Tuesday, October 24, 2017

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa China nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa China nchini, Mhe.Wang Ke. Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika Ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Mhe. Waziri Mahiga akimpongeza Mhe. Wang kwa kuteuliwa kwake kuja kuiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kwa kuwa Mwakilishi wa kwanza mwanamke kutoka Taifa hilo nchini. Mhe Wange aliwasili nchini Tarehe 22 Oktoba 2017.  


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima (kulia) na Mkuu wa Itifaki, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea mara baada ya makabidhiano.

Maafisa wa Ubalozi wa China nchini waliofuatana na Mhe. Wang wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

Wakijadiliana jambo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bibi. Justa Nyange

Picha ya pamoja.

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizunguzma na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Bi. Inmi Patterson alipofika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 24 Oktoba, 2017.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mary Matari akiwa na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Redemptor Tibaigana wakati wa mazungumzo kati ya Waziri Mahiga na Kaimu Balozi wa Marekani (hawapo pichani).
Mazungumzo yakiendelea. Kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Marekani.

Friday, October 20, 2017

Ujumbe wa Mfalme wa Oman watembelea eneo la EPZA-Bagamoyo

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo akimtambulisha Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi wa Bandari ya Bagamoyo na kupokelewa na uongozi wa Mkoa wa Pwani, tarehe 19 Novemba 2017.

Ujumbe wa viongozi wa Serikali ya Tanzania ukiwa umeongozwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (wa sita kutoka kushoto) na Ujumbe wa Mfalme wa Oman wakiwa katika picha ya pamoja kwenye jiwe la msingi la Mradi huo. kutoka kulia Balozi wa Oman nchini Mhe. Ali Abdullah Al-Mahruqi, Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima.

Mhe. Ndikilo akipokea zawadi kutoka kwa Mhe. Dkt. Mohammed.

Ujumbe wa Mfalme ukipokea maelezo ya Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ambao utahusisha Maendeleo ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) kutoka kwa Mhe. Ndikilo, viongozi pamoja na wataalam wengine alioambatana nao. 

Mwakilishi kutoka Mfuko wa Oman ambao pia ni mbia katika Ujenzi wa Bandari hiyo akitoa maelezo kwa viongozi. Wabia wengine katika ujenzi wa mradi huo ni pamoja na  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China.

===================================
Wakati huo huo Ujumbe wa Mfalme wa Oman ulipata fursa ya kutembelea eneo la kihistoria la Kaole Wilayani Bagamoyo, ambapo waliweza kusikia mengi kuhusiana na historia ya eneo hilo na kujionea maeneo mbalimbali yanayohusisha historia ya Tanzania na Oman.
Mhe. Dkt. Mohammed akinywa Maji katika kisima ambacho maji yake huwa hayakauki na hivyo iliaminika kuwa ukinywa maji hayo unaongeza siku zako za uhai.
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Mhe. Dkt. Mohammed mara baada ya kumaliza ziara yake katika eneo la kihistoria la Kaole.

=======================================
Katika nafasi nyingine Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam sambamba na wanafuzi kutoka katika shule mbalimbali za Mkoa huo walipata nafasi ya kutembelea Meli ya Mfalme wa Oman "Fulk Al salaam." kama wanavyoonekana katika picha.


Mkutano na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Miaka 72 ya Umoja wa Mataifa.

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Suzan Kolimba (Mb) akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari( Hawako pichani) kuhusu maadhimisho ya Miaka 72  ya Umoja wa Mataifa katika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC), tarehe 19 Oktoba,2017, Dar es Salaam, kulia kwake ni Bw. Alvaro Rodriguez Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini na kushoto ni Balozi Celestine Mushy Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa . Mwaka huu siku hii itaadhimishwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam Oktoba 24,2017 , Maadhimisho hayo yatafikia kilele katika tukio litakalofanyika katika Kisiwa cha Unguja, Zanzibar. Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo mwaka huu ni "Maeendeleo ya Viwanda hayana budi kuzingatia Utunzaji Mazingira ili kuleta Maendeleo endelevu".

Baadhi ya maafisa wa Wizara na Umoja wa Mataifa, wakifuatilia mkutano huo, wa kwanza kulia ni Bi. Wendy Bigham - Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Sihirika la Chakula Duniani(WFP), Bw. Jestus Nyamanga Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na mwisho ni Bw. Charles Faini Katibu wa Naibu Waziri.

