TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri
wa Mambo ya Nje wa Norway kuzuru Tanzania
Waziri wa Mambo ya
Nje wa Ufalme wa Norway, Mhe. Borge Brende atafanya ziara ya kikazi ya siku
mbili nchini tarehe 29 na 30 Juni 2017. Madhumuni ya ziara ya Mhe. Brende
ambaye atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe
29 saa tatu usiku ni kuimarisha mahusiano kati ya Norway na Tanzania.
Wakati wa ziara yake,
Mhe. Waziri Brende pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu
jijini Dar es Salaam tarehe 30 Juni 2017.
Aidha, siku hiyo hiyo
asubuhi, mgeni huyo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga (Mb.) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere na
baadaye wataweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu Ushirikiano wa
Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Mhe. Borge pia
atakutana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango (Mb.) ambapo kwa
pamoja watashiriki katika uzinduzi wa programu ya kushirikiana katika masuala
ya kodi na uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kuendeleza mafuta(oil for
development program) utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro
tarehe 30 Juni 2017. Uzinduzi wa
programu hizo pia utahudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani (Mb.) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt.
Charles Kichere.
Ratiba ya ziara ya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway inaonesha pia kwa kushirikiana na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb.) na Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani watashiriki katika shughuli za kufunga
semina ya Mradi wa Kusindika Gesi asilia (LNG) iliyoandaliwa na kampuni ya
mafuta ya kutoka Norway inayoitwa Statoil ambayo pia inaendesha shughuli zake
hapa nchini. Semina hiyo inafanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar
es Salaam.
Mhe. Waziri baada ya
kukamilisha ratiba yake nchini atarejea Norway siku ya Ijumaa tarehe 30 Juni
2017 saa nne usiku.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29 Juni 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.