Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza akimkaribisha Waziri Mahiga alipowasili kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum kwake. Pembeni ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Gamaha. |
Waziri Mahiga akimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Spika, Mhe. Aghaton Rwasa alipokutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Burundi, Mhe.Paschal Nyabenda (aliyekaa kushoto kwa Waziri Mahiga) |
====================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa
Jamhuri ya Burundi kwenye Ikulu yake jijini Bujumbura, Burundi kufuatia maagizo
ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki ikiwa ni hatua ya Tanzania kutafuta suluhu
ya kisiasa ya migogoro iliyojitokeza baina ya Serikali na vikundi vinavyo hatarisha
amani nchini humo.
Kwenye mazungumzo yao yaliyodumu takriban saa mbili,
Mhe. Mahiga alimueleza Rais Nkurunziza azma ya Rais Magufuli kuamsha mazungumzo
ya kisiasa ya kuleta amani na kwamba tayari msuluhishi aliyeteuliwa na Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Kaguta Museveni ameanza maandalizi ya uzinduzi wa
mazungumzo hayo yatakayofanyika Entebe, Uganda tarehe 28 Desemba 2015. Waziri
Mahiga pia alieleza maoni yake kuhusu hali ya utulivu aliyoiona kwa kipindi cha
takriban saa 24 alizokuwa Jjijini Bujumbura na kwamba hakusikia sauti za
milipuko wala silaha zozote.
Mhe. Nkurunziza alimshukuru mjumbe huyo wa Rais
Magufuli na kumhakikishia ushiriki wa Burundi akieleza kuwa mazungumzo ya
Entebe yatasaidia kuleta amani na mshikamano baina ya wananchi wa Burundi. Hata
hivyo Mhe. Nkurunziza alisisitiza kuwa ili mazungumzo hayo yawe na tija ni
lazima yawe muendelezo wa mazungumzo ya ndani ambayo yeye na Serikali yake
wamekwisha yaanza. Aliongeza kuwa ni matumaini yake kuwa makundi yote nchini
humo wataungana kwenye mazungumzo hayo yatakayojumuisha asasi za kiraia,
kidini, vyama vya siasa na makundi mengine ili kujadili mustakabali wa taifa
lao kwa pamoja.
Pamoja na kuridhia ushiriki wa Burundi kwenye mchakato
huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Nkurunziza alieleza kuwa yeye na
Serikali yake wako tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa
kutathmini hali ya usalama nchini mwake. Hivi karibuni Baraza la Amani na Usalama la
Umoja wa Afrika lilitangaza kupeleka vikosi vya askari elfu tano nchini Burundi
kufuatia kile kilichodaiwa kuwa viashiria vya mauaji ya kimbari kama yale
yaliyofanyika nchini Rwanda miaka ya tisini.
Rais Nkurunziza alisema uamuzi huo wa Umoja wa Afrika
umewashtua wao Serikalini na hata Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wanaohoji
sababu za umoja huo kupeleka jeshi kubwa nchini humo. Burundi imekuwa
ikishirikiana na Umoja wa Afrika kwenye ulinzi wa amani ambapo ina vikosi vya
askari zaidi ya elfu sita nchini Somalia na Afrika ya Kati.
Naye Spika wa Bunge la Burundi Mhe. Paschal Nyabenda
alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo wa Umoja wa Afrika. Mhe. Nyabenda
ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD nchini humo alimweleza Mhe.
Mahiga kuwa misingi ya kukataa ukabila imeainishwa kwenye katiba ya nchi hiyo
na makubaliano ya Arusha ambapo inalazimisha taasisi zote ziwe na uwakilishi na
pengine uwiano sawa kati ya Wahutu na Watusi. Akielezea muundo wa Bunge lake
ambalo lina asilimia 60 kwa 40 ya uwakilishi wa Wahutu na Watusi Mhe. Nyabenda
alisema kuwa Makamu wa Kwanza wa Spika Mhe. Agathon Rwasa anatoka kwenye kabila
la Wahutu na Makamu wa Pili wa Spika, Mhe. Edouard Nduwimana anatokea kwenye
kabila la Watusi.
Naibu Spika wa Kwanza wa Bunge hilo Mhe. Agathon Rwasa
ambaye pia alishiriki kwenye mazungumzo hayo alisema kuwa wakati umefika sasa
kwa Burundi kuangalia mbele na kwa manufaa na maendeleo ya vizazi vijavyo.
Alisifu maendeleo aliyoyashuhudia nchini Tanzania ambapo alisisitiza yamekuwepo
kutokana na amani nchini humo.
Akiwa nchini Burundi, Mhe.
Mahiga na ujumbe wake walikutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya
Usalama wa Raia na Mambo ya Ndani ambapo alipokea taarifa ya Waziri Mhe. Alain
Guillaume Bunyoni kuhusu hali ya
usalama nchini humo tangu Rais Nkurunziza alipochaguliwa na chama chake
kugombea tena nafasi ya Urais mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa upande wake Waziri
Mahiga alisifia jitihada zilizowekwa na Wizara hiyo hususan kwenye upande wa
ulinzi wa raia na mali zao na kusisitiza umuhimu wa Wizara hiyo na Serikali
nzima kuwaelezea wananchi na jumuiya za Kimataifa kwa ujumla jitihada za
Serikali kuleta amani nchini humo.
Ziara ya siku mbili ya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania ilianzia Entebe, nchini Uganda ambapo Mhe.
Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Mhe. Dkt Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi
wa Uganda ambaye ameanza maandalizi ya mazungumzo ya amani chini ya uenyekiti
wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
25 Desemba,
2015
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.