Rais Mstaafu wa Zanzibar
na Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji, Mhe.
Dkt. Amani Abeid Karume, leo tarehe 11 Oktoba 2024 ametangaza Taarifa ya Awali
kuhusu Uchaguzi wa Rais na Wabunge kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo
tarehe 9 Oktoba 2024.
Katika hotuba yake, Mhe.
Dkt. Karume amesema kuwa uchaguzi nchini Msumbiji kwa kiasi kikubwa umezingatia
kanuni na miongozo ya uchaguzi wa kidemokrasia ya SADC, inayosisitiza katika
haki, uhuru, usawa, na uwazi.
Amesema katika kutekeleza
jukumu lake, misheni hiyo iliangalia masuala mbalimbali muhimu kabla na wakati
wa uchaguzi, ikiwemo hali ya siasa na usalama nchini humo, usimamizi wa
uchaguzi, ripoti za vyombo vya habari kuhusu uchaguzi, na uwakilishi wa jinsia,
ambayo yote yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.
Aidha, Misheni hiyo
imeshuhudia nchi hiyo ikiwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi
chote cha kabla na wakati wa uchaguzi, ambapo kampeni, mikutano ya hadhara na mchakato wa upigaji kura vilifanyika kwa amani,
licha ya changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo, hususan katika jimbo
la Cabo Delgado.
Pia Mhe. Dkt. Karume
ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Msumbiji kwa kuonyesha ukomavu wa
kisiasa na uvumilivu katika kipindi chote cha uchaguzi, akiwataka washindani wa
kisiasa kufuata taratibu za kisheria endapo kutatokea migogoro yoyote kuhusu
uchaguzi.
Pia ametoa wito kwa wadau
mbalimbali kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati mamlaka za usimamizi wa
uchaguzi zikikamilisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi, akiwaomba
kuendelea kuhamasisha amani, uvumilivu, na utulivu kupitia majukwaa mbalimbali
katika kipindi cha baada ya uchaguzi.
Kulingana na Misingi na
Miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021,
misheni hiyo itatoa taarifa ya mwisho kuhusu uchaguzi siku 30 baada ya kutolewa
kwa taarifa ya awali.
Misheni ya SADC,
iliyozinduliwa rasmi tarehe 3 Oktoba 2024, ilipeleka waangalizi 52 katika
majimbo yote 11 ya Msumbiji ili kuangalia uchaguzi.
Mhe. Dkt. Karume
aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya
Siasa, Ulinzi, na Usalama, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza misheni
hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Phaustine Kasike akishiriki mkutano wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Awali ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Msumbiji |
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki mkutano |
Sehemu nyingine ya wadau |
Mkutano ukiendelea |
Mkutano ukiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.