Friday, March 7, 2025

UJUMBE WA SERIKALI YA FINLAND WATEMBELEA MJI WA SERIKALI MTUMBA.

 



Ujumbe wa Serikali ya Finland umetembelea Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma na kukagua kiwanja kilichotengwa kwa ujenzi wa ubalozi wa nchi hiyo katika eneo hilo la Mji wa Serikali.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Finland katika kuhakikisha inaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Tanzania.

Ujumbe huo umeongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen, ambaye aliambatana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting.

Baada ya ukaguzi wa eneo hilo, Bi. Airaksinen alieleza kuridhishwa kwake na mazingira ya kiwanja hicho, akibainisha kuwa kinatoa fursa kwa Finland kuendelea kuimarisha uwepo wake nchini Tanzania.

Aidha, alisifu jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba ili kuwezesha shughuli za kidiplomasia na utoaji wa huduma mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Zitting alisisitiza dhamira ya Finland ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali, hususani katika sekta za maendeleo, biashara, na diplomasia.

Alieleza kuwa hatua ya nchi yake kujenga ubalozi makao Makuu ya Serikali Dodoma ni ishara ya ushirikiano imara kati ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Finland pia ulitembelea maeneo mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba zikiwemo ofisi za serikali na maeneo yanayoendelea kuendelezwa na hivyo kupata  fursa ya kujionea kwa kina mwelekeo wa serikali katika kuimarisha utendaji wa taasisi zake.

Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo ulijumuisha maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ofisi ya Jiji la Dodoma.

Maafisa hao waliwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya Mji wa Serikali na juhudi zinazoendelea kufanywa ili kuhakikisha unakuwa kitovu cha shughuli za serikali na kidiplomasia nchini.

Ziara hii inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Finland, huku ujenzi wa ubalozi wa Finland jijini Dodoma ukitarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo kati ya nchi hizo mbili.



 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Hellena Airaksinen(Kushoto) na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting (kulia).
 








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.