Thursday, October 19, 2017

Watanzania wahimizwa kudumisha na kuuenzi utamaduni wao

Mgeni rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla (Kushoto) akikaribishwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy (kulia) mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za utamaduni wa muziki wa Oman zilizofanyika tarehe 18 Oktoba 2017.

Kikundi cha ngoma kutoka nchini Oman ambacho ni sehemu ya ujumbe wa Mfalme wa Oman uliopo nchini kwa ziara kikitumbuiza jukwaani.

Mhe. Dkt. Kigwangalla na Mhe. Dkt.Mohammed wakijadiliana jambo.
Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima akifuatilia buruduni iliyokuwa ikitolewa na kikundi cha ngoma kutoka Oman. Wengine ni sehemu ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Oman.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Oman ikifuatilia burudani.
Bendi ya Jeshi kutoka nchini Oman ambayo pia ni sehemu ya ujumbe huo ilitoa burudani kwa wananchi waliohudhuria hafla hiyo.


=======================================================================


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla amewataka Watanzania kuwa mabalozi wazuri katika kuzitangaza na kuzidumisha mila, tamaduni na desturi zao kwakua ndio nguzo na utambulisho wa Mtanzania popote Duniani.

Waziri Kigwangala aliyasema hayo katika sherehe za muziki wa utamaduni wa Oman zilizofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba 2017.

Sherehe hizo ambazo Mgeni rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Kigwangalla, ziliandaliwa na ujumbe wa Mfalme wa Oman uliokuja na Meli ya Mfalme huyo nchini kwa ziara ya siku sita inayotarajiwa kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 21 November 2017.

Mhe. Kigwangala alisema kupitia tamasha hilo la muziki na ziara nzima kwa ujumla, Oman inapata fursa ya kujitangaza na kuutumia utamaduni wao  kama sehemu ya utalii na kwamba hii ni nafasi ya pekee kwa Watanzania kujifunza namna gani watu wa mataifa mengine wameweza kutumia utamaduni wao kwa tija na kuongeza pato la Taifa. 

Aidha, alisisitiza ni wakati sasa makundi yote ya utalii  yaliyopo nchini kama utalii wa kwenye maji, utalii wa misitu hususan kwa kutumia upekee wa mazingira yetu, fukwe na hata historia ya binadamu vikaendelea kuhifadhiwa na kupatiwa ubunifu zaidi wa namna ya kuvitangaza na kupata mfumo wa kisasa kwa ajili ya kuwezesha watalii wengi kuingia na kutoka nchini kwa namna bora zaidi.

Halikadhalika akaongeza kwa kusema “Nchi yetu imebarikiwa sana kwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii ukilinganisha na Oman, katika fursa niliyopata ya kukutana na Naibu Waziri wa Utalii wa Oman ambaye ameambatana na ujumbe huu nimeweza kuzungumza naye mengi ambayo tutayaweka katika utekelezaji ili sekta ya utalii iweze kuongeza fedha za kigeni zaidi.”

Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Bw. Mohammed bin Hamad Al-Rumhy ameahidi kuwa Serikali ya Oman itaendeleza undugu huo kwa kufanya biashara  na kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuweza kuingia katika soko la ushindani duniani.

Lengo kuu la ziara ya ujumbe huo ni kutangaza amani katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na kudumisha undugu uliopo baina ya Tanzania na Oman ambapo utamaduni wa mataifa haya mawili umekuwa ukifanana hususan katika ukanda wa pwani kufuatia historia na muingiliano wa wananchi wake katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Tuesday, October 17, 2017

Taarifa kuhusu kuzingatia sheria katika katika kuingiza au kutoa mifugo nchini kwa ajili ya malisho na maji.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

TAARIFA KUHUSU KUZINGATIA SHERIA KATIKA KUINGIZA AU KUTOA  MIFUGO NCHINI KWA AJILI YA MALISHO NA MAJI

Hivi karibuni, tumeshuhudia kuibuka kwa wimbi kubwa la uungizaji wa mifugo kutoka nchi jirani kuingia nchini kwa ajili ya malisho na maji bila kufuata sheria za nchi. Uingizaji wa mifugo kutoka nchi moja kwenda nyingine una madhara mengi, ikiwemo kiusalama, uharibifu wa mazingira na kueneza magonjwa ya mifugo.

