TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar yazinduliwa rasmi.
Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar zilizinduliwa rams tarehe 19 Mei 2017. Shughuli za ufunguzi ziliongozwa na Mhe. Fatma Mohammed Rajab, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar ambaye alisaini kitabu cha wageni kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Ubalozi.
Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Watanzaia wanaoishi nchi Qatar walishiriki katika hafla hiyo.
Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kuzungumza machache na Watanzania walioshiriki. Aliwaeleza kwamba kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar ni sehemu ya kutekeleza malengo ya Serikali ya Tanzania ya kusogeza huduma zake kwenda kuwekeza Tanzania hususan katika sekta ya viwanda. Aliwahakikishia kwamba Ubalozi utawapatia ushirikiano watakaouhitaji katika kufanikisha azma hiyo.
Balozi aliwapongeza Watanzania hao kwa kuendelea kuwa na sifa nzuri nchini Qatar na kudumisha mshikamano miongoni mwao. Aliwahimiza waendelee kuwa raia wema na kulinda haiba na jina la Tanzania kwa kufuata sheria za nchi wanapoishi. Alisema milango ya Ubalozi itakuwa wazi kupokea ushauri wao katika mambo ambayo yatalenga kuleta tija na mafanikio kwa taifa.
Naye Bw. Said Ahmed, Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Qatar aliishukuru Serikali kwa kusikia kilio chao na hatimaye kufungua Ubalozi na kuwa na Balozi Mkazi nchini Qatar. Alimueleza Balozi kwamba jamii ya Watanzania wanaoishi Qatar itashirikiana na Ofisi za Ubalozi na kufanya kazi bega kwa bega katika kuitafutia maslahi Tanzania. Wawakilishi hao waliomba Ubalozi uandae mkutano mkubwa utakaowawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki ili kusikia maoni yao na changamoto zinazowakabili. Balozi aliahidi kufanya mkutano huo mapema iwezekanavyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Doha, Qatar 24 Mei, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.