Tuesday, April 27, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI WA BURUNDI, UINGEREZA NA UMOJA WA ULAYA

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na kupokea nakala ya hati za utambulisho za balozi mteule wa Italia hapa nchini.

Mabalozi hao wamekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Burundi Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Uingereza Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti.

Pamoja na mambo mengine, Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu Biashara na Uwekezaji na Utamaduni.

“Leo nimekutana na mabalozi watatu kutoka Burundi, Uingereza na Umoja wa Ulaya na nimejadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano katika masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji na mahusiano baina yetu na nchi zao,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa “mabalozi wote watatu wameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya nchi zetu………lakini pia tumejadili mipango ya kimkakati kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Uingereza ambapo wangependa kuona inaendelezwa katika awamu hii,” amesema Balozi Mulamula.

Nae Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Abayeho amesema uhusiano wa Burundi na Tanzania ni wa miaka mingi na wamefurahia kuuona uhusiano huo ukiendelea kuboreka zaidi na tunaamini uhusiano huo utaendelea kudumu kwa miaka mingi.

“Uhusiano wa Burundi na Tanzania ni uhusiano wa muda mrefu na tunafurahia kuona unazidi kuimarika. Mbali na masuala ya uhusiano umependekeza utekelezwaji wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa bandari, barabara na reli uharakishwe kwa manufaa ya nchi zote mbili,” Amesema Balozi Abayeho

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar amesema katika kikao chake na Mhe. Waziri wamejadili namna ya kuboresha uhusiano baina ya Uingereza na Tanzania na jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika kudumisha na kuendeleza uhusiano huo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania   na Umoja wa Ulaya ni wa zaidi ya miaka 46 na umekuwa ukinufaisha pande zote mbili hivyo Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inapata manendeleo kijamii na kiuchumi.

Katika tukio jingine, Mhe. Waziri Mulamula amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi.

“Tanzania na Italia tuna uhusiano mzuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii, uwekezaji na elimu na tumejadiliana mambo aliyoagizwa na serikali yake katika kudumisha uhusiano wa Italia na Tanzania.

Kwa Upande wake Balozi Mteule, Mhe. Lombardi amesema Italia na Tanzania zina masuala mengi ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi,kijamii na utamaduni na kwamba yuko nchini kuhakikisha  hayo yote yanatekelezeka kwa maslahi ya nchi zote mbili.

“Tunaamini kupitia maongezi yetu ya leo tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya Italia na Tanzania, lakini pia nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Italia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha mahusiano yake ya kidiplomasia yanakua na kuimarika,” amesema Mhe. Lombardi 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfredo Fanti wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi jijini Dar es Salaam

 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.