Mhe. Bernard Membe akiendesha kikao cha 43 cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumiya ya Madola Jijini London Uingereza. |
|
Kikao cha arobaini na tatu
cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola kimeipunguzia adhabu nchi ya
Fiji na hivyo kuiruhusu kushiriki kwenye baadhi ya matukio ikiwemo michezo ya
Jumuiya ya Madola ya mwaka 2014.
Kikao hicho kilichofanyika
Jijini London Uingereza chini ya uenyekiti wa
Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wa Tanzania kilifikia uamuzi huo baada ya kupitia na kuridhishwa na
hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Fiji katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao
ikiwa ni jitihada za kutetea uanachama wake ndani ya jumuiya hiyo.
Akiongoza mjadala huo, Mhe.
Membe alisifu hatua za makusudi zilizochukuliwa na nchi hiyo kama vile kushugulikia
masuala ya haki za binadamu na utawala bora, kuanzisha daftari la kudumu la
wapiga kura, kuandaa mazingira ya uwazi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Septemba
2014 ikiwemo kuandaa mazungumzo na wadau mbalimbali wa siasa na aliyekuwa
Waziri Mkuu aliyeingia kijeshi kujiuzulu na kugombea kama raia.
Akiendesha kikao hicho cha
kwanza kama mwenyekiti wa chombo hicho muhimu, Mhe. Membe alisisitiza umuhimu
wa kikosi kazi hicho kutekeleza majukumu yake bila urasimu na ubaguzi bali kwa
kutoa fursa sawa za ushiriki wa nchi wanachama na kuzingatia misingi ya haki
kwa manufaa ya wanachama wote.
Mhe. Membe pia aliwasisitizia
mawaziri wenzake wanaotumikia chombo hicho kuwa makini na kuheshimu mila na
desturi za nchi wanachama hususan zile za Kiafrika na kuepuka kushinikiza
ajenda ambazo zinagusa dini, tamaduni na mila za nchi nyingi za kiafrika, kama
vile ndoa za jinsia moja. Alisema kwa kufanya hivyo Jumuiya ya Madola itahatarisha
muungano na mshikamano uliopo sasa ndani ya jumuiya hiyo.
Aidha Mhe. Membe alisema
hazina kubwa ya Jumuiya ni wingi wa nchi wanachama na tamaduni na desturi
mbalimbali zinazowakilishwa na wanajumuiya. Hivyo kuheshimu tamaduni zote ndio
kutajenga heshima ya Jumuiya ya Madola kimataifa.
Akiwashukuru wajumbe wa
kikosi kazi kama mwenyekiti, Mhe. Membe alisema jukumu la uenyekiti wa chombo
hicho si dogo, lakini wajumbe wa chombo hicho wakiungana kwa pamoja na kwa
msaada wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola anahakika ndani ya miaka miwili ya
uenyekiti wake Jumuiya hiyo itaendelea kusimamia misingi muhimu ya jumuiya hiyo
bila kutetereka.
Mhe. Membe amewakilisha
Tanzania kama Waziri mwenye dhamana kuanzia mwaka 2011 akiwa kama mjumbe, na
mwaka 2013 Jijini Kolombo Sri Lanka alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti
kwa miaka miwili. Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Mhe. Murray McCully
alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.
Ukiacha Tanzania na New
Zealand, wajumbe wengine ni mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi saba ambazo ni
Cyprus, Guyana, India, Pakistan, Sierra Leone, Visiwa vya Solomon na Sri Lanka
ambao wanaingia kwa nafasi yao ya uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali za Jumuiya ya Madola.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali kwa Umma
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.