Friday, December 18, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHE. DKT. AUGUSTINE MAHIGA
 MKOANI ARUSHA
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Arusha kuanzia kesho Jumamosi tarehe 19 Desemba 2015.

Atakapokuwa mkoani Arusha, Balozi Mahiga atafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Richard Sezibera. Mazungumzo yao yatahusu namna ya kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.

Aidha, Mhe. Waziri atatembelea eneo la Lakilaki ambalo limetengwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za taasisi za kimataifa. Ujenzi unaoendelea hivi sasa kwenye eneo hilo ni jengo la ofisi la taasisi ya Mechanism for Crime Tribunals (MICT) inayorithi shughuli za Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambayo itakamilisha shughuli zake tarehe 31 Desemba 2015.

Mhe. Waziri pia atatembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kuonana na uongozi wa Kituo hicho  kwa madhumuni ya kufahamiana. AICC ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Mhe. Waziri atarejea jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili tarehe 20 Desemba 2015.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
18 Desemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.