Friday, February 28, 2025

WAZIRI KOMBO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI, AAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akisoma kitabu cha taarifa alichokabidhiwa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amefanya ziara rasmi katika Ubalozi wa Tanzania jijini Lilongwe, Malawi, kwa lengo la kukagua miundombinu ya ubalozi huo, kupokea taarifa za maendeleo, na kusikiliza changamoto zinazokabili shughuli za kidiplomasia.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kombo alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, pamoja na maafisa wa ubalozi, ambapo alipokea taarifa kuhusu hali ya mahusiano ya kidiplomasia, uchumi, siasa, na usalama kati ya Tanzania na Malawi.

Taarifa hiyo ilihusisha pia masuala ya mali za Serikali ya Tanzania zilizopo nchini Malawi, ustawi wa watumishi wa ubalozi, na mchango wa Watanzania waishio Malawi katika maendeleo ya taifa.

Aidha, Waziri Kombo alipokea maelezo kuhusu fursa mbalimbali zinazoweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, hususan katika uwekezaji, biashara za mpakani, na sekta ya utalii.

Akizungumza na maafisa wa ubalozi, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa. Alitoa wito kwa Watanzania waishio Malawi kushirikiana na ubalozi katika kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Balozi Agnes Kayola alimshukuru Waziri Kombo kwa ziara yake na kuahidi kuwa ubalozi utaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya Tanzania.

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akiwa katika kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akiwa katika kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi.



 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) (katikati) akiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini malawi Balozi Agness Richard  kayola (kushoto) na Mkuu wa Utawala (HOC) Bw. David Fupi (kulia).




Mkurugenzi idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Sakila Bujik


 


Thursday, February 27, 2025

TAASISI ZA UMMA NA SEKTA BINAFSI SHIRIKIANENI - WAZIRI KOMBO

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akizungumza na wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa sita wa JPCC kati ya Tanzania na Malawi.

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amezitaka taasisi za umma na sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo endelevu.

Akizungumza na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi, Waziri Kombo alisisitiza kuwa mshikamano wa wadau wa sekta zote ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

"Maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila mshikamano thabiti kati ya taasisi zetu. Ushirikiano wa karibu, mbinu bunifu, na matumizi sahihi ya fursa zilizopo ni nyenzo muhimu kwa mafanikio ya pamoja," alisema Waziri Kombo.

Aidha, alihimiza washiriki wa mkutano huo kutumia majukwaa kama JPCC kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa mataifa yote mawili.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana kwa karibu kupitia vikao kama ili kubaini maeneo mapya ya ushirikiano, kutatua changamoto kwa pamoja, na kuboresha utekelezaji wa miradi iliyopo.

"Ni muhimu kushirikiana kwa karibu, hasa tunapokuwa kwenye majukwaa kama haya, ili kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja na kufanikisha malengo ya maendeleo," alisema Balozi Mussa.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha viongozi na maafisa kutoka taasisi za umma, ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wengine ni Wizara ya Nishati, Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ulinzi na Usalama, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na Idara ya Uhamiaji.

 

 

Meza Kuu katika Picha ya pamoja, katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (wa kwanza kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Habiba Hassan Omar (wa kwanza kulia)
 


 


TANZANIA NA MALAWI ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO KATIKA AFYA NA MKATABA WA KUHAMISHA WAFUNGW




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe.Nancy Gladys Tembo wakisaini Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Afya na Mkataba wa kuhamisha wafungwa.



Tanzania na Malawi zimesaini hati  ya makubaliano katika sekta ya afya na mkataba wa kuhamisha wafungwa , ikiwa ni hatua muhimu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili jirani.

Makubaliano hayo yamesainiwa tarehe 26 Februari 2025 wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) aliyeongoza ujumbe wa Tanzania alisaini makubaliano hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo alisaini pia makubaliano hayo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kombo amesema kusainiwa kwa makubaliano haya ni moja ya mafanikio ya mkutano huo na ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi.

Mhe. Waziri amezihimiza taasisi na sekta husika kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa tija na ufanisi ili kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo, amepongeza hatua hiyo muhimu na kubainisha kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo ni chachu ya mabadiliko katika sekta za afya na haki za wafungwa.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha huduma za afya na kusaidia katika kusimamia haki za wafungwa walioko katika magereza ya mataifa hayo.

Mbali na kusainiwa kwa makubaliano hayo, mkutano huo pia umejadili maeneo mengine ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, yakiwemo biashara, elimu, miundombinu, nishati, na usalama wa mipaka.

Viongozi wa pande zote mbili wameahidi kuhakikisha kuwa uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa hayo unaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wao.

Pia, wamekubaliana kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unapaswa kufanyika kwa wakati ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa  na kuongeza ushirikiano wa pande mbili kwa kiwango cha juu zaidi.

Mkutano huo wa JPCC ulitanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania na Malawi uliofanyika tarehe 25 Februari 2025.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe.Nancy Gladys Tembo wakionyesha Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Afya na Mkataba wa kuhamisha wafungwa.
 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Gladys Tembo

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma(kulia)
 







                                                                      Picha ya pamoja