Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali
ya Tanzania imewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani mazingira
mazuri na kuwasihi kuendelea kuwekeza hapa nchini.
Ahadi
hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa
Marekani nchini Mhe. Donald Wright katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaam.
Balozi
Mulamula amesema makampuni mbalimbali kutoka Marekani yameonesha nia ya
kuwekeza katika sekta za nishati, miundombinu, afya na kilimo hususani katika
zao la korosho.
“Katika
kikao changu na Balozi tumejadili na kusisitiza umuhimu wa Kampuni za Marekani
kuwekeza nchini Tanzania.........na Balozi amenihakikishia baadhi ya kampuni
hizo zipo tayari kuwekeza hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula
Aidha,
Mhe. Waziri Mulamula amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania
kujipanga kutumia fursa ya kuuza Marekani bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa
nchini.
Kwa
Upande wake Balozi wa Marekani, Mhe. Wright amesema uhusiano wa Marekani na
Tanzania ni wa miaka mingi na kuahidi kuuendeleza na kuimarisha uhusiano huo.
“Suala
la wawekezaji kuja kuwekeza hapa Tanzania nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa
suala la wafanyabishara na wawekezaji wa Kimarekani kuja kuwekeza hapa Tanzania
ni jambo ambalo nimelipa kipaumbele na ninalifanyia kazi kwa karibu ili
wawekezaji wa Kimarekani waendelee kuja kuwekeza kwa wingi Tanzania,” amesema
Balozi Wright
Katika
tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mulamula amekutana kwa maongezi na Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe.
Dr. Ahmada El Badasui pamoja na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN),
Bw. Zlatan Milišić ambapo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano.
“Tumekubaliana
kukutana na tume za ushirikiano ili tuweze kujadili na kuona ni jinsi gani
tunaweza kuboresha masuala ya biashara na ushirikiano katika maeneo
mbalimbali,” amesema Waziri Mulamula.
Nae
Balozi wa Comoro hapa nchini amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania na
kuhakikisha uhusiano huo unaendelea kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Leo
nimepokelewa na Waziri Mulamula na tumejadiliana masuala ya ushirikiano baina
ya Comoro na Tanzania na pia tumeongelea masuala mbalimbali yanayohusu mabalozi
hapa Tanzania pamoja na maeneo ambayo tutaanza kuyafanyia kazi kati ya Comoro
na Tanzania,” amesema Mhe. El Badasui.
Kwa
upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Milišić
amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili
kuhakikisha inafanikisha malengo ya maendeleo endelevu iliyojiwekea katika
kuwaletea maendeleo watanzania.
“UN
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inafanikisha agenda zake
za maendeleo endelevu,” amesema Bw. Milišić.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata
Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El
Badasui wakati wa maongezi yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini
Dar es Salaam
Balozi
wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El Badasui akimuelezea jambo Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula wakati
wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata
Mulamula (Mb) akisalimiana na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN),
Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Mratibu
Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić akimueleza jambo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata
Mulamula (Mb) wakati wa maongezi yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara
jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.