Ikumbukwe kuwa tarehe 13 Oktoba, 2017, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa agizo la kuondoa mifugo yote iliyo nchini kinyume cha sheria ndani ya  siku saba (7). Kutofanya hivyo kutapelekea mifugo hiyo kutaifishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kufuatia agizo hilo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  inatoa wito kwa Watanzania wote wenye mifugo nchi jirani wafuate taratibu za kisheria na kama kuna mifugo kwenye malisho nje ya Tanzania waiondoe mara moja ili kuepusha hasara na usumbufu.

Aidha,  wizara inatoa wito kwa Watanzania hususan wanaoishi Mikoa iliyopakana na nchi jirani kuwa wazalendo kwa kutokushirikiana na raia wa nchi za kigeni kuvunja sheria mbalimbali za nchi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
17 Oktoba, 2017

Monday, October 16, 2017

Meli ya Mfame wa Oman yawasili Jijini Dar es Salam kwa ziara


Meli ya Mfalme wa Oman " Fulk Al Salaam" imewasili leo Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya siku sita inayotarajiwa kumalizika tarehe 21 Oktoba, 2017. Meli hiyo imewasili na Mjumbe Maalum wa Mfalme, Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Mhe. Dkt. Hamad Al Rumphy Mahammed ambaye ameambatana na watu zaidi ya mia tatu (300)  kutoka katika sekta mbalimbali.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akisalimiana na  Mhe. Dkt. Hamad Al Rumhy Mahammed mara baada ya kuwasili katika Bandari ya Dar es Salaam. Pembeni ya Waziri Mwinyi ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashimu Mgandila.

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Waziri Mahammed katika sherehe za mapokezi zilizofanyika Bandarini Dar es Salaam. Pembeni yake ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Charles Mwijage.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Aziz Mlima akisalimiana na Mhe. Dkt. Mahammed.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima akisalimiana na Waziri Mahammed. Pembeni yake ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaniva.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ayoub Mndeme akisalimiana na Waziri Mahammed.

Mhe. Waziri Mwinyi akikaribishwa ndani ya Meli na Mhe. Waziri Mahammed.

Mhe. Waziri Mwinyi pamoja na Dkt. Kolimba wakiwa katika mazunguzo na Mhe. Waziri Mohammed mara baada ya kuingia ndani ya meli.

Balozi Dkt. Mlima akifatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea  baina ya Mawaziri Mwinyi na Waziri Mahammed. Kushoto kwake ni Balozi wa Oman nchini, Mhe. Ali Abdullah Al-Mahruqi.

Viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania na Oman wakijadiliana ndani ya Meli. 

Vikundi vya ngoma vikitumbuiza katika viwanja vya bandari mara baada ya Meli kuwasili.

Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakifuatilia hafla ya mapokezi ya Meli ya Mfalme wa Oman.

Waziri Mwijage akutana na Balozi wa India nchini


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb.) akizungumza na Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya kuhusu kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, viwanda na uwekezaji kati ya Tanzania na India. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Oktoba, 2017. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.), Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. Magabilo Murobi (hawapo pichani).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.) (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima (wa pili kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. Magabilo Murobi (wa kwanza kulia) wakati wa mazungumzo kati ya Mhe. Mwijage na Balozi wa India nchini (hawapo pichani).
Mhe. Dkt. Kolimba akichangia jambo wakati wa mazungumzo kati ya Waziri Mwijage na Balozi Arya.
Mazungumzo yakiendelea

Saturday, October 14, 2017

Taarifa kuhusu ziara ya meli ya Kifalme kutoka Oman nchini

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu ziara ya meli ya Kifalme kutoka Oman nchini

Meli ya Kifalme ya FULK AS SALAAM ya Mfalme Qaboos Bin Said Al Said wa Oman iliyo katika ziara ya kirafiki katika Pwani ya Afrika Mashariki itatia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ziara ya siku sita kuanzia tarehe 16 hadi 21 Oktoba, 2017. Lengo kuu la ziara hiyo ni kueneza ujumbe wa amani, upendo na kuimarisha urafiki uliodumu kwa muda mrefu kati ya Oman na Tanzania. 

