mashirika mbalimbali ya Misaada kwa mchango
wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi.
237. Mheshimiwa
Spika, vilevile, tunapenda kutoa shukrani zetu kwa wadau mbalimbali ambao wameendelea kutujengea
uwezo Wizarani ikiwemo kufanikisha uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma.
Tunazishukuru Serikali za Kuwait na Oman kwa msaada wa magari; UNDP kwa vifaa
vya mawasiliano; na Jamhuri ya Korea na Kuwait kwa msaada wa Kompyuta.
Vilevile, Wizara inamshukuru Mheshimiwa Jasem Al-Najem Balozi wa Kuwait nchini,
kwa utayari wake wa kuendelea kutusaidia katika maeneo mengine na Mheshimiwa Dkt.
Lu Younqing Balozi wa China nchini kwa kuahidi kutoa fedha zitakazojenga nyumba
ya Wageni Mashuhuri eneo la Chamwino hapa Dodoma.
MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018
238.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu, kwa mwaka
2017/2018 Wizara imepangiwa bajeti ya kiasi cha Shilingi 150,845,419,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 142,845,419,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00
ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
239.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara kwa
mwaka wa fedha 2017/2018, Shilingi 133,424,290,000.00
ni
kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 9,421,129,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara.
Kati ya fedha za Matumizi Mengineyo Shilingi
410,000,000.00 ni kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora
Tanzania, Shilingi 3,341,148,909.00
ni kwa ajili ya fedha za Mishahara na Matumizi Mengineyo ya Chuo cha Diplomasia
na Shilingi 513,060,356.00 ni kwa
ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
240.
Mheshimiwa Spika, katika fedha za bajeti ya Maendeleo kiasi cha Shillingi 8,000,000,000.00 zilizopangwa
kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Shilingi
1,815,527,215.00 zitatumika kukarabati jengo la ofisi na makazi ya
watumishi, Ubalozi wa Tanzania Kampala; Shilingi
315,425,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Balozi yaliyopo
Kinshasa, DRC; Shilingi 477,293,775.00 ni
kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya Ubalozi na makazi ya watumishi, Ubalozi wa
Tanzania Harare; Shilingi 373,320,000.00
ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya Balozi, ubalozi wa
Tanzania Beijing; Shilingi 534,682,500 ni
kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi, Ubalozi wa
Tanzania Pretoria; Shilingi 593,300,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za
ubalozi zilizopo Ubalozi wa Tanzania
Lilongwe; Shilingi 508,420,000.00
ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi Ubalozi
wa Tanzania Cairo; Shilingi 865,300,200.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya
Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini;
Shilingi 257,006,310.00 ni
kwa ajili ya ukarabati wa jengo la zamani la ofisi ya Ubalozi wa Tanzania
Washington DC, Shilingi 259,725,000.00 ni
kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi, ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Shilingi 195,943,440.00 ni kwa ajili ya
ukarabati wa makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania Brussels; na Shilingi 1,804,056,560.00 ni kwa ajili
ya ujenzi wa jengo la ofisi ya ubalozi, Ubalozi wa Tanzania Muscat.
241. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2017/2018, Wizara inatarajia kukusanya
kiasi cha Shilingi 25,773,882,820.00
ikiwa ni maduhuli ya Serikali.
HITIMISHO
242.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza
kutekeleza kikamilifu majukumu ya Wizara, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, naomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
150,845,419,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi
142,845,419,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
243.
Mheshimiwa Spika, naomba
kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa
kunisikiliza.
244. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.