Mhe. Chiume akiendelea na hotuba ya ufunguzi, kushoto ni Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Stergomena Tax |
Wajumbe wa mkutano. |
Picha ya Pamoja ya Baraza la Mawazri wa SADC. Waliokaa wa kwanza kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum |
Mhe Tax Aainisha mafanikio ya SADC katika kipindi cha mwaka 2013/2014
Na Ally
Kondo, Lilongwe
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Stergomena Tax aeleza
mafanikio ya SADC katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti na Mpango Kazi wa
Jumuiya hiyo kwa mwaka 2013/2014. Mhe. Tax alitoa maelezo hayo mbele ya Mkutano
wa Baraza la Mawaziri wa SADC ambao ni wa kwanza kushiriki tangu alipochaguliwa
kushika wadhifa huo. Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa SADC unafanyika Lilongwe, Malawi na unatarajiwa kukamilika tarehe
11 Machi, 2014.
Mhe. Tax ambaye ni Mtanzania alisema kuwa SADC ilitekeleza
kikamilifu na kwa mafanikio makubwa mpango kazi wa kusuluhisha mgogoro wa
Madagascar. Hivyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Madagascar, kurejeshewa uanachama
wa SADC baada ya kufanya uchaguzi wa amani
kati ya mwezi Oktoba na Desemba, 2013 ambao umerejesha utawala wa Katiba
katika nchi hiyo.
SADC pia katika kipindi hicho, ilituma timu za waangalizi wa
uchaguzi katika chaguzi za Madagascar, Swaziland na Zimbabwe. Katika nchi zote
hizo, waangalizi wa uchaguzi hao walikamilisha majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Sanjari na hayo, SADC imeendelea kujadiliana na COMESA na EAC
kuhusu ushirikiano wa kuanzisha Soko Huru la Pamoja baina ya nchi za jumuiya
hizo. Awamu ya kwanza ya majadiliano hayo yanatarajiwa kukamilika mwaka 2015.
Aidha, SADC inajivunia kuanza kwa utekelezaji wa Itifaki ya
Jinsia na Maendeleo katika nchi wanachama. Itifaki hiyo imeanza kutekelezwa
baada ya theluthi mbili ya nchi za SADC kuidhinisha Itifaki hiyo.
SADC pia inakamilisha Rasimu ya Itifaki kuhusu kuanzisha upya
Mahakama ya SADC.
Katika orodha hiyo ya mafanikio, SADC pia imeweza kuwa na
chombo cha kuandaa miradi ya maendeleo, chombo ambacho kitasaidia kubuni miradi
makini itakayoweza kupata fedha kutoka taasisi za fedha. Sambamba na hili, SADC
imeandaa Mpango Mkuu wa miradi ya miundombinu.
Katika mkutano huo, Mhe. Tax alitaja pia maeneo yatakayopewa
kipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2014/2015. Maeneo hayo ni pamoja na:
kuimarisha soko huru katika nchi za SADC; majadiliano ya utatu wa kuanzisha Soko
huru la pamoja la nchi za EAC, COMESA na SADC; maendeleo ya viwanda na maendeleo ya
miundombinu katika ushirikiano wa utatu (EAC,SADC, COMESA) na utekelezaji wa
Mpango Mkuu wa Kikanda wa Maendeleo ya Miundombinu.
Vipaumbele vingine ni: utekelezaji wa mikakati ya kikanda ili
kuboresha upatikanaji wa uhakika wa chakula (food security); kuhamasisha na
kujenga amani pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala bora katika Kanda ya
SADC; na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.