Tuesday, December 15, 2015

Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Seiji Kihara yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara hiyo leo.

Walioshuhudia mazungumzo hayo kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mbelwa Kairuki, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi, Mindi Kasiga na Katibu wa Waziri, Bw. Thobias Makoba.
Katikati ni Balozi wa Japani Mhe. Masahau Yoshinda nchini akiwa na Maofisa kutoka Serikali ya Japan.
Mazungumzo yanaendelea.
Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akikabidhi zawadi ya picha kwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan.
Balozi Mahiga akiagana na Mgeni wake Mhe. Kihara.


TAARIFA FUPI YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA KUHUSU UHUSIANO KATI YA JAPAN NA TANZANIA TAREHE 15 DESEMBA 2015


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo leo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Seiji Kihara ambaye aliwasili nchini jana kama Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Japan Mhe.  Shinzo Abe ambapo kesho tarehe 16 Desemba 2015 anatarajiwa kuwasilisha Ujumbe wa Waziri Mkuu wa Japan kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.   Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Pamoja  na kuwasilisha ujumbe kwa Mheshimiwa Rais, mgeni huyo anatarajiwa kuhudhuria hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mkopo wa dola za kimarekani milioni 96 utakaotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wa Kenya na Tanzania wenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka Singida na Manyara kupitia Babati na Arusha mpaka Namanga.


          MAHUSIANO KATI YA TANZANIA NA JAPAN
Tanzania na Japan zimekuwa katika uhusiano na ushirikiano wa karibu mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru wake. Mahusiano hayo yamekuwa yakikua na kuimarika miaka hadi miaka katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, nishati, Kilimo, biashara, viwanda, usafirishaji na uwekezaji.  Kufanyika kwa ziara hii ya Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan ni muendelezo wa kukuza ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.


            MIRADI MIPYA ITAKAYOFADHILIWA NA SERIKALI YA JAPAN



Serikali imeingia makubaliano na Serikali ya Japan kutekeleza miradi mitatu ya ujenzi wa barabara yenye lengo la kupunguza tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam linaloathiri uchumi wa nchi yetu. Miradi hiyo ni pamoja na:



    Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Juu katika eneo la TAZARA (TAZARA flyover):

Mkataba wa ujenzi wa Barabara hiyo tayari ulikwishasainiwa tangu tarehe 15 Oktoba 2015 na ujenzi unategemewa kuanza mapema mwakani.



              Mradi ya Ujenzi wa Barabara ya Morocco – Mwenge

Serikali ya Japan itafadhili upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco ili kuweza kupunguza msongamano wa magari.  Upanuzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.  Tayari Serikali imekwishaanza hatua za mwanzo za ujenzi wa barabara hiyo kufuatia uamuzi wa Mhe. Rais kuelekeza fedha zilizokuwa zigharamie sherehe za uhuru zitumike kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo.


            Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Gerezani mpaka bendera tatu

Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa fedha za msaada kutoka Serikali ya Japan. Ujenzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.



Mbali na miradi ya ujenzi wa barabara, Serikali ya Japan imeingia makubaliano na Serikali ya Tanzania kutekeleza miradi ya umeme kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa matumizi ya wananchi na viwandani kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM.    Miradi itakayotekelezwa kwa ufadhili kutoka Japan ni pamoja na:



 Mradi ya Ujenzi wa Njia ya Kusafirishia Umeme Kenya – Tanzania Power Interconnection Project


Mradi huu una lengo la kuimarisha usambazaji kwa kuuza na  kununua umeme katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Kenya. Ni ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wenye KV400 na urefu wa kilomita 414.5 kutoka Singida na Namanga kupitia Babati na Arusha.

Mkataba wa mradi huu unatarajiwa kutiwa saini baadaye leo Wizara ya Fedha na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi wa  Mambo ya Nje wa Japan.



    Ujenzi wa mradi wa Mtambo wa kuzalisha umeme katika eneo la Kinyerezi (Kinyerezi II power plant project).



Mkataba wa ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 300 huko Kinyerezi ulisainiwa  tarehe 27 Machi 2015 kati ya Serikali na Benki ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Japan (Japan Bank for International Cooperation – JBIC).  Utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa kuanza mapema mwakani.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.