Meli hiyo ambayo imeanzia Zanzibar tarehe 12 hadi 15, 2017 inatarajiwa kuja na ujumbe wa zaidi ya watu mia tatu (300) ukiongozwa na Mhe. Mohammed bin Hamad Al Rumhy, Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman ambaye ataongozana na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Umma ya Kukuza Uwekezaji nchini Oman, Dkt. Salim Al Nasser Ismaily na Mhe. Maitha Al Mahrouqi, Katibu Mkuu wa Utalii. 

Mara baada ya kuwasili katika Bandari ya Dar es Salaam, Meli hiyo itapokelewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Hussein Ali Mwinyi (Mb.) na viongozi mbalimbali wa Serikali. 

Aidha, tarehe 17 Oktoba, 2017 kutakuwa na hafla maalum ya chakula cha mchana ndani ya Meli hiyo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. 

Tarehe 18 Oktoba, 2017 kutakuwa na tukio la Muziki wa Kitamaduni utakaopigwa mubashara na Bendi kutoka Oman katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. 

Pia tarehe 19 Oktoba, 2017 wananchi wakiwemo wanafunzi wataruhusiwa kufanya ziara ya kutembelea Meli hiyo kwa utaratibu maalum. Pamoja na kutembelea Tanzania, Kenya ni nchi nyingine iliyopewa nafasi ya kutembelewa na Meli hiyo ya Kifalme. 

Meli hiyo itaondoka Bandari ya Dar es Salaam tarehe 21 Oktoba, 2017 kuelekea Mombasa, Kenya. 

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
14 Oktoba, 2017

Thursday, October 12, 2017

Balozi wa Hispania atembelea Wizara

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Hispania nchini Tanzania Filex Costales, katika mazungumzo yao walizungumzia masuala mbalimbali ya mahusiano kati ya Tanzania na Hispania hususani suala la jimbo la Catalonia kutaka kujitenga na Hispania
Mazungumzo yakiendelea.

Wednesday, October 11, 2017

Tanzania na Cuba kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb.) akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo,alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea
Dkt. Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe.Prof. Polledo, wa pili kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Amerika na Ulaya Bi. Mary Matare, na wa kwanza kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bi. Lilian Kimaro na kushoto ni afisa wa Ubalozi wa Cuba hapa nchini.

=======================================



Serikali ya Tanzania na Cuba zimeahidi kuendelea kuweka mikakati madhubuti kwaajili ya kuimarisha ushirikiano wa siku nyingi ulioasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo Hayati Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castor.

Hayo yamesemwa leo katika mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo walipokutana katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mhe. Kolimba alieleza Cuba imekuwa mdau wa Maendeleo nchini tangu enzi za ukoloni ambapo ilishiriki katika kupigania Ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla na hivyo kuleta undugu baina ya watu wa mataifa hayo mawili.

Aidha, aliongeza kwa kusema “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua jitihada na mchango wa Serikali ya  Cuba katika Sekta  ya Afya kwa kuleta madakatari kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Pia ujenzi wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha ni sehemu ya jitihada za kuwasaidia Watanzania katika kuhakikisha wanakuwa na Afya bora ili kuweza kumudu majukumu yao ya kila siku katika kuliletea Taifa maendeleo” alisema Dkt. Kolimba.

Halikadhalika Mhe. Prof. Polledo alisisitiza kuwa Cuba itaendeleza ushirikiano na Tanzania na kuzidi kuangalia maeneo mengine ya ushirikiano hususani upande wa michezo ambapo nchi hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mchezo wa ngumi pamoja na walimu stadi wa mchezo huo ambao wamekuwa wakitoa mafunzo katika mataifa mengine ya Afrika.

Pia alieleza kutambua mchango wa Tanzania katika Kikao cha 72 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa msimamo wake wa kutaka Cuba kuondolewe vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimekuwa vikikwamisha na kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya Taifa hilo. “ ni wakati sasa Cuba na Tanzania zikaimarisha ushirikiano wake kwa kuhakikisha unakuwa na mafanikio  kiuchumi kwa manufaa ya mataifa hayo” alisema Prof. Polledo