Kikundi cha ngoma kutoka nchini Oman ambacho ni sehemu ya ujumbe wa Mfalme wa Oman uliopo nchini kwa ziara kikitumbuiza jukwaani. |
Mhe. Dkt. Kigwangalla na Mhe. Dkt.Mohammed wakijadiliana jambo. |
Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima akifuatilia buruduni iliyokuwa ikitolewa na kikundi cha ngoma kutoka Oman. Wengine ni sehemu ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Oman. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Oman ikifuatilia burudani. |
Bendi ya Jeshi kutoka nchini Oman ambayo pia ni sehemu ya ujumbe huo ilitoa burudani kwa wananchi waliohudhuria hafla hiyo. |
=======================================================================
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla amewataka Watanzania kuwa
mabalozi wazuri katika kuzitangaza na kuzidumisha mila, tamaduni na desturi zao
kwakua ndio nguzo na utambulisho wa Mtanzania popote Duniani.
Waziri
Kigwangala aliyasema hayo katika sherehe za muziki wa utamaduni wa Oman
zilizofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam tarehe 18
Oktoba 2017.
Sherehe
hizo ambazo Mgeni rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Kigwangalla, ziliandaliwa na ujumbe wa Mfalme wa Oman uliokuja na Meli ya Mfalme huyo nchini kwa ziara ya siku
sita inayotarajiwa kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 21 November 2017.
Mhe.
Kigwangala alisema kupitia tamasha hilo la muziki na ziara nzima kwa ujumla,
Oman inapata fursa ya kujitangaza na kuutumia utamaduni wao kama sehemu ya
utalii na kwamba hii ni nafasi ya pekee kwa Watanzania kujifunza namna gani watu wa mataifa
mengine wameweza kutumia utamaduni wao kwa tija na kuongeza pato la Taifa.
Aidha,
alisisitiza ni wakati sasa makundi yote ya utalii yaliyopo nchini kama utalii wa kwenye maji,
utalii wa misitu hususan kwa kutumia upekee wa mazingira yetu, fukwe na hata
historia ya binadamu vikaendelea kuhifadhiwa na kupatiwa ubunifu zaidi wa namna
ya kuvitangaza na kupata mfumo wa kisasa kwa ajili ya kuwezesha watalii wengi kuingia
na kutoka nchini kwa namna bora zaidi.
Halikadhalika
akaongeza kwa kusema “Nchi yetu imebarikiwa sana kwa kuwa na idadi kubwa ya
vivutio vya utalii ukilinganisha na Oman, katika fursa niliyopata ya kukutana
na Naibu Waziri wa Utalii wa Oman ambaye ameambatana na ujumbe huu nimeweza
kuzungumza naye mengi ambayo tutayaweka katika utekelezaji ili sekta ya utalii
iweze kuongeza fedha za kigeni zaidi.”
Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Bw. Mohammed bin Hamad
Al-Rumhy ameahidi kuwa Serikali ya Oman itaendeleza undugu huo kwa kufanya
biashara na kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuweza
kuingia katika soko la ushindani duniani.
Lengo
kuu la ziara ya ujumbe huo ni kutangaza amani katika ukanda wa Afrika Mashariki
sambamba na kudumisha undugu uliopo baina ya Tanzania na Oman ambapo utamaduni
wa mataifa haya mawili umekuwa ukifanana hususan katika ukanda wa pwani kufuatia
historia na muingiliano wa wananchi wake katika shughuli mbalimbali za kiuchumi
na kijamii.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.