==========================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MAHIGA AONGOZA UJUMBE WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC NCHINI DRC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe Augustine Mahiga yupo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi 13 Oktoba, 2016.
Mhe. Mahiga ambaye anaongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi hiyo yupo nchini humo kwa maagizo ya Mwenyekiti wa Asasi, Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutathmini hali ya siasa ilivyo nchini humo ili kushauri ipasavyo.
Aidha, tathmini hiyo inafanyika kufuatia hali tete ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama nchini DRC iliyochangiwa na maandamano yaliyofanyika tarehe 19 Septemba, 2016 ambayo yaliandaliwa na vyama vya upinzani kwa lengo la kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kutangaza tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Awali misheni hii ilikuwa ifanye ziara kati ya tarehe 4 na 5 Oktoba, 2016, lakini kutokana na ziara ya Kitaifa ya Mhe Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo hapa nchini ililazimu kuahirishwa. Aidha, kufuatia mazungumzo kati ya Mhe Rais John Pombe Joseph Magufuli, na Mhe Rais Jospeh Kabila wakati wa ziara hiyo walikubaliana Misheni hiyo ifanye ziara kwa tarehe hizo.
Hadi sasa Misheni hiyo imeweza kukutana na wadau mbalimbali ambapo imewasisitiza umuhimu wa kushiriki kwenye mjadala ikiwa ni njia pekee ya kuweza kuwakwamua hapo walipo pamoja na umuhimu wa uvumilivu wa kisiasa na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi kwa kipindi watakachokuwa wamekubaliana pamoja.
Wadau hao ni pamoja na Mabalozi wa Nchi SADC walioko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Mhe. Eden Kodjo, Msuluhishi Mkuu wa Umoja wa Afrika; Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wadau wengine ni Muungano wa vyama vilivyosusia kushiriki katika mjadala shirikishi wa kitaifa ( Rassamblement); Muungano wa vyama vinavyounda Serikali (Presidential Majority); Asasi zisizo za kiserikali zinazoshiriki katika mjadala shirikishi wa kiitaifa; Asasi zisizoshiriki katika mjadala shirikishi wa kitaifa na Taaisi za kidini.
Itakumbukwa kuwa, Mkutano wa 36 wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika uliofanyika Mbabane, Swaziland mwezi Agosti 2016 ulimteua Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama. Nchi zingine zinazounda Asasi hii ni Angola (Makamu Mwenyekiti) na Msumbiji (Mwenyekiti anayeondoka).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 11 Oktoba, 2016.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.