TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa
Mambo ya Nje wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier (pichani), atafanya ziara ya
kikazi ya siku moja hapa nchini tarehe 25 Machi, 2014 yenye lengo la kuimarisha
ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani hususan katika
masuala ya biashara na uwekezaji.
Mhe. Steinmeier
ambaye atafuatana na ujumbe wa watu 80 wakiwemo wafanyabiashara kutoka
makampuni makubwa ya Ujerumani, Wabunge, watendaji wa Serikali na Waandishi wa
Habari, ataonana kwa mazungumzo na Mwenyeji wake Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa siku hiyo hiyo katika Hoteli ya
Hyatt Regency, Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yatafuatiwa na Mkutano wa pamoja
kati yake na Mhe. Membe na Waandishi wa Habari (Press Conference).
Akiendelea na
ziara yake, Mhe. Steinmeier atatoa hotuba na kujadiliana masuala mbalimbali na
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Kituo cha Mafunzo ya Sheria
cha Afrika Mashariki kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani(TGCL) katika
Ukumbi wa Nkrumah uliopo chuoni hapo.
Vile vile siku
hiyo hiyo ya tarehe 25 Machi, 2014, Mhe. Steinmeier ataitembelea Kampuni ya STRABAG
iliyopo Ubungo, Dar es Salaam. Kampuni hii kutoka Ujerumani inajishughulisha na
ujenzi wa Barabara za Mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam. Akiwa eneo
hilo Mhe. Steinmeir atakutana na Waziri wa Ujenzi, Mhe. John Magufuli pamoja na
Wawakilishi wa Makampuni ya Ujerumani yaliyopo hapa nchini.
Akiwa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa kuondoka nchini, Mhe.
Steinmeier atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Lazaro Nyalandu kuhusu masuala ya Uwindaji haramu wa wanyamapori Afrika
Mashariki.
IMETOLEWA
NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
24
MACHI, 2014
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.