Friday, September 27, 2024

NJE – SPORTS YAONESHA DIPLOMASIA YA MICHEZO INAVYOTEKELEZWA KWA VITENDO DHIDI YA TAKUKURU

Leo tarehe 27 Septemba, 2024 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo amefika na kujionea Mtanange kati ya Timu ya Nje Sports wanaume na vijana wa kupambana na Kuzuia rushwa TAKUKURU, ambapo kandanda safi na lenye kuonesha namna Diplomasia ya Michezo inavyotekeleswa na Nje– Sports, inayoshiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea Mkoani Morogoro.

Nje – Sports Wanaume pamoja na kuonyesha kabumbu safi mbele ya Mhe. Londo iliadhibu bila huruma Timu ya Takukuru kwa Mikwaju ya Penati baada ya dakika 90 kuisha bila kufungana. Nje – Sport ilifanikiwa kuweka kimiani Penati 7  dhidi ya 6 za Mpinzani wake Takukuru, Wazee wa Kupambana na Kuzuia Rushwa. Kwa matokea Hayo Nje – Sports wanaume wamesonga mbele na kuingia 8 Bora.

Matokeo mengine kwa Upande wa Nje - Sports Kamba wanawake iliyokuwa imekabiliwa na Majuruhi ya wachezaji wake muhimu haikuweza kufua Dafu dhidi ya Timu ya Uchukuzi Wanawake. 

Kunako Mpira wa Netiboli mchezo uliokuwa na mbwembwe zilizo vuta hisia za mashabiki na wapenzi wengi wa mchezo wa Netboli, Nje – Sports wanawake waliokuwa wakipasiana mpira kwa kasi kitu ambacho kiliwashtua wapinzani wake Timu ya Bunge kucheza kwa tahadhari kubwa kitu ambacho kiliwasaidia kuibuka na Ushindi. Nje – Sports walipoteza kwa kufungwa goli 49 – 35.     

Awali, Mhe. Londo alipata fursa ya kuzungumza na wanamichezo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, (Nje - Sports) na kuwaeleza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo amemtuma kuwafikishia salamu zake na kueleza kuwa alitamani sana kuja kujionea namna wanavyo tekeleza Diplomasia ya Michezo kwa vitendo katika Mashindano ya SHIMIWI, hata hivyo anafurahishwa kwa namna Nje – sports inavyo fanya vizuri katika mashindano hayo ukizingatia na yeye pia ni mdau mzuri wa michezo. 

“Kwanza nimekuja kutoa salamu za Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo, kwa vijana wake wa Wizara ya Mambo ya Nje wanaoshiriki michezo hapa yeye Waziri yupo Nje ya Nchi lakini amenituma kuja kuwasilisha Salamu zake za Upendo kwa Vijana wake, pia amewataka vijana wake wawakilishe Wizara katika Michezo hii na kuwa Mfano wa Kuigwa na Wizara na Taasisi nyingine za Serikali.” Amesema Mhe. Londo.

Aidha, Mhe. Londo ametoa rai kwa wanamichezo wote wanaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kutumia msemo wa walatini wenye maana ya “Akili safi inakaa kwenye Mwili Safi”, ambapo alieleza kuwa mwili safi ni pamoja kufanya mazoezi, pia mwili safi hutokana na michezo, hivyo ili mtu uwe na akili safi lazima uushughulishe mwili, na kushughulisha mwili kuna jenga Afya ya mtu na kujikinga na maradhi pamoja na kujenga mahusiano chanya kwa jamii nzima inayomzunguka.

Kwa Upande wa Mwenyekiti wa Michezo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ismail Abdallah, alitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri Londo kwa kufika na kuzungumza na wachezaji. 

“Mhe. Naibu Waziri Tunashukuru sana kwa kutenga muda na kuweza kufika, tunatambua kuwa unaratiba ngumu za shughuli za kitaifa, ujio wako unawafanya wanamichezo kupata hamasa ya kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya SHIMIWI” Amesema Bw. Ismail Abdallah

Pamoja na Mambo mengine, Mhe. Naibu Waziri Mhe. Denis Londo amepanga kukutana na Wanamichezo wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Nje – Sports kwa ajili ya kupata nao chakula cha pamoja na kubadilishana nao uzoefu kwenye maswala ya michezo katika kuimarisha Diplomasia ya Michezo.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.