Friday, October 18, 2024

WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MTENDAJI WA ALMA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo tarehe 17 Oktoba, 2024 amefanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Muungano wa Viongozi wa Nchi za Afrika katika kupambana na Malaria (ALMA), Dkt. Joy Phumaphi katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya hususan suala la kutokomeza malaria kwa kuboresha maabara na viwanda vya bidhaa za afya ikiwemo za kupambana na ugonjwa wa Malaria.

Kwa upande wa Waziri Kombo ameipongeza taasisi ya ALMA kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria pamoja na maradhi yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, saratani na kichocho.

Pia, Waziri Kombo ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kufanya kazi na ALMA kupitia Balozi zake za New York, Addis Ababa na Geneva ili kusaidia kusukuma agenda za afya zinazopendekezwa na kufanyiwa maamuzi katika maeneo hayo ya uwakilishi wa kikanda na kimataifa.

“Balozi zetu za Addis Ababa, New York na Geneva zitaendelea kufanya kazi nanyi kwa karibu kwakuwa Serikali inathamini mchango wenu katika kuimarisha sekta ya afya, hivyo msisite kuwasiliana nasi pale tunapohitajika kusaidia kufanya maamuzi kwa maslahi ya uum” Balozi Kombo.

Vilevile, amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele katika suala la kutokomeza malaria kwakuwa tangu ALMA iwekeze jitihada zake nchini, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete amekuwa kinara katika kutokomeza Malaria kupitia taasisi ya ALMA, hivyo jitihada alizozifanya pamoja na viongozi wengine wa Afrika zitaendelezwa ili kuhakikisha malaria inatokomezwa.

Naye Dkt. Phumaphi ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake katika kuimarisha sekta ya afya nchini pamoja na namna ambavyo inafanya vizuri katika matumizi ya kadi ya ALMA inayotumika katika kujipima utendaji na uwajibikaji kwenye mapambano dhidi ya malaria nchini. 

Kadhalika, amemshukuru Waziri Kombo kwa  kuihakikishia ALMA kuendelea kupata ushirikiano kupitia Balozi za Tanzania jijini Addis Ababa, Newyok na Geneva na kueleza kuwa hii ni hatua kubwa kwa ALMA katika kuziwezesha agenda za mapana ya Afrika na kuwezesha kupafa fedha za miradi.

“Tumeomba usaidizi wa Tanzania kwakuwa tuna imani na nafasi yake ya ushawishi katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kwakuwa siku zote imekuwa ikiheshimika na kuungwa mkono katika agenda mbalimbali zenye tija kwa watanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema Dkt. Phumaphi.

Hata hivyo, jitihada zilizofanyika zimewezesha kutokomeza malaria kwa asilimia kubwa hususan Zanzibar katika awamu tatu inasomeka katika taarifa za kiafya kuwa ni eneo huru kwa malaria.

Jitihada nyingine ni pamoja na kuziwezesha taasisi za Tanzania ikiwemoTaasisi ya Afya ya Ifakara kufanya kazi na Kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika “Africa CDC’’ na kuwezesha miradi ya sekta kama za mazingira na kilimo kuzinufaisha jamii katika masuala ya afya mfano, miradi ya kilimo kugawa vyandarua kwa wakulima na miradi ya umwagiliaji kwa wakulima kusaidia jitihada nyingine.

Jitihada hizo zinaendelea pia kwa nchi nyingine za Afrika kwa kufanya tafiti ili kuona maeneo mengine yatakayosaidia jitihada hizo badala ya kutegemea sekta ya afya pekee kusimamia afya ya wananchi ambapo wakati mwingine imekuwa ikielemewa katika bajeti zake kukamilisha malengo ya kutokomeza maradhi.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.