Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, amekutana na kumuaga Balozi
wa Ireland nchini, Mhe. Paul Sherlock ambaye amemaliza muda wake wa utumishi na
amemtakia maisha mema na kumwambia kuwa ni matarajio yake kuwa atakuwa balozi mwema
kwa Tanzania nchini Ireland na kwingineko duniani.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi
ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Prof.
Kabudi amesema kuwa Ireland imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na
Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali
nchini ikiwemo miradi ya maendeleo, elimu, kilimo, afya pamoja na biashara na
uwekezaji.
“Kupitia uhusiano imara kati ya
Tanzania na Ireland hivi karibuni tulivyopatwa na janga la covid 19, Ireland
imetoa msaada wa Euro milioni 1.5 ambapo baadhi ya fedha hizo zilipelekwa Shirika
la Afya Duniani ofisi ya hapa Tanzania na Shirika la Chakula duniani ofisi ya hapa
nchini kwa ajili ya kununua chakula lakini pia kwenda katika mfuko wa Benjamini
Mkapa kwa ajili ya kuajiri wafanyakazi na kujenga vituo vya afya ili kutusaidia
kupambana na Covid 19,” Amesema Prof. Kabudi.
Waziri Kabudi amemhakikishia Balozi Sherlock,
kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ireland utaendelea kuimarika
hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara, na kutoa wito kwa Serikali ya
Ireland kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za kilimo,
viwanda hasa vya nguo pamoja na ujenzi.
Aidha, Balozi Sherlock ameishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa
ikimpatia alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa
ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa
na uhusiano wa kidiplomasia kwa miaka 40.
" Natumaini kuwa serikali ya Ireland
kupitia uhusiano wake na Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Tanzania za kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga
mbele kimaendeleo," amesema Balozi Sherlock.
Tanzania na Ireland zimetimiza miaka
40 ya uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Ireland ilipofungua ubalozi
wake nchini Tanzania mwaka 1979.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi akiongea na Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Paul Sherlock wakati
alipokuwa akimuaga katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi
wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi katika Ofisi ndogo
za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya mlima Kilimanjaro Balozi wa Ireland
nchini, Mhe. Sherlock katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi
wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock akimuonesha moja ya picha katika kitabu alichompatia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi kama zawadi
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidi zawadi ya kitabu cha picha Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.