Monday, March 8, 2021

KISWAHILI CHAPENDEKEZWA KUTUMIKA RASMI SADC

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Lugha ya Kiswahili imependekezwa kuanza kutumika rasmi katika majadiliano kwenye vikao vya ngazi ya baraza la mawaziri na katika utendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pendekezo hilo limewasilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.

“Sisi kama Tanzania tumependekeza suala la lugha ya Kiswahili kutoka kwenye lugha ya kazi kwenye ngazi ya baraza la mawaziri hadi wakuu wa nchi na serikali wa SADC linabadilika na kuiwezesha lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi kwenye utendaji wa SADC,” Amesema Balozi Ibuge.

Balozi Ibuge ameongeza kuwa, SADC wamekuwa wakitumia lugha za kikoloni kwa muda mrefu na kwa busara za wakuu wa nchi na Serikali wameamua kuanza kwa mpangilio ambapo lugha ya Kiswahili itaanza kutumika katika ngazi ya baraza la mawaziri pamoja na  vikao vya wakuu wa nchi, na kuishusha lugha hiyo kwenye sekta na kuingia rasmi katika matumizi ya SADC.

Kikao hicho ni maandalizi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC unaotegemewa kufanyika tarehe 12, Machi jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao


Mkutano ukiendelea 


Mkutano ukiendelea 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.